loader
Picha

SMZ: Tunatekeleza yaliyoasisiwa na Karume

Ni takribani miaka 48 sasa tangu Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume alipouawa kikatili na wapinga maendeleo April 7 mwaka 1972 katika makao makuu ya chama kilichokuwa kinatawa Zanzibar cha Afro-Shirazi Party (ASP) ambapo sasa ni makao makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Tamko la Baraza la Mapinduzi mwaka 1972 liliweka bayana kwamba ‘’hayati Abeid Amani Karume ameuawa na kuzikwa lakini kilichokufa ni kiwiliwili chake tu, mawazo, busara na mambo yote mema yataendelea kulindwa na kuenziwa kwa faida ya wananchi wa Zanzibar.”

Leo tunapoadhimisha Karume Day, tumeshuhudia awamu mbali mbali za marais waliopata kuongoza Zanzibar wakiendelea kufuata nyayo na kuyalinda mambo yote ya msingi yaliyoanzishwa na kiongozi huyo.

Zanzibar inatajwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo katika Bara la Afrika kutekeleza kwa vitendo maazimio na matamko ya Jumuiya za Kimataifa yanayohusu haki za binadamu na utawala bora mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964.

Hata katika tamko lake la mwanzo mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964 lililotangazwa na Hayati Karume alisema Zanzibar itaongozwa kwa misingi ya kulinda utu wa binaadamu na kuwajali wazee pamoja na watoto yatima. Hatua hiyo ilikwenda sambamba na kuundwa kwa wizara inayoshughu

likia haki za wananchi sawa pamoja na kujenga nyumba za kuhifadhi wazee wasiojiweza ziliopo Sebleni Unguja.

“Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 yakiongozwa na hayati Abeid Amani Karume ndiyo yaliyokuja kuweka sawa utekelezaji wa haki za binaadamu ambapo makundi yote ya vijana, wazee na watoto yalitambuliwa rasmi,” anasema Haroun Ali Suleiman, Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Waziri Haroun Ali Suleiman akizungumza na gazeti hili kuhusu miaka 48 ya kifo cha mwasisi wa taifa hili, anasema Wizara yake na taasisi zake zinaendelea kutekeleza mambo yote ya msingi yaliyoasisiwa na Karume kwa vitendo.

Kwa mfano, anasema mamlaka ya kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi (Zaeca) kwa kiasi kikubwa imeweka misingi ya kupambana na rushwa kwa viongozi waliokabidhiwa majukumu ikiwemo wa Serikali na taasisi za umma.

Anasema rushwa ni aduwi wa haki na sehemu ambayo rushwa imetawala basi watu wa kawaida kwa maana ya wanyonge hawana nafasi ya kupata mambo ya msingi wanayostahiki kuyapata.

“Tumepiga hatua kubwa katika kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi katika sehemu za utoaji wa huduma... Tunawataka watu kutoa taarifa za rushwa ili tuwachukulie hatua za kisheria,” anasema.

Anasema hayati Karume alichukizwa na vitendo vya matajiri kuwakopesha fedha wananchi wanyonge na baadaye kuwatoza riba kubwa na hivyo kuwaweka katika maisha magumu.

“Mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12... Hayati Karume alipiga marufuku matajiri kuwatoza fedha wananchi wanyonge katika mfumo wa riba pamoja na rehani,” anasema.

Anasema Karume alianzisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu na kuongozwa na marehemu Mohamed Aboud ambaye baadaye alichukuliwa na kupelekwa Tanzania Bara na kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa kwanza mzalendo baada ya kuondoka kwa mzungu.

Aidha anasema kwa upande wa watumishi wa umma, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haipo nyuma ilitekeleza yale yote yaliyoasisiwa na Karume katika kujali watumishi wake.

Suleiman anasema Karume alikuwa akisema siku zote kwamba tumefanya mapinduzi kwa ajili ya wananchi walio wengi kushika hatamu ya kuongoza dola.

Anasema wizara yake imekuwa ikizingatia maslahi ya watumishi wake ikiwemo kuongeza mishahara mara kwa mara kadri hali ya mapato yanapokuwa nzuri na kuweka mazingira mazuri kwa kubuni kuwawekea fedha zao wakati watakapostaafu.

“Hayati Karume siku zote alikuwa akizungumza suala la hatma ya wafanyakazi na kuhakikisha wanakuwa na akiba yao wakati watakapostaafu... Ndiyo maana tumeanzisha mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF,” anasema.

Katika kongamano la utawala bora na haki za Binaadamu pamoja na maadili, Wizara ya nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilimtunuku na kumpa tuzo maalumu ya usimamizi na muanzilishi wa utawala bora Zanzibar rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein.

Tuzo hiyo ni pamoja na kutambuwa mchango wa Dk Shein katika kuyaendeleza mambo yote mazuri yaliyoasisiwa na hayati Karume katika kipindi cha uongozi wake wa miaka tisa.

Suleiman aliyekuwa Waziri wa Elimu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda wa miaka kumi 2000-2010 anasema hayati Karume anaendelea kuenziwa ambapo sekta ya elimu sasa inatolewa bure kwa wananchi wote kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.

“SMZ imefanikiwa kumuenzi hayati Karume vziuri sana hata katika jambo muhimu la elimu. Sasa elimu inatolewa bure pamoja na matibabu huku wazee wakiendelea kutunzwa katika nyumba bora na sasa pensheni jamii inatolewa kwa wazee wote waliofikisha umri wa miaka 70,” anasema waziri huyo mwandamizi wa SMZ.

Mapema akifunguwa kongamano hilo la utawala bora, Rais Shein alisema yeye ni muumini mkubwa wa dhana ya utawala bora pamoja na misingi yake muhimu ikiwemo iliyoasisiwa na hayati Abeid Amani Karume.

Dk Shein amekuwa akifuata na kusimamia mambo yote ya msingi yaliyoanzishwa na hayati Karume kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar ikiwemo elimu bure, matibabu bure na ujenzi wa makazi bora ya wananchi.

Dk Shein anasema katika kipindi chake cha uongozi wa takribani miaka tisa sasa amefanya kazi kubwa kuhakikisha mambo ya msingi yaliyoasisiwa na hayati Karume ambayo ndiyo yaliyopelekea kufanyika kwa mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yanadumishwa na kuenziwa.

Anayataja mambo hayo kuwa ni pamoja na elimu bure, matibabu bure pamoja na kuwapatia hifadhi bora wazee na makazi mazuri wananchi wa kawaida.

Anasema katika sekta ya elimu hivi sasa michango yote iliyokuwa ikitolewa na wazazi kwa ajili ya kuchangia sekta hiyo imefutwa na ni marufuku mzazi kudaiwa fedha kwa ajili ya gharama za elimu.

“Hayati Karume alitangaza elimu bure Septemba mwaka 1964 na mimi nimeamua kulinda na kuheshimu uamuzi huo ambapo nimefuta michango yote na hakuna mzazi atakayedaiwa kutoa fedha kwa ajili ya gharama za elimu,” anasema Dk Shein.

Aidha anasema serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 90 kwa ajili ya kujenga nyumba bora za kisasa, makazi ya wananchi hapo Kwahani ikiwa ni moja ya azma ya hayati Karume kuona wananchi wanaishi vizuri.

“Tumeanzisha mradi wa ujenzi wa makazi nyumba za ghorofa Kwahani mjini Unguja... Hayati Karume mara baada ya mapinduzi alianzisha mradi wa ujenzi nyumba za makazi katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuishi wananchi wake,” anasema.

Mifano ya wazi katika mambo muhimu ya kumuenzi hayati Karume yanayotekelezwa na Rais Shein katika kipindi cha uongozi wake ni pamoja na kuanzisha pensheni ya jamii kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazee Zanzibar (Juwaza) Masururu Saad Ferouz anasema kinachofanywa na Dk Shein katika kipindi cha uongozi wake ni kutekeleza yale yote yaliyofanywa na hayati Karume ikiwemo kuwahifadhi na kuwapatia matunzo bora wazee.

Ferouz anampongeza Dk Shein kwa kuanzisha pensheni jamii kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70 ambayo inatolewa bila ya ubaguzi huku zaidi ya wazee 28,022 wakifaidika na malipo hayo bila ya kujali kama mtu alikuwa mtumishi wa serikali au la.

“Sisi wazee tunampongeza kwa dhati Rais Shein kwa kuanzisha pensheni jamii na kuwapatia wazee Sh 20,000 kila mwezi bila ya ubaguzi.,’’ anasema Forouz.

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi