loader
Picha

Mataifa yaeleza namna kupunguza vifo vya corona

BAADHI ya mataifa yenye wagonjwa wengi na vifo vichache yameeleza hatua zilizochukuliwa na nchi hizo katika kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa wa corona.

Mataifa hayo ni pamoja na Ujerumani, Singapore, Isarel na Japan. Katika kupambana na vifo vya maambukizi ya virusi vya corona mataifa hayo yameelezea njia walizotumia ikilinganishwa na nchi nyingi za Ulaya, Marekani na Asia ambazo idadi ya vifo iko juu.

Kwa mujibu wa tovuti ya worldometers, mpaka jana, Ujerumani ilikuwa na jumla ya wagonjwa 84,794 na vifo 1,107, Israel wagonjwa 6,857 na vifo 36, Japan wagonjwa 2,617 na vifo 63, Singapore wagonjwa 1,049 na vifo vitano.

Miongoni mwa hatua ambazo nchi hizo zimechukua katika kudhibiti idadi kubwa ya vifo ni pamoja na kufanya upimaji wa mapema na endelevu kwa wananchi wao. Kwa mujibu wa mtaalamu wa virusi na tabia zake katika Hospitali ya Charite mjini Berlin, Chiristian Drosten, idadi kubwa ya vipimo vilivyofanyika nchini humo vililenga kuwatambua mapema watu walioambukizwa, hivyo kusaidia kupunguza idadi ya vifo.

“Tuna vifo vichache kwa sababu tunafanya vipimo vingi vya kimaabara,” anasema Drosten ambaye pia ni Mshauri wa Serikai na Mkurugenzi wa Taasisi inayohusika na masuala ya virusi na tabia zake katika Hospitali ya Charite mjini Berlin.

Mtaalamu huyo wa virusi anasema sababu zingine zilizoisaidia Ujerumani kudhibiti idadi ya vifo ni mwitikio wa mapema katika kuufuatilia ugonjwa huo, kuwepo kwa mtandao wa maabara huru ambazo zilianza kuwapima watu tangu mwezi Januari wakati maambukizi yalikuwa bado yako chini.

Kutokana na mtandao huo wa kimaabara, Ujerumani iliweza kufanya vipimo zaidi ya nusu milioni kila wiki hali inayoelezwa kusaidia kupunguza idadi ya vifo kwa kuwa watu wote walioonesha dalili za kawaida au hawakuwa na dalili yoyote walipimwa.

Mbali na sababu hizo mbili, sababu nyingine iliyoisaidia Ujerumani ni kuwekeza katika sekta ya afya kwa muda mrefu ikiwemo kuwa na vyumba vya kutosha vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu pamoja na mashine za kupumulia.

Kutokea kwa mlipuko wa virusi hivyo, kumezifanya hospitali nchini humo kupata muda wa kutosha kuongeza uwezo wao. Imeelezwa kuwa mipango inaendelea nchini humo ya kuongeza mara mbili vitanda katika vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu ambavyo kwa sasa viko 28,000.

Sambamba na hilo, Serikali nchini humo imepanga kuongeza idadi ya mashine za kupumulia hadi kufikia 35,000, wakati Ufaransa na Italia zina wastani wa mashine 7,000 na 5,000 kila moja za kupumulia. Nchini Singapore nako licha ya kuwa na wagonjwa 1,049, lakini wamefanikiwa kupunguza idadi ya vifo ambako mpaka jana walikuwa na vifo vitano.

Baada ya kukumbwa na mlipuko wa homa kali ya mfumo wa upumuaji (SARS) mwaka 2002 na 2003 uliosababisha watu 8,098 kuambukizwa duniani kote na vifo 774, Singapore iliamua kuimarisha miundombinu yake ya afya katika kupambana na magonjwa ya mlipuko baada ya wananchi wake 238 kuambukizwa na wengine 33 kufa kwa SARS.

Miongoni mwa mipango waliyoitekeleza ya muda mrefu ambayo imewasaidia kupambana na virusi vya corona ni pamoja na ujenzi wa hospitali maalumu za kuwatenga watu walioambukizwa, vyumba visivyo na magandamizo wa hewa ili kuzuia hewa kutoka chumba kimoja isisambae kwenda chumba kingine pamoja na sheria kusimamiwa ipasavyo.

Sambamba na hilo, Singapore ilizindua programu maalumu ya simu inayoitwa ‘TraceTogether’ inayosaidia kuwafuatilia na kuwatambua washukiwa wa maambukizi ya corona.

Programu hiyo ilitengenezwa na Taasisi ya Teknolojia ya Serikali (GovTech) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya nchini humo. Programu hiyo ilizinduliwa Machi 20 mwaka huu na wananchi wanatakiwa kuipakua katika simu zao.

Kupitia programu hiyo, wananchi wa Singapore wanaweza kuombwa na Wizara ya Afya kutoa taarifa zao kama sehemu ya uchunguzi na mtu akikataa kutoa ushirikiano anaweza kushitakiwa chini ya Sheria ya Magonjwa ya Kuambukiza. Kwa upande wa Israel licha ya kuwa na wagonjwa 6,857, lakini imefanikiwa kupunguza idadi ya vifo ambapo mpaka jana ilikuwa na vifo 36.

Miongoni mwa hatua ambazo taifa hilo imezichukua katika kukabiliana na maambukizi hayo na kufanikiwa kupunguza idadi ya vifo ni pamoja na serikali kuamua kuwafuatilia wagonjwa na washukiwa wa maambukizi hayo kupitia simu zao za mkononi.

Hatua zingine ambazo Israel imezichukua ni kupunguza usafiri wa umma kwa asilimia 75, na kuziruhusu teksi kuendelea kutoa huduma lakini kwa masharti ya kubeba abiria mmoja tu anayetakiwa kukaa siti ya nyuma huku madirisha ya gari yakiwa wazi.

Nchini Japan, licha ya kuwa na wagonjwa 2,617, lakini idadi ya vifo ni ndogo. Idadi ndogo ya vifo nchini humo inatokana na mtindo wa maisha walionao hata kabla ya maambukizi ya virusi vya corona kutokea.

Miongoni mwa mitindo hiyo ya maisha ni namna yao ya kusalimiana kwa kuinama tu bila kushikana mikono au kubusiana ambapo hufundishwa salamu hiyo tangu wakiwa watoto.

Mtindo mwingine wa maisha uliowasaidia kuwa na vifo vichache vya corona ni tabia yao ya kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono pamoja na kuvaa barokoa katika maisha yao ya kila siku hata kabla ya kutokea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Aina hii ya maisha imeelezwa kuwasaidia Wajapan katika kupambana na maambukizi ya virusi vya corona na kupunguza idadi ya vifo. (Imeandikwa na Matern Kayera kwa msaada wa mtandao)

HUYU ni mama wa mitindo. Ni malkia wa nguvu. Ni ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi