loader
Picha

Makonda atoa maagizo 8 kudhibiti Corona

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa maagizo manane kudhibiti corona ikiwamo kuruhusu bodaboda na bajaji kubeba abiria katikati ya jiji, kuomba serikali itoe mabasi 200 ya mwendokasi yaliyoegeshwa na kunyunyiza dawa ya kuua virusi na wadudu kwa helikopta jijini humo.

Aidha, ameziagiza mamlaka za usafiri mkoani humo kufupisha safari ndefu za daladala na kutangaza leo kabla ya saa saba mchana akiwasihi wamiliki wa nyumba, majengo na mabanda ya biashara, wapunguze pango la nyumba kwa asilimia 50 kwa kuwa biashara nyingi sasa hazifanyiki kama ilivyokuwa kawaida.

Makonda aliyasema hayo jana alipozungumza na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika eneo la Kituo cha Mabasi (Daladala) cha Makumbusho kuhusu hatua mbalimbali ambazo mkoa huo unachukua kudhibiti maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Alisema ili kupunguza msongamano na watu kuchelewa kazini, sasa ameamua kuruhusu bajaji na pikipiki zote zibebe abiria mpaka maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam na mengineyo na kuwasisitiza kuzingatia sheria za usalama barabarani, kutopita kwenye njia ya mwendokasi na kuvaa kofia ngumu.

Kuhusu mabasi ya mwendokasi, alisema kuna mabasi 200 Bandari Kavu Ubungo na amemwandikia barua Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kumwomba aruhusu yaingie barabarani kubeba abiria ili kuwapunguzia wananchi kero na kuondoa msongamano.

"Ndugu zangu hili la Mwendokasi lipo nje ya mamlaka yangu lakini nimemwandikia barua Waziri mwenye dhamana (Jafo) aruhusu mabasi hayo, si chini ya 200 yamepaki Ubungo Bandari kavu, nafahamu yana mgogoro lakini kwa tatizo hili yabebe abiria wa Ubungo, Kimara na Mbezi,” alisema Makonda.

Makonda alisema hatua ya kunyunyiza dawa iliyoanza maeneo mbalimbali wakitumia magari ya Serikali, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Polisi ni endelevu na ili kuyafikia maeneo yote ya mkoa, sasa watatumia helikopta kudhibiti corona, mbu wa malaria, dengue na wadudu wengine wote hatari kwa afya ya jamii.

Makonda aliagiza mamlaka inayopanga safari za daladala ya Latra (Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini) ikae na Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa) wabadilishe 'ruti' daladala ziende umbali mfupi, ziwe za kutosha barabarani na abiria wote wakae na kuwahi kazini. “Nimeona changamoto ya usafiri.

"Mfanyakazi anayetoka Mbezi Mwisho, anatakiwa kwenda kazini Posta. Anayetoka Goba, Tegeta, Mbagala, Chanika, Gongo la Mboto, Pugu anatakiwa afike katikati ya mji kufanya kazi, akikaa kwenye basi 'level seat' daladala inayotoka Mbagala kwenda Kawe, itabidi apaki gari kwa hasara," alisema.

Aliagiza hatua hiyo ya kufupisha safari za daladala ifanyike haraka na uamuzi wake kutangazwa kabla ya leo saa saba mchana na Latra wasipofanya hivyo, yeye (Makonda) ataandaa ratiba yake na kuitangaza. Alisema hatua ya kukaa katika daladala itakuwa endelevu hata baada ya janga la corona kuisha nchini.

“Janga hili halina tajiri, masikini wala mtu mwenye elimu. Kila mmoja awe na nia thabiti ya kujikinga. Hatuna sababu ya kubanana kwenye daladala, tulindane na kufuata maelekezo na masharti bila shuruti,” alieleza.

Eneo lingine alilogusa Makonda ni pango la nyumba. Aliwaomba wamiliki wa majengo, nyumba na mabanda ya biashara na za kuishi Jijini Dar es Salaam kupunguza kodi kwa asilimia 50 ili kuwawezesha wafanyabiashara na wafanyakazi kukabili hali zao za uchumi zilizoyumba kutokana na Covid-19.

"Wapo watu wamepanga, chumba kimoja au viwili, maofisi na apartment, nimejaribu kuongea na baadhi ya wamiliki wa majengo tayari wamiliki 50 wamekubali, rai yangu kwa wenye nyumba, vibanda washushe kodi kwa asilimia 50 kwa miezi mitatu kuwezesha wananchi wamudu hali ya maisha kwa sasa.

“Biashara nyingi sasa ni changamoto, lakini biashara ya nyumba ni matokeo ya mtu kufanya biashara nyingine. Ninawaombeni wenye nyumba, majengo wote mkubali. Sitangazi bei mpya ya kupanga, ni ombi. Jukumu langu ni kusemea wananchi wa kawaida," Makonda alitoa rai kwa wenye nyumba.

Aliwataka wanaume na wazazi kutulia nyumbani na watoto wao kwani Serikali ilifunga shule ikiamini wazazi wanaweza kuwalinda watoto hivyo kama ni disko, wanaume wacheze nyumbani na familia zao. Makonda alisema serikali inasimamia wageni wanaoingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kukaa karantini siku 14 lakini tangu Machi 28 ndege nyingi zilisitisha safari.

CHAMA cha ADA- Tadea kimesema kitendo cha Mbunge wa Kawe, ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi