loader
Picha

Tembo wanavyopamba Hifadhi ya Ruaha

“TEMBO ndiye mnyama anayeongoza kwa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu duniani huwa habadilishi njia ya kupita yaani akishapita, basi hata kizazi na kizazi kitaendelea kupita hapo hapo.”

Ndivyo anavyosema Ofisa wa Shirika la Uhifadhi na Utafiti wa Tembo (STE) lililopo mkoani Iringa, Frank Lihwa wakati akizungumzia utafiti kuhusu tembo unaofanywa na shirika hilo. Kimsingi, tembo ni mmoja wa wanyama vivutio vya asili vilivyopo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mkoani Iringa.

Taarifa kutoka vyanzo kadhaa vya kimtandao zinasema hifadhi hii ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,226 na kwamba, ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote nchini na ya pili kwa ukubwa katika Afrika baada ya Hifadhi ya Kafue iliyopo nchini Zambia.

“Hifadhi hii ina idadi kubwa ya tembo wanaokusanyika katika eneo moja kuliko eneo lingine lolote Afrika Mashariki,” kinasema chanzo kimoja na kuongeza kuwa, hifadhi hii pia ina sifa ya kuwa na aina za wanyama na mimea karibu yote inayopatikana katika nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.

Mintarafu tembo katika hifadhi hii, Lihwa anasema mnyama huyu hupendwa hata na wanyama wengine kutokana na tabia na mwenendo wake awapo hifadhini kwani mara nyingi tembo amekuwa msaada kwa wanyamapori wengine wawapo hifadhini.

“Tembo ni mmoja wa wanyama ambao katika kipindi cha nyuma, wamekuwa wakisakwa na majangili na kuuawa kwa wingi ili kupata meno yake,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, miaka kadhaa iliyopita, wingi wa mnyama huyo ulipungua kwa kiwango kilichotishia ukuaji wake.

Baada ya majangili hao kudhibitiwa na serikali, tembo sasa wanaonekana kuongezeka na hata kufika katika makazi ya watu.

Lihwa anasema shirika hilo linafanya utafiti wa tembo kwa sababu ni mmoja wa wanyama wanaoathiri mfumo mzima wa ukuaji wa viumbe hai.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Ruaha mkoani hapa, kwa sasa hakuna mzoga wa tembo anayekutwa ameuawa kutokana na ujangili.

“Mara ya mwisho kukutana na mzoga wa tembo ilikuwa mwaka 2018 na ilikuwa ni tembo mmoja aliyeuawa na majangili na kesi iko mahakamani,” anasema.

Mbali na mnyama tembo kuupamba Mkoa wa Iringa, mkoa huo pia ni moja ya maeneo ya kiikolojia yenye vivutio vingi vya asili zikiwemo hifadhi za wanyamapori, milima na hata maporomoko mbalimbali ya maji.

Mkoa huo pia una vivutio vya kihistoria na kitamaduni kama vile eneo la malikale la Isimila na makumbusho ya Mkwawa ya Kalenga.

Akizungumza mkoani hapa hivi karibuni na waandishi wa habari za mazingira kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Ofisa wa STE, Lihwa anasema shirika hilo linafanya utafiti wa tembo kwa sababu ni mmoja wa mnyama anayeathiri mfumo mzima wa ukuaji wa viumbe hai.

Waandishi hao wanafuatlia suala la uhifadhi wa mazingira na utalii chini ya mradi wa PROTECT unotekelezwa na Shirika la Misaada la Marekani.

Utafiti wa STE, unafanyika katika Hifadhi ya Wanyamapori Ruaha, mkoani hapa wakishirikiana na jumuiya za uhifadhi wa wanyamapori katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Wanyamapori ya Ruaha (MBOMIPA), lakini pia wakiwa na mradi Kilombero mkoani Morogoro.

Lihwa anasema: “Tembo ni mnyama anayechimba maji katika hifadhi za wanyamapori hususani katika kipindi cha kiangazi; maji hayo yanasaidia hata wanyama wengine wasiokuwa na uwezo wa kupata maji katika kipindi hicho cha kiangazi,” anasema.

Anaongeza: “Katika kipindi cha masika mnyama huyo (tembo) hupanda milimani kwa sababu anaogopa kutitia kwenye maji…”

Lingine linaloshangaza kwa mnyama huyu ni kwamba, tembo amekuwa akisambaza mbegu nyingi kupitia kinyesi chake, lakini pia akiwa na uwezo mkubwa wa kudondosha miti na wanyama wengine wanaokula majani wakifaidi kwa kuwa miti mingine hawawezi kuifikia.

Kwa mara ya mwisho anasema walikutana na mizoga hiyo mwaka 2018, lakini hadi sasa hakuna mzoga mpya wa tembo.“Mizoga mingine midogomidogo ni kama ya swala, lakini hata hivyo, vifo vingi vya wanyama hao ni vile vya asili.

Anasema wamekabiliana na ujangili wa tembo kutokana na msaada mkubwa walioupata kutoka kikosi cha taifa cha kuzuia ujangili.

Kuhusu utalii, Ofisa Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Kanda Nyanda za Juu Kusini, Paul Isazi, anasema wanafanya kazi katika mikoa minane ya Kusini mwa Tanzania ili kuendeleza na kukuza sekta ya utalii nchini hususani Kanda ya Kusini.

Mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini ni Iringa, Morogoro, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Katavi, Rukwa na Njombe.

HUYU ni mama wa mitindo. Ni malkia wa nguvu. Ni ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi