loader
Picha

Wajita; kabila lenye asili mchanganyiko

WATU wengi ambao hawajafi ka mkoa wa Mara wamekuwa wakidhani kwamba mkoa huo una kabila moja tu; Wakurya.

Ukweli ni kwamba mkoa wa Mara una makabila mengine mawili makubwa mbali na Wakurya ambayo ni Wajita na Wajaluo. Kabila lingine ambalo linapatikana mkoa wa Mara, hususani katika wilaya ya Bunda ni Wasukuma ambao siku hizi wamesambaa pia katika maeneo mbalimbali wanakoishi Wajita.

Wajita, Wakurya na Wajaluo ni makabila yasiyosikilizana lugha isipokuwa maneno machache na pia yana mila na desturi zinazotofautiana. Kwa mfano, wakati Wakurya wana mila ya kukeketa wanawake, Wajita na Wajaluo hawana mila hiyo. Au wakati wanawake wa Kikurya wanachunga ng’ombe na hata kukamua mifugo, kwa Wajita hiyo ni kazi ya wanaume pekee.

Katika makala haya tutaangalia zaidi kabila la Wajita ambao wanapatikana zaidi maeneo ya Musoma Vijijini (Majita) na wilaya za Butiama na Bunda. Kuna lahaja tatu za Wajita ambazo ni Wajita, Waruri na Wakwaya ambao lugha yao imeathirika zaidi na Wakurya kutokana na kupakana nao.

Hata hivyo, lahaja hizo tatu zinasikilizana zikitofautiana katika lafudhi. Hawa wanapokuwa nje ya mkoa wa Mara wote wanaitwa Wajita. Mbali ya kufanana lugha, wanafanana pia mila na desturi.

Wajita wana muingiliano mkubwa na makabila kama Waha, Wahaya, Wanyankole, Wanyoro, Watoro, Wakerewe, Wahangaza, Wanyambo, Wazinza, Wakara na kiasi wanaingiliana pia na lahaja za Kikurya za Kikabhwa, Kisweta na Kisimbiti. Wakati Rais Yoweri Museveni alipokuwa Chato Julai mwaka jana alisema alikuja, alijiuliza kama jina Chato ambayo iko upenuni mwa Ziwa Victoria inatokana na Obhwato (mtumbwi) akauliza nokumanya obhwato? (Unajua mtumbwi?) Na kama ni Wajita wangeuliza (oumenya obhwato?).

Kadhalika Museveni alisema aliwahi kupita kwenye kivuko cha Busisi na kuuliza maana yake na wakamwambia ni sisimizi. Hata Wajita sisimizi wanaitwa hivyo hivyo; obhusisi. Makabila ambayo lafudhi zao zina uhusiano wa karibu zaisi na Wajita ni Wakarewe, Wazinza na Wahaya. Ingawa Wajita wengi hawajui Kikerewe, lakini inasemekana kuwa asilimia 70 ya Wakerewe wanaongea Kijita kama lugha yao ya biashara.

Koo za Wajita Wajita wana koo nyingi kama Bhajigabha, Bhegamba, Bhatata, Bhagaya, Bharamba, Bhaanga, Bhalinga, Bhaila, Bhalaga, Bhatimba, Bhayango, Bhashora na wengineo.

Na wale wanaozungumza lafudhi ya Kiruri pia wana koo mbalimbali kama Bhatandu, Bhasikwa, Bhashora, Bhatyama, Bhamangi na Bhambogo huku koo kubwa ya Wakwaya ikiwa ni Bhagangaji. Wajita ni watu wachapakazi sana na wasiopenda dhihaka kwenye kazi, wenye msimamo na wenye kupenda utani na wapole, ila wakali sana wanapoonewa.

Shughuli kubwa ya Wajita ni kilimo, uvuvi na ufugaji. Ufugaji wao ni wa kawaida tofauti na wenzao Wakurya ambao huwa na makundi makubwa ya ng’ombe. Wajita wanapenda elimu na ndiyo maana tangu wamisionari walipofika eneo la Rusoli walijenga shule kisha kudahili wanafunzi wa kutosha.

Historia ya Wajita Inasemekana makabila mengi ya mkoani Mara si wabantu asilia lakini walipofika huko wengine walichagua kuzungumza lugha ya kijita inayojulikana kama Kisuguti na lugha nyingine za Mara. Yako maelezo mengine yanayoonesha kwamba baadhi ya Wajita asili yao ni nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Sudan kama Wanubi wa Sudan Kusini na pia Niger kama Wahausa na Nigeria kama Waigbo.

Kuna Wajita wengine wana asili ya Kinilo-Sahara kutoka kusini mwa Sudan. Jina kama Magoti linalotumiwa na Wajita wengi ni jina kubwa pia katika watu wa jamii ya kabila la Wadinka.

Mfano mwingine ni jina la Maiga ambalo ni jina kubwa tangu zama za milki ya Songhai katika nchi ya Niger ya sasa. Kwa ufupi kabila hili limebeba mchanganyiko wa watu wenye asili mbalimbali. Kuna masimulizi pia kwamba Wajita wengi walipokuwa wanashuka kutoka kaskazini mwa Afrika walifanya makazi yao nchini Uganda.

Lakini kutokana na kuvurugwa na tawala za huko za akina Kabaka, wakaamua kuvuka Ziwa Victoria, wenzao ambao leo wanajulikana kama Wakerewe wakabaki visiwani, wengine ndio Wazinza na wale waliofika katika ufukwe wa Ziwa Victoria mkoani Mara ndio Wajita wa leo.

Inasemekana pia jina la mkoa wa Mara linatokana na neno Jabar Mara, mlima mkubwa ulioko Darfur, ambayo si mbali na Kordofan, magharibi mwa Sudan, kwenye jamii ya Wafur na nyinginezo zinazopatikana katika mlima Mara. Jina hilo baadaye lilipewa Mto Mara na kuzaa mkoa wa Mara.

Majina mengi ya vijiji vingi vya Wajita utayakuta pia Rwanda, Uganda na Burundi. Mfano majina hayo ni Rusori, Buringa, Bururi na mengineyo. Baadhi ya majina ya koo za Wajita kama yalivyotajwa hapo juu pia yanapatikana Rwanda, Uganda, Niger na Burundi na hivyo ni rahisi kutambua koo zao kulingana na miiko yao.

Kuna hata miiko ya jamii ya Wajita ambayo pia unaweza kuikuta katika jamii za nchi hizo. Kwa mfano, Wajita wa koo za Rusori wengi kuna aina fulani ya samaki kwa asili walikuwa hawaliwi kama ilivyo katika jamii za nchi nyingine. Hata hivyo, kulingana na mazingira ya siku hizi baadhi ya miiko hiyo haizingatiwi tena.

Mila nyingi za asili za Wajita unaweza pia kuzikuta kwa Wanyoro wengi, Waankole, Watoro na Wanyambo. Kwa Wajita ilikuwa mwiko kuua nyoka kama chatu na kifutu kama ilivyo kwa Wahausa na Waigbo. Lakini siku hizi vijana wa Kijita wameacha mila hiyo wakisema ‘kunasha mairi enu ngaluma bhanu’, yaani hatuwezi kudekeza nyoka kwa kutowaua wakati wanagonga watu! Kuna baadhi ya koo katika Wajita zinaheshimu sana chura kama ilivyo kwa koo kadhaa za Rwanda.

Wajita wenye asili ya Kibantu wapo pia na hawa inasemekana wanatokea katika koo za Bahitira. Mfano Waruri wengi ni Wabantu na wanatokea Bururi na ni kabila ambalo pia liko Uganda. Pia wapo ambao wana asili ya Kush. Mfano: inaaminika Wajita wa kwanza kufika Musoma ni wale wenye asili ya Rusori.

Mpaka sasa wao ni weupe na warefu na pua zao zimechongoka kiasi. Inasemekana pia kwamba hawa siyo Wabantu na wana asili ya Kinubi na makabila ya Ethiopia na wengine pia asili yao wametokea Bunyoro na wengine wakitokea Rwanda na Burundi. Wajita wengi wenye asili ya Banyoro ni warefu sana, ingawa wengine ni weusi siku hizi kutokana na mchanganiko.

Wajita wenye asili ya Unubini na hao wanaotokea Banyoro zamani walikuwa kama Waarabu kwa mbali na wengi ni kutoka Rusori. Watu ambao wametokea Ethiopia wakiwa na asili ya Kushi na wana mwingiliano wa karibu na Watutsi ni Watimba na Watimbaru. Watimba ndio ukoo mkubwa katika kabila la Wajita, ambao asili yao walitokea Hemit, Ethiopia.

Wajita pia walikuwa na utawala wao, ambapo watemi wao walikuwa wa ukoo wa Bhatimba, ambao ni Kusaga, Makunja, Magai, Majinge huku baadhi ya Watemi wa Waruri ikiwa ni pamoja na Mtwenge, Marumbo, Wandwi na wengineo. Dini Wajita wengi ni washika dini. Kati ya madhehebu ambayo yameenea sana kati ya Wajita ni Wasabato.

Wamisionari wa Kisabato walifika Ujitani muda mrefu kueneza dini hiyo pamoja na kujenga shule. Shule za Bwasi, Kasoma na Rusoli zimejengwa na wamisionari wa Kisabato na zilisaidia sana kuwafanya Wajita wengi kwenda shule.

Wajita wengi wanaozungumza lahaja ya Kikwaya ni Wakatoliki wakati Waruri wengi ni mchanganyiko wakiwemo na Waislamu Baadhi ya Watanzania maarufu kutoka kabila la Wajita ni Dk Chinuno Magoti (daktari wa binadamu), Wilson Mukama (aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM), Kangi Lugola (Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani) na Aristablus Musiba (mwandishi wa riwaya).

Wengine Abel Mwanga (mwanasiasa), Charles Kusaga, (mkurugenzi wa hospitali ya Bugando), Joseph Kusaga (mkurugenzi na mmliki wa Clouds Media) Jaji Dan Mapigano, Profesa Sospiter Muhongo (Waziri wa Madini wa zamani) na wengineo. Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali

HAKUNA aliyefahamu jina lake wala asili yake. Hata yeye mwenyewe ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi