loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera serikali uwazi matumizi mkopo wa elimu

JUZI serikali iliweka wazi kuwa itazingatia makubaliano ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Elimu ya Sekondari (SEQUIP), uliofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 500 (Sh trilioni 1.135) na kutaka uvumi hasi kuhusu jambo hilo uachwe.

Serikali ilisisitiza pia kuwa itawashirikisha wadau wa elimu katika hatua zote za utekelezaji wa mradi huo utakapoanza, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kuhusu SEQUIP.

Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji na ubora wa elimu ya sekondari na kuwezesha watoto wa kike, waliokosa fursa ya kuwa shuleni rasmi, wanapata elimu kwa njia mbadala, kujenga mabweni na kuimarisha mifumo ya kidijitali.

Hatua ya serikali ya kuweka wazi msimamo huo, ilitokana na kuwepo kwa uvumi na uzushi katika mitandao ya kijamii kwa baadhi ya watu, kutoa maoni hasi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo, katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa juzi jijini Dodoma, alisema serikali imejipanga kutekeleza mradi huo ipasavyo. Aliwataka wananchi kupuuza uvumi kupitia mitandao ya kijamii kuhusu mradi huo.

Alisema uvumi huo, aliouita wa hali ya juu na maoni mbalimbali yasiyozingatia taarifa sahihi, yanayotolewa katika mitandao ya kijamii kuhusu SEQUIP, ni kinyume cha ukweli kuhusu mradi huo.

Alisisitiza kuwa serikali itashirikiana na wadau ili lengo la mradi huo la kuwafikia wanafunzi zaidi ya milioni 6.5 wa shule za sekondari nchini, lifikiwe.

Kwa dhati kabisa tunaipongeza serikali, kwa kutoa msiamamo huo, ambao bila shaka umewaumbua wale wote waliokuwa wanazusha mambo yasiyo sahihi kuhusu fedha hizo kupitia mitandao ya kijamii.

Tunaipongeza zaidi serikali kwa kuweka wazi kuwa inajipanga kutekeleza mradi huo kama ulivyokusudiwa na kupangwa na malengo yake mengine, kama ilivyokubaliwa na pande zote mbili, Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, moja ya makubaliano hayo (yaliyoridhiwa na Benki ya Dunia) ni kuwepo kwa mfumo wa kuwawezesha watoto walio nje ya shule, kupata fursa ya kufikia malengo yao ya kielimu kupitia njia mbadala iliyo rasmi.

Ni matumaini yetu kuwa kutokana na msimamo huo wa serikali, wadau wote watajitokeza na kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa mradi huo, unafanyika kikamilifu na kwa uwazi, hatua ambayo hatuna shaka itasaidia kwa kiwango kikubwa kufikia lengo la kuboresha elimu ya sekondari nchini kulingana na makubaliano baina ya Benki ya Dunia na serikali.

Hivyo, kwa dhati kabisa tunaipongeza serikali, kwa kuonesha uwazi wa matumizi ya mkopo huo wa mabilioni ya Benki ya Dunia katika kuboresha elimu na tunaamini Watanzania na dunia nzima, wameelewa nia ya dhati ya serikali katika kuwasaidia wanafunzi masikini wa Tanzania.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi