loader
Picha

Wabunge waipongeza serikali ya JPM

WABUNGE wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi na mafanikio, yaliyopatikana katika sekta mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitano.

Walitoa pongezi hizo wakati wakichangia mjadala wa mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) alimpongeza Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri, kwa kazi nzuri wanayofanya kuendeleza nchi kwa kipindi cha miaka mitano na maendeleo makubwa yaliyopatikana.

“Miaka mitano tumeona maendeleo makubwa katika kila sekta, miradi mingi imetekelezwa vyema pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” alisema Mbogo.

Alisema vitu na mambo mengi ya thamani, yamefanyika na hayo yametokana na mabadiliko ndani ya chama. Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM) alipongeza serikali kwa juhudi na maendeleo yaliyofanyika nchini, ikiwemo watu wenye ulemavu kuthaminiwa na kushirikishwa katika masuala mbalimbali.

Mollel aliipongeza serikali kwa kumchagua Naibu Waziri, Ikupa Stella Ikupa aliyemuelezea amekuwa akifanya kazi nzuri, kushughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu na kudhihirisha kuwa ulemavu sio kulemaa. Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM) aliishukuru serikali kwa kurudisha heshima ya Mkoa wa Tanga, kwa kulisimamia suala la kilimo cha mkonge.

“Sasa heshima ya Tanga imerudi. Tanga ilikuwa ikitegemea mkonge lakini kilimo hicho kilionekana kufa. Sasa wananchi wa mkoa huo wataanza kuinuka kiuchumi, “ alisema Chatanda.

Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu (CCM) alimshukuru Rais Magufuli kwa kupeleka Tabora maji kutoka Ziwa Victoria. “Igunga tunajengewa chuo cha Veta, umeme bado kata tano tu…tunamshukuru Rais na serikali kwa kutuletea maendeleo makubwa,” alieleza Dk Kafumu.

Naye Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CCM), alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa maendeleo makubwa na kwa kipindi cha miaka minne “bajeti inakuja bila ukakasi.”

Alimpongeza Waziri Mkuu, Majaliwa kwa kuwaongoza mawaziri na kwenda na kasi ya maendeleo makubwa, yaliyopatikana chini ya uongozi thabiti wa Rais Magufuli. Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema) alimpongeza Rais John Magufuli kwa kusema Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utafanyika, licha ya kuwapo kwa virusi vya corona na kwamba utakuwa wa uhuru na hali.

“Napenda kumpongeza Rais na nilimuona akikutana mabalozi wa nchi za nje na aliwaahidi kuwa uchaguzi utakuwa wa uhuru na haki na pia niliona Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi akikutana na mabalozi na kuwahakikishia kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki,” alisema.

Alisema kuwa Watanzania wanahitaji kuchagua viongozi wanaowataka na sio kiongozi kuwachagulia. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) alimpongeza Rais kwa kueleza kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki na kuomba Mungu aondoe ugonjwa wa corona ili uchaguzi ufanyike Oktoba.

Karibu wabunge wengi waliochangia, walipongeza juhudi mbalimbali za serikali, ambazo Waziri Mkuu azieleza pia katika hotuba yake, ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ambayo imefanyika na mingine inayoendelea kufanyika.

WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),akiwemo Wilfred ...

foto
Mwandishi: Angela Semaya, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi