loader
Picha

…Ataja mafanikio lukuki ndani ya miaka 5

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano mafanikio makubwa yamepatikana na yamesaidia kuimarisha hali ya kiuchumi na kijamii katika taifa hili.

Alieleza mafanikio hayo wakati akiwasilisha hotuba yake kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya bunge kwa mwaka 2020/2021.

Alisema Rais Dk John Magufuli kifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, aliwaahidi wananchi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawatumikia na kuwajali. Waziri Mkuu alisema katika kutekeleza azma hiyo, ndani ya kipindi cha takribani miaka mitano mafanikio makubwa yamepatikana na yamesaidia kuimarisha hali ya kiuchumi na kijamii kwenye taifa.

Aliyataja mafanikio hayo kuwa ni ujenzi wa miundombinu muhimu ya kiuchumi hususan ya usafiri na usafirishaji sambamba na uimarishaji wa huduma muhimu za kijamii ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele.

Aliyataja kuwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa, ufufuaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ufufuaji wa mali za ushirika mfano, UCU SHIRECU na Mamlaka ya Mkonge Tanzania na ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere.

Alisema pia ulinzi wa maliasili na rasilimali na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, afya na maji ni kati ya hatua za msingi zinazochukuliwa na serikali katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, katika kipindi cha miaka mitano, miradi hiyo muhimu iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kutoa mfano wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa ambao hadi Machi 2020 umetumia Sh trilioni 2.96 na kukamilika kwa asilimia 75 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na asilimia 28 kwa kipande cha Morogoro hadi Makutupora.

Alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huu umewezesha utoaji wa zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 664.7 kwa wazabuni na wakandarasi wa ndani 640. Aidha, ajira zipatazo 13,177 za kitaalam na zisizo za kitalaam zimezalishwa na kati ya hizo, ajira za kitaalam kwa wazawa ni asilimia 46.5 ikilinganishwa na asilimia 53.5 ya wageni.

Waziri Mkuu alisema serikali inatumia gharama kubwa kujenga miundombinu hiyo wezeshi ya kiuchumi kwa lengo la kulifanya taifa kuwa na uchumi imara wa kujitegemea na wenye kuhimili ushindani na kuwa fedha hizo pia zimekuwa chanzo cha ajira na zabuni kwa watanzania zinazowasaidia kuongeza kipato.

Alisema mradi huo utakapokamilika utaongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria pamoja na kupunguza gharama za uchukuzi na kuwa utachochea ukuaji wa miji na sekta nyingine kama vile kilimo, viwanda, utalii na biashara na vilevile, mradi huo utakuwa chanzo cha ongezeko la mapato ya serikali yatakayosaidia katika kuboresha maslahi ya watumishi na huduma za kijamii kama vile afya, elimu na maji.

Alisema ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere litakapokamilika litazalisha umeme wa megawati 2,115 na hadi Machi, 2020, mradi huo umegharimu Sh trilioni 1.28 na umekamilika kwa asilimia 10.74.

Alisema serikali imefanikiwa kutekeleza Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA), na vijiji vilivyounganishiwa umeme nchini vimeongezeka kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015 hadi vijiji 9,001 mwezi Machi, 2020 na kuwa mradi huo pia umezinufaisha taasisi 11,128 zikiwemo za elimu, afya, dini, mashine za kusukuma maji na huduma za biashara.

Alibainisha kuwa katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga, serikali inaendelea kuiimarisha ATCL na hadi kufikia Machi, 2020 tayari ndege nane mpya zenye thamani ya Sh trilioni 1.27 zimepokelewa na kuanza kazi na kuongeza kuwa malipo ya awali ya Sh bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine tatu mpya yamefanyika.

“Ununuzi wa ndege hizi, umeongeza ufanisi katika usafiri wa anga, kuongezeka kwa mapato ya Serikali, kuimarika kwa utalii na kuongezeka kwa fursa za ajira katika sekta ya huduma,” alisema.

Aliongeza kuwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi imeongezeka kutoka Sh bilioni 31 kwa Mwaka 2015 hadi Sh bilioni 269 kwa mwaka 2019. Serikali pia imegharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya kwa kujenga zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za halmashauri za wilaya 69 na hospitali za rufaa za mikoa.

Katika eneo la elimu, serikali imeongeza mikopo kwa ajili ya elimu ya juu kutoka Sh bilioni 365 mwaka 2015 hadi Sh bilioni 450 mwaka 2019. Elimumsingi bila Ada nayo imetekelezwa kwa mafanikio makubwa na kuhakikisha watoto wote 1 5 wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kupatiwa elimu.

Alisema maboresho yanayofanyika kwa upande wa elimu ya msingi yanazingatia uhitaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia. Kuanzia mwaka 2015 hadi Februari, 2020 vyumba vya madarasa 166,627, maabara 5,801, nyumba za walimu 57,541, matundu ya vyoo 231,612 yamejengwa na madawati 2,886,459 yamenunuliwa.

Aidha, idadi ya shule za msingi zenye madarasa ya elimu ya awali imeongezeka kutoka madarasa 16,889 mwaka 2015 hadi kufikia madarasa 17,771 mwaka 2020.

Kadhalika, idadi ya shule za sekondari imeongezeka kutoka shule 4,708 mwaka 2015 hadi shule 5,330 mwaka 2020. Kuhusu maji, alisema serikali imetekeleza ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji 1,423. Kati ya miradi hiyo, 792 imekamilika ikihusisha miradi 710 vijijini na miradi 82 mijini na pia serikali ilipokea ombi la wabunge na kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Maji na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Alisema ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa Sh trilioni 1.3 mwaka 2019, likichangiwa na hatua za makusudi zilizochukuliwa na serikali hususan kuimarisha matumizi ya mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki, kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato.

MTANDAO wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) umesema wasichana 40 ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi