loader
Picha

Mkoa wa Singida katika vita dhidi ya COVID-19

UGONJWA unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) umetangazwa kama janga la kimataifa ukisababisha maelfu ya vifo katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Tofauti na maradhi mengi yaliyowahi kutokea, maradhi haya yanaathiri watu wa kada zote wakiwamo hata viongozi wakuu wa nchi na taasisi mbalimbali wakiwamo wananchi wa kawaida, wanadiplomasia, wafanyabiashara, viongozi wa dini na hata wakuu wa usalama na huku baadhi ya mataifa yaliyoendelea kama Italia na Marekani yakizidi kumwaga machozi kwa kiasi kikubwa.

Hata kwa Tanzania, walioathirika na kuthibitishwa kupata virusi hivyo hadi wakati ninaandika makala haya walikuwa 13. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa corona ni wa kizonotiki kwa maana ya kwamba, virusi hivyo vinaambukizwa kati ya wanyama na binadamu.

Uchunguzi wa kina uligundua kuwa kuna aina kadhaa za virusi vya corona vinavyozunguka kwa wanyama, lakini havijaambukiza kwa binadamu. WHO linaainisha dalili kuu za maambukizi za ugonjwa huu kuwa ni pamoja na kupata matatizo ya kupumua, homa, kikohozi.

Katika hali kali zaidi, maambukizi yanaweza kusababisha nimonia, kuishiwa pumzi, matatizo ya figo na hata kifo. Wazee na watu wenye matatizo ya kiafya kama vile ugonjwa wa pumu, kisukari wanakuwa kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha wanapokumbwa na corona.

Kwa mujibu wa WHO, hadi sasa chanjo ya kutibu virusi hivi haijathibitika. Ugonjwa huu unaenea kupitia matone madogomadogo ya mate, chafya, kukohoa, kupumua (mdomo) au kamasi (pua), kugusa-kiti, nguo, vyombo, kitanda au meza yenye maambukizi.

WHO linasisitiza kuwa namna ya kujikinga na corona ni kwa kunawa mikono kwa sabuni kila wakati, kutoshikana mikono, kukaa umbali kwa takribani mita 2 baina ya mtu na mtu, kufunika mdomo kwa tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya, na kuepuka kugusana na mtu mwenye dalili ya ugonjwa huu. Hadi ninaandika makala haya mwishoni mwa juma, hakuna mtu aliyekufa kwa ugonjwa huu nchini.

Kuhusu mgonjwa wa kwanza kuthibitika nchini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema: “Mgonjwa huyu baada ya kuwasili na kupimwa na wataalamu wetu, hakuonesha dalili zozote, lakini baada ya kufika hotelini anasema alianza kujisikia vibaya na akaamua kujitenga kabla ya kwenda hospitalini.” “Baada ya vipimo kuchukuliwa kupelekwa Dar es Salaam, ilithibitika kuwa ana maambukizi ya corona.”

Kimsingi, juhudi za Tanzania kukabili ugonjwa huu zinazoongozwa na Rais John Magufuli zilianza kwa Rais kufuta mbio za mwenge zilizotakiwa kuanza hivi karibuni akifuatiwa na kisha, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akatangaza kufunga taasisi zote za elimu nchini (shule, vyuo na vyuo vikuu) kwa siku 30 tangu Machi 17, 2020 serikali ikipiga marufuku mikusanyiko yoyote isiyo ya lazima ikiwamo michezo yote inayokusanya makundi ya watu.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dk Tigest Katsela Mengestu, anaipongeza Tanzania kwa hatua inazochukua kukabili ugonjwa huo. Mkoa wa Singida nao unaendelea kuwa salama na kuunga mkono jitihada za serikali kudhibiti kuingia na kusambaa kwa ugonjwa huo nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi anasema tayari mkoa huo umewakutanisha wadau mbalimbali wa afya, wakiwemo viongozi wa dini, wataalamu wa afya, wafanyabiashara na vyombo vya habari, ili kuweka mikakati kabambe ya pamoja kukabili COVID-19.

Anasema katika kikao hicho maalumu cha kupambana na corona, wadau wamehimizwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, ili kukabiliana na janga hilo kwa kuzingatia kuwa Mkoa wa Singida ni kitovu cha nchi kwani barabara zote kuu zinazounganisha Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika kupita hapo, hivyo kuwa na mwingiliano mkubwa wa wasafiri.

“Jambo la msingi kwa sasa katika mkoa wetu wa Singida ni kuwawezesha wananchi wetu kuuelewa vizuri ugonjwa huu ili wajikinge kirahisi kabisa, na hiyo ndiyo silaha yetu kubwa ya kwanza huku tukimtanguliza Mungu,” anasema Dk Nchimbi.

Anaitaja baadhi ya mikakati itakayotumika kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwamo ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovic anasema, kila halmashauri ndani ya Mkoa wa Singida imetenga chumba maalumu kwa watu watakaohisiwa kuwa na ugonjwa huo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na kisha, kufuata taratibu za kitaifa kwa ajili ya kuchukua sampuli na kupeleka kwenye maabara ya kitaifa kwa uchunguzi zaidi kadiri ya miongozo na taratibu zilizowekwa na Serikali.

Anasema Kituo cha Afya Sepuka kimetengwa kama Kituo Maalumu cha Mkoa wa Singida kwa ajili ya wagonjwa wa corona. “Huwezi kujua mgonjwa anaweza kutokea katika eneo gani la mkoa wetu ndiyo maana tumejiandaa kwa kila kituo,” anafafanua Dk Ludovick.

Dk Nchimbi anafafanua akisema tayari mkoa wake kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, umeshatoa mafunzo maalumu ya siku tatu kwa wataalamu ambao wameshakwenda kuwafundisha kwa ngazi za chini ili kukabiliana na ugonjwa huo kila eneo.

Kutolewa kwa mafunzo hayo kunawafanya wataalamu kuimarika na kujiamini wanapopata mgonjwa wa corona badala ya kutaharuki. Nchimbi anawataka wazazi kuhakikisha watoto na wanafunzi wote mkoani kwake wanaacha kuzurula katika kipindi hiki ambapo shule zimefungwa kutokana na ugongwa huu na badala yake, wakae nyumbani na kujisomea.

Anasema: “Adhabu kali zitatolewa kwa wazazi na walezi watakaobainika kuwaacha watoto wakizagaa mitaani bila sababu za msingi.”

Anasisitiza kwamba, ameshatoa maelekezo kwa kila kaya, taasisi, sehemu za biashara na vituo vyote vya mabasi kuwa na miundombinu ya kunawia mikono na vitakasa mikono (sanitaisers) kwa sababu njia kuu ya kupata virusi hivi ni kupitia mikono. Anatoa mwito kwa watengenezaji wa vitakasa mikono mkoani Singida kutengeneza kwa wingi katika kipindi hiki na kuendelea kuviuza kwa bei ileile.

Anasema mkoani Singida, atakayebainika kupandisha bei ya vifaa kinga vyovyote atachukuliwa hatua kali za kisheria. Dk Nchimbi anaelekeza kuwa, inapotokea mtu kuhisiwa kuwa na ugonjwa huo, wanajamii wachukue tahadhari ya kumchagua mwanakaya kumhudumia mgonjwa, badala ya wanafamilia wote kumhudumia kwa mazoea itakayopunguza msongamano hospitali na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Anawataka wananchi wa Singida kuachana na tabia, mila na desturi zitakazochangia kuenea kwa ugonjwa. Tabia hizo ni pamoja na kunywa pombe za kienyeji katika makundi ya pamoja huku wakizungusha chombo kimoja cha pombe hiyo na badala yake, waachane na ulevi.

Anaagiza wamiliki na wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni mkoani Singida kuchukua taarifa sahihi za wageni wanaoingia na kutoka katika sehemu zao na kujua hali zao zikoje ili pindi wanapobaini mgeni ana dalili za ugonjwa huo, watoe taarifa haraka.

“Mkoa wa Singida ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu na kwa sasa ndiyo tunaanza msimu wa kuuza vitunguu na tunapata wageni wengi wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya Tanzania... kila mkazi wa mkoa wangu awe mlinzi wa mwenzake ili tudhibiti kabisa uingiaji na usambaaji wa ugonjwa huu katika mkoa wetu,” anasisitiza Nchimbi.

Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi anawataka wananchi kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya kujikinga na corona ili kuzuia kuporomoka kwa uchumi wa nchi. Anasema ugonjwa wa corona umeleta umejeruhi uchumi wa dunia ambapo masoko makubwa ya mitaji katika miji ya London Uingereza na New York, Marekani yameyumba jambo litakalowafanya wawekezaji wengi kuogopa kuwekeza katika sehemu mbalimbali duniani.

Profesa Ngowi anasema nchi zinazotegemea utalii kama Tanzania zipo hatarini kuathirika zaidi kwa kuwa watalii wanashindwa kufika katika kipindi hiki kwa hofu ya kuambukizwa ugonjwa huu.

“Kwa kufanya hivyo, shughuli zote za kwenye mnyororo wa utaliii kama usafirishaji, kilimo, hoteli na watoaji huduma za kuwasaidia watalii wataathirika sambamba na wategemezi wao,” anasema Ngowi.

Profesa Ngowi anawataka wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuepusha mfumuko wa bei na kushuka kwa ukuaji wa uchumi. Anasema: “Kwa mwaka huu ukuaji wa uchumi kwa nchi yetu ulikadiriwa kukua kwa asilimia takribani 8 ambapo kwa sasa kama ugonjwa wa corona utaingia ukuaji huo unaweza usifanikiwe.”

Mwandishi ni Ofisa Habari wa Mkoa wa Singida.

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: John Mapepele

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi