loader
Picha

Uwekezaji unavyosaidia kukataa umasikini

FAMILIA nyingi za Kiafrika hasa mijini, zina utamaduni wa kutaka kukidhi kila matakwa ya watoto hata kama mahitaji hayo hayana msingi. Si ajabu kusikia watoto katika familia hizo wakililia kununuliwa chipsi na kuku, kwa madai tu kwamba, hatupendi ugali, maharage, mchicha au mtindi.

Maharage ndiyo kikwazo kikubwa kwa watoto. Familia nyingi zina utamaduni wa wazazi kuuliza watoto: “… mtakula nini?” jibu rahisi la watoto ni: “Chipsi kuku” “Zege” au siku hizi wengine wanasema:

“Kivuruge” yaani chipsi mayai; na kuku. Tatizo ni baadhi ya familia kuishi kwa shinikizo la watoto au kuiga. Uchunguzi umebaini kuwa katika sehemu nyingi Tanzania hasa mijini, bei ya kilo moja ya unga ni wastani wa Sh 1,500.

Hiyo, mnakula wote; na wakati mwingine kama si familia ya watu wengi, mnakula zaidi ya mlo mmoja. Lakini bei ya chipsi kuku ni kati ya Sh 4,000 na Sh 5,000. Hiyo, ni kwa mtu mmoja.

Hii ina maana kuwa, mkiwa watano, basi mnahitaji wastani wa Sh 25,000 kwa mlo. Kama mtafanya hivyo kwa wastani wa mlo mmoja kwa siku; mchana au usiku, kwa siku na kwa wiki nzima maana yake mnalazimika kutumia Sh 175,000. Hii ni fedha nyingi kwa mwezi na hata mwaka.

Mujuni James, mkazi wa PuguDar es Salaam, ambaye kitaaluma ni mhasibu anasema: “Fedha hizo zingeweza kuwekezwa.” Anasema: “Kiafya ugali na maharage, mchicha na mtindi ni vitu vyenye uwekezaji bora zaidi kuliko chipsi kuku…”

Theopista Mtwango, mamalishe katika eneo la Mwenge Dar es Salaam, anasema: “Wazazi na watoto tunakosea; hatuangalii kwamba kuna kesho na kesho kutwa; kuna kutibiwa kuna suala la shule na kuna umuhimu wa akiba hasahasa kuwekeza kwa manufaa ya baadaye.

Mamalishe mwingine wa Magomeni-Mapipa jijini humo anayekataa kutajwa anasema: “Chipsi, mayai, kuku na soda baridi zimeleta shida katika familia nyingi na mwishowe kusababisha umaskini…hapa ni muhimu kuchunga maisha maana kuna midomo mingi inahitaji uilishe na si kuilisha tu, bali na shida nyingine za maisha kama mavazi, maradhi hata malazi hasa katika familia zetu hizi za Kiafrika ambazo hata ndugu wengine kama wazazi nao wanakutegemea.”

Anasema mambo mengine zaidi ya hayo ni pamoja na kwenda ufukweni, mgahawani huku pia kukiwa na shida za kiukoo maana kwa Waafrika, mtoto wa mwenzio ni wako pia.

Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ya UTTAMIS, Daudi Mbaga anasema: “Kwa kipato chochote unachopata, jaribu kuweka kiasi hata kidogo kwa ajili ya dharura; lipa madeni yako kwa mpangilio maalumu, weka kiasi hata kidogo kama akiba ya uzeeni huku ukikumbuka ipo siku watoto wataenda sekondari au chuoni, pamoja na ugumu wa maisha pambana na hali yako.”

Anaongeza: “Wanaokuzunguka waambie ukweli kuwa huwezi kuwatimizia kila kitu, acha wakuchukie, lakini kama ni chipsi kuku wajifunze kutafuta kwa jasho lao. Wanaokutegemea waende kwa bajeti yako si kwa matamanio yao, waambie ukweli ili upate ziada kwa uwekezaji...” Vyanzo mbalimbali vinahimiza wategemezi wanaoweza kufanya kazi, watafute hata vibarua.

Mfano, wakati watoto wanasubiri matokeo ya mitihani na nyakati za likizo au baada ya kumaliza chuo ili waongeze pato la familia, wanapaswa kujisughulisha kwa namna mbalimbali halali kupata kipato.

Mbagga anasema: “Uliza kama watoto, ndugu chini ya familia yako wana madeni na yalikuwa ya nini? Je, kila mtu ana bima ya afya maana maradhi yanaweza kukutoa katika malengo yako na pesa yote ikaishia kwenye matibabu... Kama huna bima ya afya, unaweza kutumia hadi thumuni ya mwisho na pengine ukaingia hata kwenye madeni badala ya kuwa mwekezaji, sasa ukawa fukara wa kutisha.”

Anasisitiza: “Kwa watoto waambie ukweli kuhusu maisha; waambie maisha si rahisi na si chipsi, mayai na kuku, bali yanaweza kuwa rahisi kama watakuwa wawekezaji katika sehemu sahihi kama UTT-AMIS. Haya yawe mambo muhimu katika mpango wenu wa pamoja, kumbuka UTT AMIS ni kampuni ya serikali. Kataa umaskini kupitia uwekezaji.”

Kwa mujibu wa uchunguzi, hata unapokuwa na pesa kidogo unaweza kuwa mwekezaji katika mifuko hiyo na ukawekeza mara kwa mara kadri unavyopata.

“Mifuko hii inatoa faida jumuishi hivyo kuufanya mtaji na faida yako kuwa vizuri zaidi kadri miaka inavyosonga mbele,” anasema Mbagga na kuongeza:

“Kufanya hivyo ni kuwapa watoto wako upendo wa kweli, badala ya upendo wa chipsi, mayai na kuku. Kumbuka kila mtu ni muhimu, lakini hakuna mwenye umuhimu kama baba, mama na watoto (familia yako).

Inaelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa, kila jambo lina mtazamo na ufumbuzi wake tofauti, hivyo lazima kuwa makini vinginevyo, utatuzi wapendwa wako kama hao wanaweza kuwa chanzo cha mdororo wako kiuchumi.

Chanzo kimoja kinasema: “Kama wanakutegemea sana, kaa panga nao; angalia mpango upi utakuwa mzuri na utakuwezesha kuendelea na maendeleo yako ya kiuchumi vinginevyo mtakufa wote...”

Kinaongeza: “Ondoa hisia, angalia kila jambo kiuhalisia, tumia mifano halisi kwa kuwa kufanya hivyo si ukatili kwa watoto, au familia, bali ni nia njema kwani uchumi wako ndiyo uchumi wao.

Mbagga anasema: “Wekeza kwa bidii na ni vizuri kuanza kuwekeza ukiwa bado kijana. Kumbuka kuna siri kubwa kati ya uwekezaji na muda. Kumbuka japo thamani ya kipande inapanda na kushuka au inaendana na thamani ya mifuko, bado ukianza mapema utakuwa vizuri kiuchumi miaka ya mbele.”

Anatoa mfano akisema: “Ukiwekeza Sh 200,000 kwa mwezi, utakuwa umeweka Sh 24,000,000 kwa miaka 10. Kama pesa hizo zitakuwa kwa riba ya asilimia 10 kwa mwaka, utakuwa na Sh 40,968,995.78.”

“Kama riba ikawa asilimia 12, uwekezaji wako utakuwa Sh 46,007,737.9 ndani ya miaka 10. Kama uwekezaji huo ni wa miaka 20, utakuwa umewekeza Sh 48,000,000 kwa asilimia 10 utakuwa na Sh 151,873,767.20 kama asilimia ni 12 utakuwa na Sh197,851,073.08,” anafafanua Mbaga.

Anasema hayo ndiyo maajabu ya uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Kumbuka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) inasisitiza kueleza ukweli kuwa thamani ya kipande inaweza kupanda au kushuka. Katika mafunzo mbalimbali kuhusu maandalizi ya kustaafu vyema, mtaalamu wa saikolojia, Dk Chris Mauki anasema kwa mfano kuwa, kuwekeza kwa malengo ya baadaye hasa kustaafu kunapaswa kuanza siku ya kwanza unapoanza kazi na si kusubiri kutumia mafao ya kustaafu ili kuwekeza.

Katika hili, Mbagga yeye anasema malengo ya baadaye si tu kustaafu, bali pia elimu kwa watoto.

“Fikiria wakifika chuo itakuwaje, wakifikisha miaka ambayo wanaweza kufanya kazi wasome huku wakifanya kazi ambayo si lazima iwe ya ajira..” Mfano, nyumbani mnaweza mkawa mnafuga mifugo kama kuku, ng’ombe, mbuzi na mingine, badala ya kuajiri mtu wa kuhudumia mifugo hiyo ni vizuri watoto wakapangiana zamu.

Pesa ambayo ungemlipa mfanyakazi kwa kazi hiyo inaweza kuwekezwa kwa maisha ya baadaye, kumbuka Sh 1,000,000 ikikaa ndani ya uwekezaji miaka 30 kwa kwa asilimia 15 itakupa Sh 66,000,000, hivyo, ingekuwa milioni mbili, tatu, nne, wakati wa likizo ndefu watoto wanaweza ongeza tija zaidi. Naye anapozungumzia maisha ya watoto katika taasisi za elimu hasa shule na vyuo, Mbagga anasema:

“Watoto waishi kwa gharama za bwalo za chuo na si kwa chipsi, kuku na mayai. Hii itawasaidia kuishi maisha halisi na si maisha ya kuiga baada ya chuo.” Anasema ili uweze kuwekeza, wapeleke watoto shule unazoweza kumudu gharama zake.

“Kumbuka kuwasaidia watoto au wanafamilia wako si kuwapa pesa tu; nenda nao kanisani, msikitini, shambani na wasaidie katika mipango yao. Wape watoto maarifa ya maisha ili wasiwe na akili za darasani pekee,” anasema Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT-AMIS.

NAMNA YA KUFANYA UWEKEZAJI

Mbagga anasema: “Kwanza epukeni ugomvi wa hela kati ya mke, mume na pengine hata ndugu ikiwemo wazazi. Ugomvi wa pesa umefanya familia nyingi kusambaratika kutokana na kila mmoja kuona mahitaji yake ni muhimu zaidi ya mwenzake na pale ambapo kila mtu anabajeti kivyake.”

Hatua nyingine ni kujadili kwa pamoja kuhusu matumizi yenu na mkwepe kukuza na kuchanganya mambo na kuhakikisha ugomvi haufuti mafanikio au makubaliano mazuri ya awali.

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi