loader
Picha

Mikoa 12 yaagizwa kuandaa miongozo uwekezaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka mikoa 12 ifi kapo Septemba mwaka huu, iwe imeandaa na kuzindua miongozo ya fursa za uwekezaji kama mikoa 14 mingine ilivyofanya.

Mikoa ambayo imezindua miongozo ya fursa za uwekezaji ni Ruvuma, Songwe, Pwani, Lindi, Kagera, Mtwara, Geita, Kilimanjaro, Simiyu, Manyara, Dodoma, Mwanza, Kigoma na Morogoro.

Majaliwa aliitaka mikoa hiyo 12, kutenga maeneo ya uwekezaji ili kuhamasisha na kuvutia uwekezaji. Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo wakati akiwasilisha bungeni jijini hapa hotuba ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.

“Tunapokuwa na miongozo wa uwekezaji katika mikoa yetu inarahisisha uhamasishaji na kumvutia mwekezaji kuja nchini na kufanya uwekezaji ambao utakuwa na tija kwa taifa,” alieleza Waziri Mkuu.

Aliliambia Bunge kwamba Tanzania kijiografia na kibiashara, iko sehemu nzuri na kuna kila sababu ya kuandaa miongozo yenye kuainisha fursa za uwekezaji zilizopo katika mikoa na kutenga maeneo ya uwekezaji. Alieleza kuwa miongozo hiyo itachochea uwekezaji nchini.

“Kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara jumla ya mikoa 14 ndiyo iliyokwishazindua miongozo ya fursa za uwekezaji. Hivyo ni lazima mikoa iliyobaki iandae miongozo hii ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kujitangaza kimataifa kupitia fursa zilizopo nchini,” alieleza.

Aliongeza, “Miongozo ya fursa za uwekezaji za kila mkoa itawekwa katika tovuti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuzitangaza ndani na nje ya nchi.”

Alisema TIC ina jukumu la kuhamasisha na kutangaza vivutio vya uwekezaji.

Alifafanua kwamba miongozo hiyo, itaongeza kasi ya wawekezaji kuja Tanzania na kuwekeza katika meneo ya vipaumbele vyao.

“Kupitia TIC tumeandaa Kitengo ya Huduma Mahali Pamoja ‘One Stop Centre’ chenye watendaji kutoka taasisi kumi ambao wameendelea kutoa huduma za muda mfupi kwa wawekezaji wetu kupitia kituo hicho,” alisema.

Aliliambia Bunge kuwa hadi kufikia Februari 2020, jumla ya miradi 146 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1,514.57 imesajiliwa na inategemewa kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 26,384.

“Endapo tutafanikiwa kuandaa miongozo ya fursa za uwekezaji nchini na kuweka katika tovuti ya TIC idadi ya miradi ya uwekezaji itaongezeka zaidi hii ikiwa ni pamoja na maboresho ya mazingira ya biashara yanayoendelea kufanywa na serikali,” alisema Waziri Mkuu.

SHIRIKA la Taifa la Biashara (ZSTC) limesema ni makosa kwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi