loader
Picha

Majaliwa ataja mambo 10 ya mkazo 2020/2021

SERIKALI imesema katika mwaka wa fedha 2020/2021, imeweka mkazo katika masuala 10 ikiwamo kuimarisha na kudumisha amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo ili kuleta maendeleo endelevu hususan katika kipindi cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020.

Pia serikali itaweka mkazo kwenye kulinda uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe bila kuingiliwa; mipaka ya nchi; haki; kuimarisha ujirani mwema na kuunga mkono sera ya kutofungamana na upande wowote kama dira na msimamo wetu katika mahusiano na nchi nyingine katika Jumuiya ya Kimataifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana bungeni jijini hapa wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2020/2020. Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh 312,802,520,000 kwa ajili ya ofisi hiyo na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh 88,429,156,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh 224,373,364,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Majaliwa pia aliomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh 121,786,257,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, kati ya fedha hizo, Sh 113,567,647,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 8,218,610,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Alisema serikali pia itatilia mkazo katika kudhibiti upotevu wa mapato kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na utoaji huduma hususan kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuondoa urasimu usio wa lazima pamoja na kuwahudumia wananchi wote kwa tija bila ubaguzi wa aina yoyote.

Alisema pia inatilia mkazo katika kuendelea kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji. “Serikali itatilia mkazo katika kuhimiza uwajibikaji wa watendaji wa serikali katika ufuatiliaji wa miradi ya kielelezo hususan ujenzi wa miundombinu muhimu ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo reli, bandari, ujenzi wa meli, vivuko, viwanja vya ndege, barabara na madaraja.

“Pia kuwatumikia Watanzania wote kwa kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa kukamilisha na kuendelea na ujenzi wa miradi ya miundombinu ya maji, afya na elimu,” alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema pia serikali itahakikisha inaimarisha uzalishaji na usambazaji wa nishati ya uhakika kwa kukamilisha Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa MW 2,115 la Julius Nyerere na kuhakikisha vijiji vilivyobaki katika utekelezaji wa mradi wa REA III vinapatiwa umeme.

“Pia kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi, mashamba na maeneo ya makazi, uwekezaji na ujenzi wa viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira zaidi kwa Watanzania, kusimamia kikamilifu matumizi sahihi na yenye tija ya rasilimali zilizopo ili zitumike kwenye maeneo yanayochochea ukuaji uchumi na utoaji huduma bora kwa wananchi,” alifafanua.

Aliongeza, “Pia kuhimiza Watanzania kufuata maelekezo ya serikali kuhusu kujikinga, kudhibiti na kutosambaza virusi vya Corona ili kupunguza athari za kijamii na kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na maambukizi hayo. Serikali kwa upande wake inashirikiana kwa karibu na jumuiya za kimataifa katika kukabiliana na kutokomeza maambukizi ya virusi hivyo vya corona.”

Alitoa wito kwa kila mwananchi kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa.

Alisema katika kufanikisha hayo, serikali imejipanga kwa kuanisha vipaumbele kadhaa muhimu vilivyojikita katika masuala makuu manne kwa kuzingatia Sera na Miongozo. Waziri Mkuu alisema serikali imeweka vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2020/2021 ambavyo vimejikita katika masuala makuu manne.

Aliyataja masuala hayo kuwa ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo.

Waziri Mkuu alisema Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021 yamezingatia Sera na Miongozo ikiwa ni pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/2021 na kuwa ni Mpango wa mwisho katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka wa kutekeleza Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.

CHAMA cha ADA- Tadea kimesema kitendo cha Mbunge wa Kawe, ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya na Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi