loader
Picha

Hatari ya vipodozi vyenye viambata sumu

NCHINI Tanzania wanawake wengi wamepata madhara kiafya baada ya kutumia vipodozi vyenye viambata sumu.

Baadhi yao wamejikuta wakilazimika kutumia gharama kubwa kujitibu baada ya kupata madhara yatokanayo na vipodozi hivyo.

Kwa baadhi ya watumiaji wa vipodozi hivyo, huhitaji vipimo vya maabara kufahamu jinsi vilivyowaathiri, kwani wanatambulika hata kwa kuwaangalia.

Wengi waliopata madhara ya kiafya kutokana na vipodozi vyenye viambata sumu (mkorogo), wamekuwa na mvuto wanaokusudia kwa muda mfupi Lakini madhara yanayojitokeza baadaye ni makubwa, ikiwemo kupoteza maisha au kutumia fedha nyingi kujitibu.

Kwa kutambua madhara hayo ya vipodozi, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo limepewa jukumu la kusimamia vipodozi hivyo kupitia Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019, limekuja na mkakati mpya wa kuelimisha wananchi aina ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania.

Mkakati pia utaambatana na uendeshaji wakwenye soko kwa lengo la kuviondoa sambamba na kutoa elimu kwa umma na kusajili vipodozi. Kabla ya TBS kukabidhiwa jukumu hilo mwaka jana, usimamizi wa vipodozi ulikuwa ukifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Ili kuhakikisha vipodozi vyenye viambato sumu haviendelei kutumiwa na Watanzania, TBS inawataka wananchi na watumiaji wa vipodozi vilivyopigwa marufuku kuepuka matumizi ya vipodozi hivyo, kwani vina madhara ya afya kwa watumiaji.

Lakini, pia shirika hilo linawataka wafanyabiashara wa vipodozi, kupeleka taarifa za vipodozi wanavyouza na kuvisajili kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wake. Hatua hiyo itawasaidia kujua ni vipodozi vipi, vimepigwa marufuku na vile vinavyoruhusiwa kwenye soko la Tanzania.

Mratibu wa Usajili wa Majengo na Bidhaa za Chakula na Vipodozi wa TBS, Moses Mbambe anataja miongoni mwa vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini kuwa ni krimu na losheni zenye kiambata cha Hydroquinone na sabuni zenye kiambata cha Hydroquinone.

Vingine ni sabuni zenye kiambata cha zebaki (Mercury), krimu zenye kiambata cha zebaki na michanganyiko yake na kipodozi cha kupunguza unene chenye kiambata cha mmea uitwao phytolacea Spp.

Mtaalamu huyo anasema vipodozi hivyo, vinatokana na mmea ‘Arctostaphylos Uva URSI (bearberry extract) wenye viambato vya Hydroquinone na Abutin, ambavyo ni sampuli zipatazo tano na vipodozi vyenye kiambata cha Tin Oxide, kinachosababisha muwasho kikitumiwa karibu na eneo la macho, ambavyo jumla ni sampuli sita.

Vipodozi vingine ni vile vyenye kiambata cha Malic acid, ambacho kinababua seli za ngozi na kusababisha weupe, mfano Aha Whitening Cream.

Mbambe anataja vingine kuwa ni vipodozi vya nywele vyenye kiambato cha Apocynum Cannbium Root Extract, mfano African Gold Glo na vipodozi vinavyotokana na Tussilago Farfara, mfano Soft and Free Hair Food.

“Vingine ni vipodozi vya kuzuia harufu (antiperspirant) vilivyo na Aluminum Zirconium Compound, mfano wa hivyo ni Triplc Dry Antiperspirant,” anasema Mbambe.

Anaongeza kuwa “Vingine ni krimu zenye misuguano (Homones in Steroids), jeli zenye Steroids na vipodozi vingine vyenye kiambato sumu cha Hydroquinone & steroid na vingine.”

Mbambe anasema mtu yeyote anayetaka kujua vipodozi ambavyo havitakiwi kwenye soko la Tanzania afike kwenye ofisi za TBS makao makuu na ofisi za kanda. Anasema muda si mrefu orodha hiyo itawekwa kwenye tovitu ya shirika.

Akizungumzia madhara ya vipodozi hivyo, Mbambe anasema vipodozi vyenye Hexachloraphene, mtumiaji akijipaka hupenya kwenye ngozi na kuingia kwenye mishipa ya fahamu hasa kichwani.

Pia, anasema husababisha ugonjwa wa ngozi na kuathiri ngozi, pindi mtumiaji anapokuwa kwenye mwanga. Vile vile anasema ngozi huwa laini na kusababisha mtu kupata ugonjwa kama fangasi au maambukizi ya vimelea vya maradhi. Kwa vipodozi vyenye zebaki, Mbambe anasema husababisha madhara ya ngozi, ubongo, figo na kwenye viungo mbalimbali vya mwili.

“Zebaki inapopakwa kwenye ngozi hupenya taratibu ndani ya mwili na kusababisha sumu yake kuingia kwenye damu, hivyo kuleta madhara mengi mwilini,” anasema Mbambe. Aliongeza kuwa “Mjamzito akitumia vipodozi vyenye zebaki mtoto huathirika akiwa bado tumboni na huweza kuzaliwa akiwa na mtindio wa ubongo.” Lakini, pia anasema vipodozi hivyo, husababisha ngozi kuwa laini na yenye mabaka meusi na meupe na husababisha mzio wa ngozi na muwasho. Kuhusu kiambata chenye Steroids, Mbambe anasema hilo ni kundi la homoni. “Homoni hizi hutengenezwa kwenye miili ya binadamu na wanyama, pia zinaweza kutengenezwa nje ya mwili wa binadamu (artificial hormones) katika kundi hili. Corticosteroids ndizo hutumika sana kama viambata kwenye vipodozi,” anasema Mbambe. Anafafanua kwamba Steroids zikitumika kwa muda mrefu, husababisha madhara mbalimbali, kama ugonjwa wa ngozi na kutokwa na chunusi kubwa.

“Pia ngozi huwa nyembamba sana na laini na endapo itapata jeraha au kufanyiwa upasuaji, kidonda hakitapona na pia husababisha magonjwa ya moyo,”anasema Mbambe.

Kwa upande wa vipodozi vyenye Chroloform, mtaalamu huyo anasema husababisha kansa ya utumbo mpana na kibofu cha mkojo, na pia husababisha ugonjwa wa akili na ule wa mishipa ya fahamu.

Kwa mujibu wa Mbambe, Chroloform husababisha ngozi kuungua, maumivu makali, ngozi kuwa nyekundu na kutokwa na vipele.

Akizungumzia vipodozi vyenye viambata vya Chlorofluorocarbon, anasema hivyo husababisha madhara kwenye mishipa ya katikati ya fahamu na hivyo kusababisha mtu kutopumua vizuri.

“Lakini pia husababisha kichefuchefu, kutapika, kuumwa kichwa, kusikia usingizi na kusikia kuzunguzungu,” anasema Mbambe.

Kuhusu Methylene Chloride, anasema husababisha saratani na madhara kwenye mishipa ya kati ya fahamu, kwenye maini na kwenye mishipa ya moyo.

Kwa upande wa matumizi ya vipodozi vyenye kiambato cha Bithionol, Mbambe anafafanua kuwa athari zake ni kupata mzio wa ngozi na athari kwenye ngozi ikiwa itapata mwanga kwenye jua.

“Iwapo sumu itaingia kwenye mishipa ya fahamu husababisha ugonjwa wa mishipa ya fahamu na kwamba sumu ya zebaki ikiingia mwilini kwa kiwango kikubwa husababisha madhara kama upofu, uziwi na upotevu wa fahamu mara kwa mara,” anasema Mbambe.

Kwa upande wa kiambata chenye Vinyl Chloride, anataja madhara yake kuwa ni kusababisha kansa ya maini, ubongo, mapafu na mfumo wa damu. “Sumu hii pia husababisha kuumwa kichwa, kusikia kizunguzungu na kupoteza fahamu,”anasema Mbambe.

Kuhusu Zirconium, anasema husababisha kansa ya ngozi, huku vipodozi vyenye Halogenated Salicylanilide, madhara yake yakiwa ni kusababisha mzio wa ngozi mara inapopata mwanga wa jua na ugonjwa wa ngozi.

Kwa upande madhara yanayosababishwa na kiambata sumu cha Chloroquinone, Mbambe anasema; “Katika kundi zima la viambata, Chloroquinone hutumika zaidi kutengeneza vipodozi. Hydroquinone husababisha madhara ya muwasho wa ngozi, mzio wa ngozi, saratani, kuchubuka kwa ngozi na kusababisha mabaka meupe na meusi.”

Pamoja na madhara hayo ya kiafya, Mbambe anasema kuna madhara kadhaa ya kiuchumi yanayosababishwa na matumizi ya vipodozi visivyo na ubora na usalama kwa watumiaji.

Madhara hayo ni Wizara ya Afya hulazimika kutenga fedha nyingi, kwa ajili ya ununuzi wa dawa na kuwahudumia watu waliopata madhara ya vipodozi. Fedha hizo zingeweza kwenda kugharimia shughuli zingine za maendeleo ya nchi.

Madhara mengine ni fedha nyingi zinapotumika kununua vipodozi na mikorogo, hupunguza kipato cha familia kwa sababu zingetumika kwa ajili ya ustawi wa familia.

Kwa msingi huo, Mbambe anataka watumiaji wa vipodozi na wananchi, kujiepusha na matumizi ya vipodozi vilivyopigwa marufuku, kwani huleta madhara mengi kwa afya ya watumiaji na taifa kwa ujumla.

“Ni muhimu kwa wafanyabiashara wa vipodozi kuleta taarifa za vipodozi wanavyouza TBS kwa njia ya mtandao ili kuwasaidia kujua ni aina zipi za vipodozi vimepigwa marufuku nchini na vilivyoruhusiwa,” anasema

HUYU ni mama wa mitindo. Ni malkia wa nguvu. Ni ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi