loader
Picha

Madiwani 11 Chadema wakacha kikao cha baraza

MADIWANI 11 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Jimbo la Iringa Mjini wamekacha kuhudhuria kikao maalumu cha baraza maalumu la madiwani wa manispaa hiyo jana hatua iliyomnusuru Meya wake Alex Kimbe kung’olewa madarakani.

Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanamtuhumu meya huyo kufanya makosa yaliyogawanywa katika makundi manne, ambayo kama yatasababisha apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye, anaweza kupoteza kiti.

Hata hivyo, ili wang’olewa madarakani madiwani hao wa CCM 14 watahitaji kuungwa mkono na angalau madiwani wanne kati ya 12 wa Chadema ili kupata theluthi mbili ya kura zinazohitaji kwa mujibu wa kanuni. Kikao cha jana kiliitishwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Ahamed Njovu juzi baada ya kupokea taarifa ya timu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kuchunguza tuhuma zinazomkabili meya huyo kwa mujibu wa matakwa ya sheria.

Hapi aliunda timu hiyo baada ya kupokea taarifa ya tuhuma zinazomkabili meya huyo pamoja na utetezi wake. Kabla ya kuahirishwa kwa kikao hicho, Njovu alisema kwa mujibu Kanuni Namba 9 (II) ya Kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ya mwaka 2015; akidi katika mikutano maalumu ya halmashauri itakuwa theluthi mbili ya wajumbe wote na itahesabiwa kabla ya wakati wa ufunguzi wa kikao.

“Kwa kanuni hiyo theluthi mbili ya wajumbe 26 wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ni wajumbe 17,” alisema Njovu baada ya taarifa kutolewa kwamba wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni 15 ambao kati yao 14 ni wa CCM na mmoja ni meya mwenyewe kutoka Chadema.

Akiahirisha kikao hicho, Meya wa Manispaa ya Iringa aliyekuwa wa mwisho kusaini karatasi ya mahudhurio, alisema “kwa kuzingatia kanuni hiyo tuna upungufu wa wajumbe wawili, kwa hiyo mkutano huu unaahirishwa.”

Kimbe alisema baada ya kuahirishwa kwa mkutano huo hatua itakayofuata ni kwa katibu wa baraza hilo (Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa) kuandika barua kwa waziri mwenye dhamana ili ndani ya siku saba atoe mwongozo wa utaratibu wa kuitisha kikao kingine.

Akizungumzia na waandishi wa habari baadaye kuelezea sababu za madiwani wenzake kutohudhuria baraza hilo maalumu, Meya Kimbe alisema; “Sio kazi yangu kujua kwa nini madiwani wa chama changu hawajahudhuria, sina taarifa zao wala mkurugenzi hana taarifa zao.”

Wakati baraza hilo likishindwa kufanyika kutokana na kutotimia kwa akidi, Kimbe alisema alikwishafungua kesi Mahakama ya Wilaya ya Iringa kupinga mchakato wa kumuondoa madarakani kwa madai haukufuata taratibu.

JAJI Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk Eliezer Feleshi amewataka ...

foto
Mwandishi: Frank Leonard, Iringa

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi