loader
Picha

AfDB yaipaTanzania mabilioni kukabili nzige

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeidhinisha msaada wa dharura wa Dola za Marekani milioni 1.5 (zaidi ya Sh bilioni 3.45), kukabili Nzige wa Jangwani katika nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, ikiwemo Tanzania.

Pamoja na kwamba Tanzania haijavamiwa na nzige hao, AfDB imeitaja kuwa miongoni mwa nchi iliyo katika tishio la kuvamiwa kutokana na dalili za kuwepo kwa makundi mapya ya nzige hao wiki chache zijazo.

Msaada huo uliidhinishwa juzi Jumatano na Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo kwa nchi tisa za Muungano wa Maendeleo Afrika Mashariki na Nchi za Pembe ya Afrika (IGAD) ikiwa ni hatua za kukabiliana na Nzige wa Jangwani na tishio la uvamizi wa nzige hao hatari kwa usalama wa chakula na makazi.

Taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Nje wa AfDB, Makao Makuu jijini Abidjan nchini Ivory Coast, ilieleza kuwa msaada huo utaratibiwa na IGAD, iliyopewa dhamana kuratibu rasilimali za nchi hizo kwa niaba ya Umoja wa Afrika (AU).

IGAD inashirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) la Umoja wa Mataifa (UN), linaloongoza uratibu wa msaada wa washirika wa maendeleo, kudhibiti uvamizi wa nzige, kulinda makazi na kusaidia urejeshwaji wa hali nzuri ya maisha kwa kaya zilizoathirika katika Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika. FAO itafanya kazi kama wakala wa utekelezaji wa msaada huo.

“Fedha hizo zitatumika kudhibiti kuenea kwa uvamizi wa nzige kwa sasa, kuzuia kundi lijalo la nzige na kufanya tathmini ya athari na ufuatiliaji ili kuongeza utayari na ufahamu. Sehemu ya fedha pia itatumika katika gharama za kiutawala,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Nchi tisa zilizonufaika kwa msaada huo ni Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na Tanzania. Kenya, Ethiopia na Somalia zimetajwa kuathirika zaidi kwa nzige, ambao wanatarajia kuunda kundi jipya wiki chache zijazo.

Uvamizi huo unahatarisha maisha ya watu, usalama wa chakula na uzalishaji wa kilimo. Taarifa hiyo ilieleza kuwa hali ya nchi za Ethiopia na Somalia, imekuwa mbaya kwa miaka 25 huku Kenya imeathirika kwa tatizo hilo kwa miaka 70.

Aidha, imefafanua kuwa Ethiopia nzige wameharibu zaidi ya hekta 30,000 za mazao ikiwamo kahawa na chai yanayochangia asilimia 30 ya mauzo ya nje ya taifa.

Licha ya hatua za serikali kuingilia kati, nzige wameripotiwa katika sehemu kubwa za nchi hiyo. Nchini Djibouti, zaidi ya asilimia 80 ya mashamba ya mifugo 1,700 yaliyopo katika kanda 23, yameathirika kwa uharibifu wa nzige hao wa jangwani.

Kwa mujibu wa taarifa ya FAO, pamoja na serikali kuchukua hatua kuwakabili nzige hao nchini Kenya, maeneo 18 kati ya 47 nchini humo, yameathirika na zaidi ya hekta 70,000 za mazao mbalimbali zimeharibiwa.

Mazao hayo ni mahindi, maharage na malisho ya mifugo. Kundi la Nzige wa Jangwani lilielezwa pia kutishia kuvamia nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zikiwamo Uganda, Tanzania, Sudan Kusini, Sudan na Eritrea.

WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),akiwemo Wilfred ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi