loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanafunzi watumie vizuri muda huu kujisomea

KATIKA kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, imefunga shule zote za awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kwa kipindi cha siku 30.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikiwa ni moja ya mikakati ya serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona nchini. Kutokana na agizo hilo la Waziri Mkuu, sasa wanafunzi wengi wamerejea nyumbani.

Hali iliyopo Tanzania Bara ni hiyo hiyo kwa Tanzania Zanzibar, ambako Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imefunga shule na vyuo kutokana na ugonjwa huo wa corona.

Hivyo, tumevutiwa na kauli ya Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Asiya Iddi Issa alipozungumza na gazeti hili juzi.

Mkurugenzi huyo anataka wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya kidato cha sita, nne na pili, wasibweteke muda huu shule zilipofungwa kwa dharura, badala yake wajisomee vizuri nyumbani.

Kwamba mitihani itafanyika tu ingawa itategemea hali ya ugonjwa wa corona utakavyokuwa.

Na sisi tunasisitiza kuwa kipindi hiki, ambapo shule zote zimefungwa ni muda muafaka kwa wanafunzi kujisomea majumbani na kubadilishana maarifa katika masomo yao, ikiwemo kujindaa kwa mitihani ya taifa. Tunawaomba wanafunzi, hasa wanaotarajiwa kufanya mitihani ya kitaifa, wajaribu kutumia muda huu kusoma kwa bidii.

Huu si wakati wa kupoteza muda, bali ni fursa nyingine ya kujisomea kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo ya mitandao. Siri ya kufaulu katika mitihani ni kusoma na kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mitihani.

Wanafunzi wanaweza kujisomea kupitia maktaba na mitihani iliyopita inayotungwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), ambayo inapatikana katika mitandao.

Pia, ni jukumu la wazazi kuhakikisha kuwa watoto wanatumia muda huu kusoma na kujifunza wakiwa nyumbani.

Njia pekee ya kuwafanya wanafunzi wasio na mitihani, na wanaokabiliwa na mitihani kuendelea vizuri, ni kwa wanafunzi wote kutumia siku 30 za mapumziko kusoma kwa bidii na kurejea mambo yote waliyojifunza darasani.

Jambo lingine ni wazazi wahakikishe kuwa watoto wao, ikiwemo wanafunzi, wanakwepa mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje ambayo imezuiwa na serikali. Mikusanyiko hiyo ni shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali, shughuli za kisiasa na nyinginezo za kijamii.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi