loader
Picha

Aliyekuwa Mwenyekiti ACT- Wazalendo ajivua uanachama

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Yeremia Maganja(pichani) ametangaza rasmi kujivua uanachama wa chama hicho, na kusisitiza kuwa hivi karibuni pamoja na wenzake (hakuwataja) watatangaza rasmi chama cha siasa watakachojiunga nacho.

Pia mwanasiasa huyo ambaye pia alikuwa Mshauri wa ACTWazalendo, alimtupia lawama Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto kwamba amekuwa akiendesha kwa utashi wake binafsi. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Maganja alisema alijiunga na chama hicho akiwa kama mwathirika wa ukosefu wa demokrasia na ubaguzi aliofanyiwa katika vyama alivyokuwemo kabla.

“Tulipoanzisha ACT-Wazalendo tuliweka mambo muhimu katika Katiba na miongozo yetu ili kujenga chama kama taasisi tenganifu na viongozi na makundi…tuliamini katika uhuru wa kufanya maamuzi kupitia vikao rasmi vya chama bila ghiliba, ulaghai au mashinikizo,” alisema Maganja.

Alisema bahati mbaya uongozi wa chama hicho umeendelea kuwa dhaifu na umekuwa ukimtegemea mtu na si uongozi wa kitaasisi. “Utashi binafsi ndio maamuzi ya chama,” alisema.

Alitolea mfano uchaguzi wa ndani uliofanyika Machi 14 hadi 16, mwaka huu ulionesha kuwa tayari viongozi waliotangazwa walikuwa wamechaguliwa kabla.

“Kwa nini mtu atangaze kugombea nafasi fulani, lakini wakati wa kurudisha fomu anarudisha fomu ya nafasi tofauti… pia kwa nini wengi wajiondoe wakiwa tayari ndani ya ukumbi wa uchaguzi, lakini wapewe teuzi mbalimbali. Ni dhahiri uhuru wa uchaguzi na utashi wa kugombea vilikosekana,” alisema Maganja.

Akizungumzia kujiunga ndani ya chama hicho kwa Mwenyekiti wa sasa wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake, alisema chama hicho kiliamini kuwa kimepata neema, lakini miezi michache wakagundua kuwa kundi hilo halikujifunza kutokana na yaliyowakuta huko nyuma.

“Maalim na timu yake wao wana ajenda yao, ajenda hiyo ni mamlaka kamili ya Zanzibar, chama chochote watakachoingia hata kwa akina Profesa Ibrahim Lipumba walichotaka ni kuhakikisha kuwa kitovu cha mamlaka na maamuzi, ushawishi na rasilimali vinakuwa Zanzibar na si kwingineko,” alisisitiza Maganja.

Alisema kutokana na hali ilivyo ndani ya ACT-Wazalendo ameamua kujivua uanachama tangu jana na anapitia vyama 19 vya siasa vilivyopo na kisha atatangaza anajiunga na chama gani kuendelea na siasa.

WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),akiwemo Wilfred ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi