loader
Picha

Hakuna mgonjwa wa ndani wa corona hadi sasa- Ummy

SERIKALI imesema mpaka sasa hakuna maambukizi ya ndani ya virusi vya ugonjwa wa corona, huku wagonjwa waliothibitika kuambukizwa virusi hivyo wamefi kia 13.

Pia kuanzia Januari mwaka huu mpaka sasa, wasafiri 1,890,532 wamefanyiwa uchunguzi wa ugonjwa huo, huku mpaka sasa wasafiri 245 wamewekwa karantini ya lazima kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipozungumzia hali ya ugonjwa wa corona nchini, alipokutana na waandishi wa habari jijini hapa. Ummy alisema katika sampuli 273 zilizochunguzwa ugonjwa huo, sampuli 23 zikiwa za Tanzania Bara na 30 za Zanzibar, ni watu 13 pekee waliothibitika kuwa na virusi vya corona.

Watu watano ni raia wa kigeni na nane ni raia wa Tanzania, ambao wote wanaendelea vizuri. “Wagonjwa hawa wote 13 isipokuwa mmoja walisafiri nje ya nchi katika siku 14 zilizopita kabla ya kuthibitishwa kuugua, na huyu mgonjwa mmoja alipata maambukizi kutoka kwa mtu aliyekuwa nje ya nchi.

“Tunamshukuru sana Mungu kwani hadi sasa hakuna maambukizi ya ndani, hivyo wananchi tuendelee kuchukua tahadhari wakati serikali ikifanya juhudi za kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini,” alisema Ummy.

Akichambua, Waziri wa Afya alisema kati ya watu hao 13, wawili wamekutwa Arusha, wanane Dar es Salaam, Zanzibar wawili na Kagera mtu mmoja ambaye ni dereva wa magari makubwa aliyetokea Burundi.

“Ninafurahi kuwajulisha kuwa mgonjwa wetu wa kwanza wa Arusha amepona baada ya kumpima mara tatu na taratibu za kumruhusu kurudi nyumbani zinaendelea, hivyo sasa Arusha inabaki na mgonjwa mmoja,” alisema akimzungumzia Isabela Mwampamba, ambaye alijitangaza mwenyewe siku chache baada ya serikali kutangaza mgonjwa wa kwanza nchini tangu ugonjwa huo ulipuke Wuhan nchini China, Desemba mwaka jana.

Maabara zaidi kujengwa Alisema katika kuongeza juhudi za kupima ugonjwa wa corona, serikali inatarajia kuongeza maabara sita kwa Tanzania Bara na moja kwa Zanzibar.

Aliongeza kuwa pia kuna haja ya kuongeza maabara. Alisema tayari maabara ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) inaweza kupima sampuli na pia maabara za NIMR Mbeya, Tanga, Mwanza na Arusha na ya Nelson Mandela. Alisema vipimo vya kupima virusi kwa haraka, vitawekwa kwenye hospitali za mikoa, kanda na kwenye mipaka.

Wazanzibari waliopo nje Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed alisisitiza kuwa msimamo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwa ikifika kesho, haitaruhusu kuingia Wazanzibari kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

Hamad Rashid alisema hatua hiyo inatokana na mzigo mkubwa wa wananchi, ambao wamekuwa wakiwekwa kwenye karantini ya lazima.

“Ikifika Jumamosi kama hujarudi baki huko huko, mpaka tuwahudumie kwanza hawa, kwa sasa tumewaweka karantini watu 134, na leo (jana) kuna ndege inashusha wengine hatutaweza kuwahudumia wote,” alieleza.

BUNGE limeelezwa kuwa kipindi cha pili cha Mpango wa Kunusuru ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi