loader
Msemaji anavyozingatia aseme nini, wakati gani

Msemaji anavyozingatia aseme nini, wakati gani

“BINAFSI napenda kuwa karibu sana na watu kwa kuwa siku zote naamini pasina mahusiano mazuri na watu basi usitarajie miujiza ya kupata mambo mazuri ya kimaendeleo, naipenda kazi yangu na naifanya kwa uaminifu wote.”

Anaanza kusema Frank Lukwaro, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari ambaye kwa sasa anahudumu kama Msemaji wa timu ya Polisi Tanzania inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu ya Tanzania ikifanikiwa pia kufanya vizuri na kuvishinda baadhi ya vilabu vikongwe vinavyoshiriki ligi hiyo.

Pamoja na nafasi hiyo ya uafisa habari lakini pia anakaimu nafasi ya ukatibu mkuu wa timu kwa kipindi chote cha msimu huu wa ligi kuu kwa ufanisi mkubwa kutokana na elimu ya Utawala wa Umma aliyoisomea .

“Nawashukuru sana IGP Simon Sirro, Mwenyekiti wa Timu Kamishna Charles Mkumbo na Msemaji wa Jeshi la Polisi SACP David Misime kwa ushirikiano wanaonipatia kwa kuwa wao ndio wanaotoa dira na miongozo ambayo ninapaswa kuifuata katika kazi zangu,” anasema Frank.

Anasema siku zote anaamini kuwa mafanikio ya timu hiyo mbali na umoja wa viongozi wote ndani ya jeshi la polisi, pia umoja na mshikamano kutoka kwa wachezaji na maofisa wa polisi na mashabiki wao hasa wa mkoani Kilimanjaro yanachangiwa na mapokezi mazuri ya timu kutoka kwa watanzania wote kwa ujumla.

Frank anasema kimsingi kwa nafasi yake ya usemaji katika timu hiyo inayoshika nafasi ya sita kati ya timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo ambayo hadi kusimama kwake kutokana na ugonjwa wa Covid-19 inaongozwa natimu ya Simba yenye alama 71 dhidi ya alama zao 45, inazidi kumjenga siku hadi siku huku akiamini kuwa mafanikio zaidi yanakuja mbeleni.

“Ndiyo kwanza tunashiriki ligi kuu kwa mara ya kwanza baada ya kufanikiwa kufanya vizuri katika ligi ya daraja la kwanza msimu uliopita, kule hakukuwa na changamoto kubwa, kwa sababu timu nyingi na ligi yenyewe haina ushawishi mkubwa ukilinganisha na ligi kuu, huku inakubidi kujipanga nini cha kuzungumza na kufanya kuibeba timu yako.” anasema Frank.

Anasema katika ligi hiyo ya ushindani yenye vilabu vikubwa na wasemaji nguli, yeye kama msemaji ana kilasababu ya kuhakikisha taarifa sahihi za timu zinawafikia wananchi kwa wakati na usahihi kwa usaidizi wa benchi la ufundi pamoja na viongozi wengine wa juu wanaohusika na timu hiyo.

Kwa mujibu wa Frank, kazi ya usemaji katika timu inampasa mtu mwenye weledi wa kutosha na anayejua kipi cha kuzungumza na kwa wakati gani na ulio sahihi huku akitoa ushirikiano mzuri kwa waandishi wa habari na mamlaka zingine zinazohitaji kupata taarifa za kina kuhusu timu, jambo analosema kimsingi linazidi kumuongezea uwezo wa kitaaluma.

Anasema akiwa katika timu hiyo anakutana na mambo mengi yakiwemo yenye changamoto ambazo inambidi kuyakabili kwa vitendo ili kuleta ufumbuzi huku akitambua kuwa moja ya jukumu lake kubwa katika timu hiyo ni kuitangaza vyema kila hatua inayopitia yakiwemo maendeleo ya wachezaji.

Frank anasema kwa kawaida yeye siyo mtu wa maneno mengi kama ilivyozoeleka kwa wasemaji wengine wa baadhi ya timu zinazoshiriki ligi hiyo kwani zaidi amezoea kufanya kazi kwa vitendo akiamini kuwa ndiyo kunatoa majibu mazuri ya uwajibikaji katika majukumu mbalimbali huku akisisitiza kuwa watanzania watarajie makubwa kutoka katika kikosi cha timu ya polisi siku za usoni.

“Ligi ilikuwa ikielekea ukingoni kabla ya kusimamishwa kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19, tulikuwa tunazidi kupambana kufikia nafasi za juu, malengo yetu kwa mwaka huu yalikuwa walau tuwe katika nafasi tatu za juu msimu huu…hatuna shaka kama tukiikosa basi msimu ujao tutakuja vizuri zaidi,” anasema Frank.

Anasema changamoto iliyowafanya wawe katika nafasi hiyo kwa sasa ni kutokana na uchanga wao katika ushiriki wa ligi hiyo lakini hata hivyo anasisitiza kuwa wameweza kupambana na kuonesha dhamira yao ya kuamua kushiriki ligi kuu.

Franka anasema kuanzishwa kwa timu hiyo kulikuwa na makusudi ya kuleta mabadiliko ya kisoka nchini wakiamini kuwa na kikosi cha timu iliyochini ya jeshi la polisi wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya soka hapa nchini hususani katika eneo zima la nidhamu kwa wachezaji, benchi la ufundi na timu kwa ujumla ukilinganisha na timu zingine.

Kuhusu suala hilo, Frank anasema kuwa ni jambo la kawaida katika timu hiyo kutokana na kulelewa katika misingi ya kijeshi mahali ambapo suala la nidhamu ni wajibu wa kila askari, hivyo kutokana na timu hiyo kuwa chini ya Jeshi la Polisi inatekelezeka pasina shaka kwa kufuata misingi yote.

Anasema matarajio ya baadaye ya timu hiyo ni kufanya vizuri katika michuano yote kuanzia ya hapa nyumbani na ile ya kimataifa akiamini kuwa kikosi hicho kitaifikia kutokana na malengo iliyojiwekea tangu kuanzishwa kwake hadi sasa inapoendelea kupambana ili kutimiza ndoto hizo.

“Kabla ya kuanzishwa kwa timu hii, mimi kama mpenzi na shabiki mkubwa wa mpira nilikuwa naishabikia moja kati ya timu kubwa za hapa nchini na mapenzi yangu kwa timu hiyo yalikuwa ya ‘kindakindaki’, lakini baada ya kuanzishwa kwa timu yetu hii mapenzi kule yalikufa kabisa na siku hata timu hizi mbili zinapokutana ndiyo huwa najiona nina furaha zaidi tena pale timu yangu inapoonesha ushindani wa kutosha,” anasema Frank bila kuitaja timu aliyokuwa akiishabikia.

Anasema ana upenda mpira kutoka ndani ya moyo yake na kwamba anatamani siku moja mtoto wake Lukwaro Junior aje kuwa mmoja kati ya wachezaji hodari ndani na nje ya taifa hili huku akidai kuwa tayari ameanza kuonesha mapenzi na mpira licha ya umri mdogo wa miaka mitano aliyonayo.

Kuhusu maisha yake, anasema kuwa yeye ni baba wa mtoto mmoja kutoka kwa mke wake wa ndoa ambaye siku zote amekuwa akimsifu kwa kumsaidia katika malezi ya familia wakati anapokuwa safarini katika maeneo mengi ya nchi kwa ajili ya ushiriki wa timu yake katika michezo mbalimbali.

“Nilioa miaka sita iliyopita, tunaishi na mke wangu tukiwa na mahusiano mazuri, namshukuru kwa kuwa amekuwa mvumilivu wakati wote ambao nakuwa mbali na familia yangu, kama unavyojua timu husafiri maeneo mbalimbali hapa nchini kwa nyakati tofauti hivyo kunifanya kutumia muda mwingi mbali naye,” anaongeza Frank.

Kuhusu mambo anayoyapenda, anasema mbali na mpira pia hupenda kusikiliza muziki na kusoma vitabu vya hadithi hapa na pale anapopata nafasi ya kupumzika akiamini kuwa kwa kufanya hivyo kunamsaidia kutambua mambo mbalimbali.

Pamoja na hilo anasema anapopata nafasi hupendelea kuwa karibu na marafiki kwa ajili ya kubadilishana mambo mawili matatu ya kimaendeleo na kusisitiza kuwa kwa kufanya hivyo pamoja na mambo mengine humsaidia kupata mawazo mapya yenye kujenga wakati wote.

Anasema asichokipenda katika maisha yake ni kuona watu hasa vijana wakikaa vijiweni na kupiga porojo bila kujishughulisha kwa chochote, akisema kuwa hali hiyo inatokana na mazoea ya uvivu usio na tija yoyote kwa maendeleo yao na taifa hili kwa ujumla.

Frank amesoma elimu ya msingi, sekondari hadi kidato cha nne, kisha alijiunga na Shule ya Uandishi wa Habari Royal na alijiendeleza zaidi na kuchukua Shahada ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu Huria (OUT).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e2c45f907338a8107d7ddb8f7c476fbd.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi