loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ujumbe wa matumaini wa WHO na mapambano dhidi ya corona

DUNIA imezizima, watu ‘wamejifungia ndani’ huku wengine wakitoka kwa tahadhari kwenda kujitafutia riziki, kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Ugonjwa huo, tangu uibuke katika Jimbo la Wuhan nchini China, Desemba, mwaka jana mpaka sasa umeshaambukizwa kwa watu zaidi ya milioni 2.6 duniani, kuua watu zaidi ya 184,325 huku zaidi watu 723,192 wakipona. Hii ni kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali kuelekea mwishoni mwa juma. Corona ni virusi vinavyoweza kusababisha magonjwa kwa wanyama (mamalia na ndege) lakini pia kwa binadamu.

Inaaminiwa ni aina ya virusi vilivyohama kutoka kwa wanyama na kuathiri binadamu pia. Kwa mujibu wa Wikipedia, virusi vya corona huwa na uwezo wa kubadilika na aina nyingi husababisha magonjwa yasiyo hatari kwa binadamu.

Kudhoofika kwa mwili kutokana na mashambulio ya virusi hivyo, kunafungua milango kwa bakteria wabaya kuvamia na kusababisha maambukizo ya mfumo wa upumuo, kama mafua au homa ya mafua (influenza), yanayoisha kwa kawaida baada ya siku kadhaa. Hadi sasa hakuna chanjo au dawa ya kudhibiti virusi vya aina hiyo. Uponyaji hutegemea huduma na nguvu ya kinga mwilini wa mtu.

Virusi hivi ni hatari hasa kwa wenye kinga za mwili zilizodhoofika. Takwimu zinaonesha kuwa, maambukizi katika nchi za Afrika yanaongezeka. Takwimu zilizopo zinatisha. Kwa msingi huo, kila nchi imechukua tahadhari mbalimbali huku elimu ikipewa kipaumbe. Nchini Tanzania, Rais John Magufuli amewahimiza Watanzania pia kumtanguliza Mungu katika vita dhidi ya corona.

Kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima na hata baadhi ya shughuli kama utoaji wa elimu katika shule na vyuo zimezuiliwa katika nchi nyingi. Nchi nyingine zimeweka zuio la watu kutembea au kutoka ndani kwa muda kadhaa. Safari za ndege za kimataifa zimezuiwa katika mataifa mengi.

Kibaya zaidi, wameibuka baadhi ya watu ama wa ndani au nje ya nchi wanaojaribu kutishiana kuzua hofu miongoni mwa jamii kutokana na kusambaza taarifa zisizo sahihi, bali za kuitishana hasa kupitia mitandao ya kijamii. Serikali ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli inapambana dhidi ya watu wa namna hiyo na wengine wamebainika na kuchukuliwa hatua.

Juhudi hizi hazina budi kuendelea ili taarifa zitolewe na mamlaka husika pekee. Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limeingilia kati na kuwatoa watu wasiwasi kuhusu ugonjwa huo huku likiwataka kuchukua tahadhari kujiepusha na maambukizi. Mkurugenzi wa WHO, Dk. Tedross Adhamon Ghebreyesus katika ujumbe wake hivi karibuni anaeleza njia tano za kufuata kwa kila mtu ili kuwa salama.

Anasema: “Familia yangu pia haina tofauti na nyie, mtoto wangu shule yake imefungwa na sasa anapata mafunzo yake kupitia mitandao, lakini pia tumeona hata hali mbaya inaweza kubadilika kwani kuna nchi zilikuwa zinapitia wakati mgumu lakini sasa zinaleta matumaini.”

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, ni muhimu kila mtu kuhakikisha anatunza na kuilinda afya yake ya mwili na akili kwani ndiyo silaha itakayomsaidia. Njia hizo kwa mujibu wa mkurugenzi huyo ni pamoja na kula vizuri kwa afya ili kusaidia kinga za mwili kufanyakazi vizuri.

Anashauri watu kujizuia kunywa kupita kiasi hasa vilevi na vinywaji vyenye sukari sambamba na wanaovuta sigara kuacha kwani uvutaji huongeza hatari ya kuwa na magonjwa nyemelezi mtu anapokumbwa na virusi vya corona. Anashauri kila mtu kufanya mazoezi kwa kuhakikisha anatenga muda wa dakika 30 kufanya mazoezi ya mwili kwa watu wazima na saa moja kwa watoto.

“Kama nchi yako inaruhusu unaweza kutembea au kuendesha baiskeli, lakini kwa kuhakikisha unakaa mbali na watu wengine, lakini kama huruhusiwi hata ndani unaweza kufanya mazoezi kupitia programu za video, cheza muziki, fanya mazoezi ya yoga au panda na kushuka ngazi,” anafafanua.

Anasema kwa wale wanaofanyia kazi nyumbani ni vyema kuhakikisha hawakai eneo moja kwa muda mrefu, bali kuamka na kutembea kwa dakika tatu kila baada ya nusu saa. Mintarafu kulinda afya ya akili, Dk Tedross anasema: “Kila mtu ahakikishe anatunza na kulinda afya yake ya akili. … Ni kawaida mtu kupatwa na wasiwasi au kuchanganyikiwa linapotokea tatizo hivyo, ukiwa na hali hiyo zungumza na watu unaowafahamu hiyo itasaidia.”

Anasema pia ni vyema kusaidia jamii inayokuzunguka jambo litakaloongeza amani ya moyo. Fuatilia afya ya majirani zako, ndugu jamaa na marafiki.

“Huruma ni dawa sikiliza muziki, soma kitabu au cheza mchezo wowote unaokufurahisha na jaribu kutosoma au kufuatilia habari kwa sana kama zinakuongezea wasiwasi. Pata taarifa zako kutoka vyanzo vya uhakika,” anasisitiza.

Inasisitizwa kuwa ili kupambana kudhibiti maambukizi, watu waepeke mikusanyiko isiyo ya lazima, wakae umbali wa zaidi ya mita moja kutoka kwa mtu moja hadi mwingine, wanawake maikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka au kutumia vitakasa mikono, pamoja na kuvaa barakoa.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi