loader
Picha

Makundi haya yasaidiwe kukabili corona

UGONJWA wa Covid 19 unaosababishwa na virusi aina ya corona, unazidi kuua mamia ya watu hasa nchi za Ulaya. Kwa hapa nchini umeshaua mtu mmoja na wengine kadhaa wamelazwa.

Baadhi ya nchi zimezuia raia wake kutoka nje ya makazi yao. Kwa hapa nchini serikali imeweka msisitizo kwa wananchi kuzingatia masharti yatakayowawezesha kukabiliana na maambukizi yake.

Masharti hayo ni kama vile kunawa mikono kwa kutumia maji yanayotiririka au kutumia vitakasa mikono, kukaa umbali wa mita moja na kujikinga wakati wa kupiga chafya au kukohoa.

Hakika serikali na wadau wengine wa afya, wanajitahidi kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kuikabili corona kupitia vyombo mbalimbali vya habari, yakiwemo magazeti, televisheni, redio, mitandao ya jamii na kampeni za mitaani.

Lakini, binafsi naona jitihada kubwa zaidi, zinapaswa kuchukuliwa ili kuyafikia makundi maalum, mfano watu wenye ulemavu wa kusikia na ule wa macho. Watu hao wanatakiwa kupatiwa elimu kwa ukubwa uleule unaotolewa kwa wananchi wengine.

Jambo hilo linaweza kufanikiwa zaidi, kwa kupitia vyama vyao au kwa kumfikia mlemavu mmoja mmoja. Wasioona wanayo maandiko maalum, yanayoandikwa kwa kutumia nukta nundu, hivyo kinachotakiwa ni kuwa watengenezewe machapisho yao maalum ili wapate elimu husika.

Pia wasioona wanatakiwa kusaidiwa kunawa kila waendapo sehemu mbalimbali za watu. Kwa kufanya hivyo watakuwa wameshirikishwa kikamilifu na kuwaepusha kuathiriwa na virusi hivyo vya corona.

Pia kwa kuwa maofisa ustawi wa jamii na maofisa afya, wapo katika maeneo mengi nchini, nashauri maofisa hao walio chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wanapaswa kuhakikisha wanayafikia makundi hayo.

Wahakikishe makundi hayo na mengine yenye uhitaji, yanafikiwa na elimu ya corona. Pia jukumu la kusaidia makundi hayo ni la jamii inayowazunguka.

Kwa mfano, mtu mwenye ulemavu wa macho kwa kuwa hawezi kuona hata maji yalipo, basi jamii ndio inapaswa kumnawisha.

Ni imani yangu kuwa kwa pamoja serikali, chama cha wenye ulemavu wa macho na cha walemavu wa kusikia kwa kushirikiana na jamii, wanaweza kusaidia makundi hayo mawili, kukwepa kupata maambukizi ya virusi vya corona.

Misaada wanayoweza kupatiwa ni bidhaa zinazoweza kuwaepusha kupata maambukizi kama vile barakoa, vitakasa mikono, ndoo za maji na sabuni, bidhaa ambazo wenye ulemavu wengi hawawezi kuzipata wenyewe.

Ni vema kampuni na taasisi mbalimbali, zinazotoa vifaa vya kujikinga na corona, kuangalia uwezekano wa kusaidia makundi hayo maalum, kuyawezesha kupata elimu ya kukabiliana na corona kwa ufanisi zaidi.

Kwa pamoja tutaishinda corona na Tanzania kubaki salama yenye uchumi wake unaokua kwa kasi.

Baraza la Ushauri wa Watuamiaji wa Huduma za Mawasiliano Nchini ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi