loader
Corona yatesa viongozi, watu maarufu duniani

Corona yatesa viongozi, watu maarufu duniani

VIONGOZI na watu maarufu duniani wameambukizwa virusi vya corona vinavyosababisha homa ya mapafu. Mlipuko huo ulianzia kwenye Jiji la Wuhan katika Jimbo la Hubei nchini China na kisha kuenea katika nchi mbalimbali duniani.

Kusambaa kwa maambukizi ya virusi hivyo, kumesababisha watu wengi kuugua na pia kufa. Kati ya viongozi na watu maarufu ambao walioambukizwa wamo pia kutoka Afrika.

Kwa Afrika, viongozi walioambukizwa virusi vya corona ni Mnadhimu wa Rais wa Nigeria, Abba Kyari. Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Nigeria kilisema wakati vipimo vya Kyari vikionesha ana maambukizi, vipimo vya Rais Muhammadu Buhari vilionesha hana corona.

Imeelezwa kuwa Kyari amepata maambukizi hayo ya corona baada ya kufanya ziara katika nchi za Ujerumani na Misri hivi karibuni. Burkina Faso, mawaziri wanne wa serikali wamethibitika kuambukizwa virusi vya corona. Msemaji wa serikali nchini humo alisema viongozi hao walioambukizwa ni Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Madini, Waziri wa Elimu na Waziri wa Mambo ya Ndani ambao baada ya kupimwa wamekutwa na maambukizi.

Mawaziri hao kwa nyakati tofauti kupitia mitandao ya Twitter na Facebook walithibitisha kuwa na maambukizi ya virusi vya corona. Mawaziri hao ni Alpha Barry wa Mambo ya Nje, Oumarou Idani (Madini), Stanislas Ouaro (Elimu) na Simeon Sawadogo wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Nje ya Afrika

Mbali na Afrika, viongozi na watu wengine maarufu walioambukizwa ni Sophie Gregoire ambaye ni mke wa Waziri Mkuu wa Canada. Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau alithibitisha kuambukizwa kwa mke wake na yeye mwenyewe kuamua kujitenga kwa siku 14 na kufanya kazi zake kwa njia ya simu na video.

Nchini Iran, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Ali Velayati ana maambukizi ya virusi vya corona baada ya kufanyiwa vipimo. Dk Velayati ambaye ni Mshauri wa Kiongozi Mkuu wa Kidini, Ayatollah Ali Khamenei sasa yuko karantini nyumbani kwake mjini Tehran. Pia Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Massoumeh Ebtekar, Naibu Waziri wa Afya, Iraj Harirchi na wabunge 23 nao wameambukizwa virusi hivyo.

Wabunge wawili wamedaiwa kufa kwa corona. Huko Ulaya, maofisa wa ngazi mbalimbali wa serikali nchini Ufaransa, Uingereza na Italia, nao pia wameambukizwa virusi vya corona. Kati yao wamo wabunge kadhaa wa Ufaransa pamoja na Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo, Franck Riester ambao pia wameambukizwa.

Kutokana na hali hiyo, Rais wa Bunge la Ulaya, David Sassoli, ameamua kujitenga kwa wiki mbili kama tahadhari baada ya kufanya ziara nchini Italia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Naye Waziri Mdogo wa Afya wa Uingereza, Nadine Dorries amekutwa na maambukizi huku Waziri Mkuu, Boris Johnson aliyekuwa katika mkutano na Dorries hivi karibuni akigoma kupimwa akidai hana dalili za maambukizi. Mwanamfalme Charles wa Uingereza (71) naye amekutwa na virusi vya corona na sasa yeye na mkewe wamejitenga nyumbani kwao Scotland.

Naye Rais wa Mongolia, Khaltmaagiin Battulga na maofisa wengine wako katika karantini kwa wiki mbili baada ya kurejea kutoka China ingawa vipimo vinaonesha hana maambukizi. Nchini Hispania, Naibu Waziri Mkuu, Carmen Calvo na mke wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Begona Gomez wamekutwa na maambukizi.

Wengine walioambukizwa Viongozi na watu maarufu walioambukizwa virusi vya corona ni Seneta wa Kentucky nchini Marekani, Rand Paul, Mwanamfalme Albert II wa Monaco, Ufaransa na Waziri wa Madini na Nishati wa Brazil, Bento Albuquerque.

Wengine ni Balozi wa Israel nchini Ujerumani, Jeremy Issacharoff, Mwanasiasa wa Ujerumani, Friedrich Merz (64) aliyefanya kampeni ya kutaka kuongoza Chama cha CDU na Kiongozi Mkuu Chama cha Soka Japan, Kozo Tashima.

Viongozi wengine ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Australia, Peter Dutton, Mwandishi wa Rais wa Brazil, Fabio Wajngarten. Wengine ni Waziri wa Mazingira wa Poland, Michal Wos, huku mshindi mara tatu wa tuzo ya mapishi Marekani, Floyd Cardoz, akifariki kutokana na kuambukizwa virusi vya corona.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e9a210297af8a75583718b85cfc8c82e.PNG

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi