loader
Picha

Huna sababu kutumia neno ‘dabi’

WIKI iliyopita tulianza kuangalia kasumba miongoni mwa jamii kudhani kwamba lugha ya taifa lililowatawala ndiyo bora kuliko lugha yao waliyokuwa wakiitumia kwa karne na karne.

Tukaona jinsi hata baadhi ya Watanzania wanavyosumbuliwa na kasumba hiyo. Tulimaliza makala ile kwa kuangalia namna katika siku za hivi karibuni kulivyozuka maneno yanayotumika katika nyuga mbalimbali yakionekana kuchukua nafasi kubwa ya maneno yaliyokuwa yakitumika kwa miaka mingi na kufikisha ujumbe uliokusudiwa katika nyuga nyingine.

Tuliona matumizi ya neno vuna yanavyotumika mahala ambapo sipo kama vile kurina asali watu kusema kuvuna asali, kuvua samaki wakasema kuvuna samaki pia watu kusema kuvuna maji badala ya kukinga maji.

Makala ikasisitiza kwamba kuvuna kunaanza na kupanda na matokeo ya hatua hiyo kama ilivyo kwa mazao ndipo tunapata neno kuvuna. Leo tunaanza kwa kujiuliza. Je, lugha yetu kimuundo inakubaliana na miundo ya Kiingereza au kila lugha ina miundo yake tofauti na miundo ya lugha nyingine?

Siku hizi pia utasikia neno rasilimali linaongezewa maneno mengine ambayo kwa asili ndiyo yaliyokuwa yakitumika na kukidhi haja ya mawasiliano. Siku hizi utasikia rasilimali watu, rasilimali fedha, rasilimali maji, rasilimali misitu, rasilimali mifugo, rasilimali madini n.k. Je, tukisema nguvukazi/watumishi/wakulima, fedha, maji, misitu, mifugo, madini n.k kuna kitu kitapungua kwa dhati ya neno litakalotumika kwa muktadha mahususi?

Kinachoonekana sasa ni watu wanaamua kutotaka kutumia neno au maneno yaliyokuwa yanatumiwa na wenzao na kuamua kutumia maneno mengine ambayo hayajatumiwa na waliotangulia labda kuwasilisha jambo ambalo wanataka kuliwasilisha wakati huo, ati kuleta upya katika kitu anachokizungumza. Je, kuna upya wowote au upotoshaji na ukiukaji wa kanuni sheria na taratibu za lugha fulani?

Tuangalie neno lingine mlaji, hili nalo ni neno ambalo kwa kweli lina ukakasi mkubwa na uliopitiliza viwango kwani kila kitu siku hizi walaji, walaji hadi sasa utasikia walaji wa viuatilifu! He, inawezekanaje binadamu akawa mlaji wa viuatilifu. Je, binadamu akila viuatilifu atapona kweli? Kwanini neno walaji litumike badala ya maneno yetu ya asili kwa mfano wanunuzi au watumiaji wa viuatilifu?

Kwa nini tuseme walaji pahali ambapo tunaweza kutumia au kuteua msamiati mwingine ambao unakidhi haja ya matumizi kwa dhati yake. Walaji wa umeme, walaji wa maji, walaji wa mbolea, walaji wa mkaa, walaji wa kuni, walaji wa petroli, walaji wa mafuta ya taa, walaji, walaji walaji. Tangu lini tukala visivyolika? Lugha yetu adhimu imekosa msamiati wa kutuwezesha kusema tulichokikusudia bila kuleta ukakasi kwa msikilizaji au msomaji?

Sidhani. Wajumbe walifanya kikao chao kwenye meza ya duara. Hapa pia Kiswahili kinatosha bila kuhitaji maneno kama ‘dabi’ pana ukakasi, utasikia wamekutana kwenye meza ya duara, wakati uhalisia wake ni kwamba watu hawa walikuwa na kikao tu tena cha kuchekesha zaidi ni kwamba hawakuwa kwenye meza ya duara, walikuwa kwenye meza ya pembe nne ukumbini! Kwa nini isingekuwa walifanya kikao?

Je, tukisema hivyo ujumbe tulioukusudia haufiki? Kwa nini tuone alichowaza mzungu ndicho sahihi tena kwa kutumia maneno yaleyale aliyoyatumia wakati kila lugha ina sarufi na muundo wake tofauti na lugha nyingine?

Kwa nini tulazimishe sarufi na miundo ya lugha nyingine itumike kwenye lugha nyingine ilhali kufanya hivyo si sahihi kwani kila lugha ina kanuni, sheria na kaida zake? Wakati mwingine utasikia watu wanasema au kuandika serikali ya leo, unaanza kujiuliza serikali ya leo ndiyo serikali gani? Leo ni nini? Ukifuatilia kwa kina ndipo utagundua kumbe walikusudia serikali iliyopo madarakani.

Sasa kwanini useme serikali ya leo badala ya serikali iliyopo madarakani? Ni serikali ya chama kilichopata ridhaa ya wananchi iongoze kwa kipindi mahususi mpaka hapo uchaguzi utakapofanyika ndipo ama chama kingine kipewe ridhaa au chama hichohicho kiendelee kuongoza serikali.

Katika sekta ya michezo kumekuwa kuna maneno yaliyotumika kwa miongo kadhaa na yakakidhi haja bila kuwa na upungufu wowote.

Kwa kipindi cha meizi kadhaa sasa utasikia waandishi wa habari wakisema dabi ya Kariakoo au dabi ya Dar es Salaam. Kwa mtu aliye mdadisi ataanza kujiuliza dabi ni nini hasa? Ni neno la lugha gani hili? Kwa nini linatumika? Je, linatumika badala ya neno gani? Je, ni neno lisilokuwa na kisawe chochote katika lugha adhimu ya Kiswahili?

Unapoangalia kamusi za Kiingereza za zamani utaona kuwa (derby) yaani dabi ni mashindano ya mbio za farasi walio na umri wa miaka 3 yaliyoasisiwa mwaka 1780 na Mwakilishi wa Malkia katika mji wa Derby.

Ilipofika miaka ya 1840 neno hili liliongezewa maana likamaanisha mashindano katika michezo yoyote iwayo, hasa ya timu ambazo zinapatikana katika eneo moja kijografia.

Siku za hivi karibuni utasikia watangazaji wakisema dabi ya Kariakoo/Dar wakimaanisha pambano la watani wa jadi kati ya Simba na Yanga. Je, kabla ya watangazaji kulipokea neno hili na kuanza kulitumia kwa kasi ya moto wa nyikani, pambano hilo halikuwa na jina mahususi?

Pambano la aina hiyo lina maneno mawili yanayostahili kupewa shikamoo yanayolibainisha pambano la watani wa jadi au timu mbili zinazopatika katika mji mmoja.

Mtanange na kipute ni maneno yaliyotumika kuelezea pambano la watani wa jadi. Mtanange ni mchezo aghalabu wa mpira ambao huhusisha timu zenye upinzani mkali; mchuano mkali.

Kipute ni ushindani mkali baina ya pande mbili kwa ajili ya kitu k.v. pambano kali katika mpira wa miguu. Kumetokea nini hadi tuamue kuyaacha maneno yaliyo ya asili yetu tukayakumbatia yenye asili ya kigeni au ndio mwendelezo wa kujidharau na kujiona hatuna thamani yoyote mbele ya mtawala wetu?

Ninachokiona hapa ni ile hali ya mwanajamii kutaka kuonekana ana maneno mapya ambayo ndiyo yanatumiwa na watangazaji wa nchi zingine hasa zile zilizokuwa watawala wa nchi iliyowatawala.

Ni maoni yangu kuwa wanajamii waache kuyapokea maneno yanayotoka nje bila kuridhika kuwa lugha yao haina kabisa neno lenye maana au linalokaribiana maana na hilo neno lililobebwa juu kwa juu kutoka nje.

Kuyathamini maneno tuliyonayo au msamiati tulionao kwenye jamii ambao kwa muda mrefu umekuwa ukikidhi haja na kufikisha ujumbe tulioukusudia uifikie jamii.

Tunayo maneno mazuri yanayofikisha ujumbe mwafaka kwa wakati mwafaka kama vile sare, suluhu, majalo n.k. Mwandishi wa makala haya ni Mchunguzi Lugha Mkuu wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA).

HUYU ni mama wa mitindo. Ni malkia wa nguvu. Ni ...

foto
Mwandishi: Gertrude Joseph

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi