loader
Picha

Sheria yamwongezea nguvu Katibu Mkuu Kiongozi

MAREKEBISHO yaliyofanyika katika Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, yamempa Katibu Mkuu Kiongozi mamlaka ya mwisho ya uhamisho wa watumishi wa umma, hivyo kutopingwa au kutotenguliwa na mamlaka nyingine.

Majibu hayo yalitolewa bungeni jana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika swali la Mbunge wa Tanga Mjini, Musaa Mbarouk (CUF), aliyetaka kujua kama kumpa Mamlaka ya Mwisho Katibu Mkuu Kiongozi hakutasababisha ukiritimba katika uhamisho wa watumishi wa umma.

Katika majibu ya swali hilo, yamebainisha kuwa Sheria hiyo ya Utumishi wa Umma Sura 298, imefanyiwa marekebisho katika Kifungu cha 4(3) kupitia Kifungu cha 69 cha Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 13 ya Mwaka 2019 kwa kumpa Katibu Mkuu Kiongozi Mamlaka ya Mwisho ya Uhamisho.

“Hii imezingatia Mamlaka yake kama Mkuu wa Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 4(2) cha Sheria hii, pamoja na Mamlaka hayo, Kifungu cha 8(2) cha Sheria hiyo kinampa Katibu Mkuu (Utumishi) Mamlaka ya kuwa Msaidizi Mkuu wa Katibu Mkuu Kiongozi,” ilieleza Ofisi ya Rais, Utumishi.

Hata hivyo, katika kutekeleza majukumu ya Katibu Mkuu Kiongozi, Kifungu cha (3)(h) cha sheria husika kinampa Katibu Mkuu (Utumishi) mamlaka ya kuhamisha watumishi wa umma kutoka taasisi moja kwenda nyingine Tanzania Bara.

“Ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Katibu Mkuu (Utumishi) amekasimu Mamlaka yake kwa Katibu Mkuu (Tamisemi) ili aweze kuhamisha Watumishi wa Umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,” ilisema.

Vilevile, ilisema Katibu Mkuu (Utumishi) amekasimu Mamlaka yake kwa makatibu tawala wa mikoa ili kuhamisha Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika mikoa yao.

“Pamoja na kukasimisha mamlaka yake, Katibu Mkuu (Utumishi) anaweza kuhamisha watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yeye mwenyewe pale inapobidi,” ilielezwa.

Aidha, majibu ya swali hilo yamebainisha kuwa Mamlaka hayo yatatumika kwa kuzingatia maslahi mapana katika utumishi wa umma au pale ambapo Katibu Mkuu Kiongozi hakuridhika na uhamisho uliofanywa na Mamlaka nyingine zilizopewa au zilizokasimiwa madaraka hayo kama ilivyoelezwa.

CHAMA cha ADA- Tadea kimesema kitendo cha Mbunge wa Kawe, ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi