loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Umoja, mshikamano ngao yetu Watanzania

TANGU kuripotiwa kuingia nchini kwa maambukizi ya virusi vya corona (COVID- 19) katikati ya Machi mwaka huu, Watanzania wameendelea kudhihirisha kuwa linapotokea janga, huweza kushikamana na kuonesha uzalendo wa juu kwa Taifa lao.

Baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kutangaza kuripotiwa kwa mgonjwa wa kwanza wa virusi vya corona, Watanzania waliweka pembeni tofauti zao za kisiasa, kidini, kikabila na rangi na kugeuka kuwa taifa moja, lenye mwelekeo mmoja wa kupambana na ugonjwa huo.

Iliendelea kujidhihirisha zaidi pale viongozi wakuu wa taifa, Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walipojitokeza hadharani na kuwataka Watanzania kuchukua tahadhari za kila aina dhidi ya maambukizi, lakini bila kupeana hofu.

Mathalani, Watanzania wengi wameitikia vema mwito wa Rais Magufuli wa kuwataka kuendelea kuchapa kazi huku wakichukua hatua zote za tahadhari dhidi ya maambukizi ili kuepusha balaa kubwa lingine la kiuchumi, endapo watajifungia ndani kuogopa maambukizi.

Wameitikia pia mwito wa Rais wa kuwataka kuchukua hadhari, wanapokuwa katika nyumba za ibada, lakini watumie fursa hiyo ya kuabudu kumuomba Mungu kuiokoa dunia dhidi ya majanga mbalimbali, ikiwemo maambukizi ya virusi vya corona.

Maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi na mwitikio wa Watanzania, ulioegemea katika ari ya uzalendo, umoja, upendo na mshikamano, vimekuwa silaha kubwa katika kuzuia maambukizi kwa halaiki, ukilinganisha na mataifa mengine hususani ya jirani.

Taarifa ya jana ya Waziri Ummy, ilieleza kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa 14 wa corona na kufanya jumla ya watu walioambukizwa virusi hivyo tangu viliporipotiwa kuingia nchini kufikia 46 tu.

Hali hiyo ni tofauti na namna wadau mbalimbali, ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) walivyodhani.

Kwa mfano, WHO walitabiri kuwa hadi kufika katikakati ya mwezi huu (leo), Tanzania ingekuwa na maambukizi takribani 1,000 na hadi kufikia mwishoni mwa Mei au Juni mwanzoni, maambukizi hayo yangekuwa yamepaa na kufikia 10,000.

Ni tofauti pia na dhana ya baadhi ya nchi jirani, zilizokebehi mikakati na mbinu zinazotumiwa na Watanzania katika kukabiliana na maambukizi, hususani kitendo cha watu kutofungiwa ndani na kuruhusiwa kuendelea kuabudu, kama njia ya kuruhusu uwepo wa Mungu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Faida za mikakati na miongozo ya wakuu wa nchi, zinaonekana dhahiri, shahiri.

Tanzania sasa ni moja ya mataifa yenye wagonjwa wachache sana katika Ukanda wa Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara pamoja na kuwa kuna ongezeko la wagonjwa.

Watanzania wengi, ingawa si wote, wamebadili tabia, wana ari kubwa na wamehamasika kwa kiwango kikubwa kujilinda mtu mmoja mmoja, familia na jamii nzima kwa ujumla.

Dunia imeshuhudia namna watu wanavyonawa mikono kila mahali, kuanzia majumbani mwao hadi katika maeneo ya kazi na biashara.Ni kutokana na mwito wa Rais Magufuli, tumeshuhudia pia ibada na swala za aina yake makanisani na misikitini.

Wananchi wengi wanachukua tahadhari kubwa za kujilinda, wanakaa kwa nafasi, lakini pia wananawa mikono na kujikinga kwa njia nyingine wakati wanaabudu.

Huu ni uzalendo mkubwa na upendo kwa Taifa lao. Watanzania wanachukua hatua za kujikinga bila kufungiwa ndani, huku wakiendelea na shughuli za uzalishaji kutokana na kufahamu kuwa uchumi wa Afrika, haufanani na wa mataifa yaliyoendelea, hivyo nchi za Afrika hazipaswi kuiga hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo, kwani zikifanya hivyo zitajikuta katika majanga makubwa.

Ni ukweli ulio wazi kuwa kwa Afrika, asilimia 89.2 ya ajira zote ni ajira zisizo rasmi, ambazo watu hulazimika kufanya kazi kila siku ili wahudumie familia zao na wasipofanya hivyo, hawawezi kuishi.

Pia asilimia 90 ya biashara zote barani Afrika ni biashara ndogondogo (SMEs), ambazo huchangia asilimia 38 ya mapato ya bara hilo, hivyo kwa kuwafungia ndani watu, kuna uwezekano wa biashara hizo kufa na kusababisha uchumi kuporomoka kwa kasi.

Tunaipongeza serikali kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kuwaongoza Watanzania, kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Ushahidi upo wazi kuwa Watanzania wamebadili tabia, ingawa wapo wanaofanya utani, na wanaokebehi hatua zinazochukuliwa na wengine kukiuka maelekezo ya wataalamu.

Janga hili si la kufanyia mchezo hata kidogo. Ili kufanikiwa kulitokomeza, tunahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu. Sote tuwe askari wa mstari wa mbele, kwa kuhakikisha maelekezo yanafuatwa na sote tuwe walimu, kwa kuwaelekeza wote wanaokiuka.

Kila mmoja akitimiza wajibu wake, tutashinda vita hii, kwani umoja na mshikamano, ndio ngao yetu Watanzania.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi