loader
Picha

Mabilioni ya Benki ya Dunia kufanya haya nchini

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (pichani) ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuidhinisha mkopo wa gharama nafuu, uliolenga kutekeleza Mradi wa Maboresho ya Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), huku akitaja manufaa ya fedha hizo kwa sekta ya elimu nchini.

Mkopo ulioidhinishwa na Benki ya dunia ni dola za Marekani milioni 500 sawa na Sh trilioni 1.135. Profesa Ndalichako alisema mradi huo ni muhimu kwa Tanzania, kwa kuwa umelenga kuhakikisha kila mtoto wa Tanzania, anapata elimu ya sekondari.

“Mradi huu ni muhimu sana kwa nchi yetu, hasa ikizingatiwa kuwa serikali chini ya Rais John Magufuli inatekeleza programu ya elimu bila malipo hivyo utahusika kutengeneza miundombinu ya sekondari,” alisema Profesa Ndalichako jana jijini hapa.

Tangu kuanza kutekeleza elimu bila malipo kwa elimu msingi mwaka 2016, wanafunzi walioanza darasa la kwanza kwa sasa wako darasa la tano na wanatarajia kumaliza elimu ya msingi miaka miwili ijayo.

Waziri huyo wa Elimu alisema mkopo huo, utasaidia katika kuimarisha mafunzo ya walimu kazini. “Kupitia fedha hizo, tunahakikisha walimu wetu wana ujuzi na stadi zinazoendana na wakati wa sasa ili waweze kufundisha zaidi,” alisema na kuongeza pia fedha hizo zitasaidia kuimarisha na utoaji wa elimu kwa njia ya dijitali.

“Lakini pia tunafahamu hii ni dunia ya teknolojia, shule zetu bado ziko nyuma katika suala zima la teknolojia, kwa hiyo katika mradi huu tunataka kuanzisha mafunzo ya dijitali kwa wanafunzi wetu wa sekondari na walimu,” alisema.

Alisema kupitia fedha hizo, serikali imejipanga kumuondolea vikwazo mtoto wa kike, ambavyo vinachangia kutomaliza shule. “Lakini kubwa zaidi na la kipekee mtoto wa kike, tunataka kuhakikisha kwamba mtoto wa kike tunamuondolea vikwazo ambavyo vinasababisha asiweze kumaliza shule kwa sababu mbalimbali.

“Tutaviondoka kwa kuhakikisha tunatengeneza mazingira rafiki na salama shuleni kwa mtoto wa kike, hivyo kupitia mradi huu tunakwenda kuimarisha utoaji wa ushauri nasaha ili wanafunzi ambao wana changamoto aidha za kifamilia au zinazotokana na kijamii au zinazotokana na mazingira ya shule aweze kusaidiwa,” alibainisha.

“Kwa hiyo tunataka kutengeneza mazingira ambayo mwanafunzi wa kike akiwa na changamoto yoyote, awe na mahali pa kusemea ili serikali iweze kuchukua hatua,” alieleza Profesa Ndalichako.

Alisema kupitia mradi huo, pia serikali itaondoa changamoto kwa mwanafunzi wa kike ya kutembea umbali mrefu wa kwenda na kurudi shule, hivyo kuwa katika hatari ya kuingia kwenye vishawishi. Alisema kupitia mradi huo, serikali itajenga shule za bweni kwa ajili ya watoto wa kike ili kuwaondolea changamoto ya kutembea umbari mrefu wa kwenda na kurudi shule.

Katika kupunguza msongamano wa wanafunzi shuleni na ongezeko la wanafunzi wanaotokana na kuanza kutolewa bila malipo, serikali inatarajia kujenga shule ya sekondari katika kila halmashauri.

“Pia mradi utapunguza msongamano katika shule na ongezeko la wanafunzi, hivyo kupita mradi huu tunakwenda kujenga shule sekondari katika kila halmashauri ili kuhakikisha kuwa shule zinakuwa karibu na wanafunzi.

“Kupitia mkopo huu, watoto wakike na wakiume watanufaika na shule zitakazojengwa, mafunzo ya kidigitali walimu wao watapata mafunzo,” alisema.

Aliongeza, “Nawashukuru tena Benki ya Dunia kwa kuidhinisha mkopo huu kwani ni muhimu na unakwenda kuwanufanisha watoto wa Tanzania zaidi ya milioni sita.”

Kupitia programu hiyo, serikali imejipanga kujenga shule 1,000 mpya za sekondari, ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi lililotokana na kuanza kutolewa kwa elimu bila malipo.

MTANDAO wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) umesema wasichana 40 ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi