loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera hoteli kusitisha huduma kupisha corona

IMERIPOTIWA kuwa baadhi ya hoteli kubwa nchini, zimeanza kusitisha huduma zake kutokana na tishio la virusi vya corona (COVID-19) vinavyosababisha homa ya mapafu.

Imeelezwa kuwa kufungwa kwa hoteli hizo, kunatokana na kile kilichoelezwa kuwa homa hiyo haina tiba wala kinga, lakini pia kupungua kwa idadi ya wageni kutoka nje ya nchi, baada ya mashirika mengi ya ndege duniani kusitisha safari zake.

Mathalani, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Hoteli ya Sea Cliff Court (Hotel & Luxury Apartments), Ilona Kadri, amesema kupitia taarifa yake kwa wasambazaji, wageni na wadau wa hoteli hiyo kuwa huduma katika hoteli hiyo, zitasitishwa kuanzia kesho kutokana na tatizo hilo la virusi vya corona.

Amesema kutokana na hoteli yao kukumbwa na hali ya mdodoro wa kifedha usiotarajiwa kutokana na hofu ya virusi vya corona, wameamua kuifunga kwa muda mpaka hapo hali itakapotengamaa. Amesema wanasikitishwa na uamuzi huo kutokana na kutambua kwamba utawaathiri wasambazaji, wageni na wafanyakazi. Hata hivyo, amesema wanafuatilia hali hiyo kwa karibu.

Alisema mambo yatakapokaa sawa ikiwemo kuondolewa kwa zuio la safari, wataifungua mapema iwezekanavyo na kurudi kwenye biashara kama kawaida.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli za Serena Afrika, Mahmud Jan Mohamed, amesema katika taarifa yake kuwa wamezifunga hoteli na kambi zao zilizopo Ziwa Manyara, Ngorongoro, Serengeti, Kirawira na Mbuzi Mawe kutokana na tishio la virusi vya corona.

Anasema wamekuwa wanafuatilia tatizo la COVID-19 kwa karibu pamoja na athari zinazojitokeza katika biashara yao na kwingineko barani Afrika. Anaongeza kuwa ni vigumu kujua athari za kibinadamu na kifedha, ambazo zitasababishwa na virusi vya corona duniani kote katika sekta ya hoteli.

Mkurugenzi huyo anasema kutokana na matarajio ya biashara kwenda ndivyo sivyo pamoja na maelekezo ya serikali na itifaki, menejimenti ya hoteli hiyo inazingatia kwa kipaumbele cha pekee katika kuwalinda wafanyakazi, wategemezi wao na ubora wa maisha yao.

Amesema uamuzi huo, utapitiwa upya pale nchi zitakapokuwa zimefungua mipaka yake na kurejea kwa uhakika wa soko la biashara ya hoteli.

Kwa dhati tunapongeza hatua ya hoteli kubwa, kuamua kufunga biashara zao kutokana na hofu ya maambukizi ya corona, kutokakana na ukweli kuwa wageni wengi kutoka mataifa yaliyoathirika na ugonjwa huo, wangeweza kuingia na kufikia katika hoteli hizo na kusababisha maambukizi.

Ni matumaini yetu kuwa hoteli nyingine, ambazo hazijafunga biashara na zinapokea wageni kutoka nje, zitaiga mfano huo wa kufunga hoteli na zitachukua hatua madhubuti, kuhakikisha kuwa zinadhibiti wageni kuingia katika hoteli zao ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi