loader
Picha

Hospitali Benjamin Mkapa yapongezwa

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kuvuka lengo la kuhudumia wagonjwa 60 wa Kifua Kikuu (TB) lililowekwa na jiji mwaka jana.

Pamoja na huduma hiyo kuanzishwa hivi karibuni, Hospitali ya Benjamin Mkapa imeweza kuwafikia zaidi ya wagonjwa 60 wa TB mwaka uliopita. Kwa mujibu wa barua ya pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Aphonce Chandika, jiji limebainisha kuwa hospitali hiyo imewahudumia wagonjwa 68 ikiwa ni sawa na asilimia 113 ya lengo lililowekwa.

“Pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa kuanzishwa hivi karibuni, huduma kwa wagonjwa wa TB, wameweza kuwahudumia wagonjwa zaidi ya 60 kwa mwaka jana,” imeeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Dk Peres Lukango kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dk Gatete Mahava.

Dk Lukango alisema kwa mwaka huu, halmashauri ya Jiji la Dodoma limeweka lengo la kuwafikia wagonjwa wa TB 100 ifikapo Desemba mwaka huu. Lengo la mwaka jana lilikuwa ni kuwafikia wagonjwa wa TB 60.

“Ninawatakiwa mafanikio mema katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa TB na muweze kufikia lengo la mwaka huu la wagonjwa 100 hadi kufikia Desemba,” alisema.

Naye Mratibu wa ugonjwa wa TB katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Denis Kanyika ameonesha kufarijika kwa jinsi mchango wa hospitali hiyo umetambuliwa na kwamba hospitali hiyo imejipanga kuvuka lengo la mwaka huu la kuhudumia wagonjwa 100.

“Mpaka sasa tumeshaweza kuwahudumia wagonjwa 30, tuna imani kuwa tutafikia lengo la kuhudumia wagonjwa 100 ndani ya mwaka huu,”alisema.

Pia Dk Kanyika alitumia fursa hiyo kubainisha dalili za ugonjwa huo kuwa ni kukohoa kwa muda mrefu, homa, kutokwa jasho usiku na kupungua uzito.

Alisema pia ugonjwa huo unaenea kwa njia ya hewa wakati watu wenye vidudu vya TB kwenye mapafu wanapokohoa, kutema mate, kuongea, kupiga chafya Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2018, robo ya idadi ya watu duniani walimeambukizwa ugonjwa wa TB na maambukizi mapya hutokea kwa asilimia moja ya idadi ya watu duniani kila mwaka na kusababisha vifo vya watu milioni 1.5.

Hii inafanya ugonjwa huo kushika namba moja duniani kwa kuua watu wengi miongoni mwa magonjwa ya kuambukiza na asilimia zaidi ya 95 ya vifo hivyo vinatokea katika nchi zinazoendelea.

Hata hivyo, maambukizi mapya ya ugonjwa wa TB yanaelezwa kupungua kuanzia mwaka 2000 na asilimia 80 ya watu katika nchi za Asia na Afrika wameambukizwa.

BUNGE limeelezwa kuwa kipindi cha pili cha Mpango wa Kunusuru ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi