loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkopo Benki ya Dunia ushindi kwa wanafunzi

HATIMAYE Benki ya Dunia imetoa mkopo wa gharama nafuu wa takribani Sh trilioni 1.135 ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu.

Taarifa iliyotolewa juzi na benki hiyo ilisema mkopo huo wa mabilioni ya shilingi (Dola za Marekani milioni 500), utawezesha mamilioni ya vijana kupata na kuhitimu elimu ya sekondari katika mazingira bora ya kusomea.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilisema uamuzi huo wa Benki ya Dunia wa kuidhinisha kiasi hicho cha mkopo nafuu unapaswa kupongezwa na wote wanaoitakia mema Tanzania.

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Mipango, fedha hizo zitasaidia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia Mradi wa Maboresho ya Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP). Zitatumika pia kuongeza ubora wa elimu kwa kuimarisha elimu ya watoto wa kike na wa kiume kwa sababu watajengewa mazingira mazuri ya miundombinu ya elimu.

Aidha serikali imesema wajibu wa Wizara ya Fedha na Mipango ni kuhakikisha fedha zitakapofika nchini zinatumika vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa kupitia Wizara Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Uamuzi wa benki kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA) unatajwa kuwa ni wa kihistoria ikizingatiwa shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanaharakati nchini na wa kimataifa waliokuwa wakiitaka benki isitoe mkopo kwa Tanzania wakidai kwamba ina sera na sheria ya elimu ya kibaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia iliyotolewa juzi, SEQUIP utaelekezwa moja kwa moja kunufaisha wanafunzi wapatao milioni 6.5 kwa kuimarisha shule zinazoendeshwa na serikali na kutengeneza njia kwa wanafunzi walioacha mfumo rasmi wa shule. Mradi huo hutumia njia ya ulipaji fedha kwa awamu na fedha hutolewa baada ya kuona utekelezaji wa makubaliano ya awali una matokeo mazuri.

Kwetu sisi tunachukulia hatua hiyo ya uidhinishwaji wa fedha hizo ni ushindi kwa wanafunzi wote nchini, kwani sasa watanufaika kwa kuboreshewa mazingira ya elimu.

Tunasema hivyo kutokana na kuamini kuwa kila mtoto anastahili elimu bora na kwa vile mradi huo unatoa kipaumbele kwa vijana wa Tanzania; basi huu ni ushindi mkubwa kwao.

Kutokana na kuidhinishwa kwa fedha hizo, matumaini yetu ni kuwa matatizo yaliyoanza kujitokeza katika sekta ya elimu kama ya uhaba wa madarasa, vifaa vya kufundishia na kujifunzia sasa yatapatiwa majawabu.

Kwetu sisi tunachukulia mkopo huu nafuu uliotolewa na Benki ya Dunia kwa Tanzania kuwa utaleta neema katika sekta ya elimu na ndio maana tunasema hatua hiyo ya kuidhinishwa kwa fedha hizo ambazo awali zilizuiliwa ni ushindi kwa wanafunzi wa Tanzania.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi