loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bravo Tanzania vita ya malaria

KATIKA ukurasa wa tano wa gazeti hili kuna habari inayoeleza kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Habari hiyo inaeleza kuwa, kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo nchini kimepungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017.

Aidha, maambukizi mapya ya ugonjwa huo yamepungua kwa asilimia 19, kutoka wagonjwa 150 mwaka 2015, hadi wagonjwa 122 kwa kila watu 1000 mwaka 2019, huku vifo vitokanavyo na malaria vikipungua kwa asilimia 67 kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi vifo 2,079 mwaka 2019.

Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani.

Sisi tukiwa sehemu ya jamii, tumefarijika kuona jitihada zinazofanywa na serikali pamoja na jamii kwa ujumla kupambana na ugonjwa huo unaoelezwa kuua watu wengi kila mwaka kuliko magonjwa mengine, zimeanza kuzaa matunda.

Ugonjwa wa malaria umekuwa tishio kubwa kwa afya na maisha ya watu wengi barani Afrika ikiwamo Tanzania, hivyo habari kwamba umeanza kupungua nchini kwetu ni za kutia faraja.

Hata hivyo, tunapenda kutoa rai kwa serikali na jamii nzima kuongeza nguvu katika mapambano haya ili hatimaye tuweze kuutokomeza kabisa ugonjwa huu hapa nchini kwani ni jambo linawezekana. Kila mmoja wetu anapaswa kuendelea kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria ili kuepuka madhara yanayotokana na ugonjwa huu na hatimaye tuweze kuutokomeza kabisa hapa nchini.

Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kupambana na ugonjwa huu ikiwamo udhibiti wa mbu kwa kutumia njia mbalimbali kama kunyunyizia viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu na upuliziaji dawa ya ukoko katika kuta ndani ya nyumba kwenye halmashauri zenye maambukizi makubwa.

Pia imekuwa ikigawa vyandarua, ambapo kwa mwaka 2019, jumla ya vyandarua 6,936,202 viligawiwa kwa makundi maalumu wakati wa kliniki za watoto na shule za msingi katika mikoa 14 nchini ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Katavi, Tabora, Kigoma, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga, Kagera na Simiyu.

Hata hivyo wakati tukitoa kongole kwa mafanikio yaliyopatikana katika mapambano haya, tunapenda kusisitiza jamii kuendelea kushiriki kikamilifi kutokomeza ugonjwa huu kwa kutumia kwa usahihi vyandarua vyenye dawa, matumizi sahihi ya dawa za malaria, kutunza na kuweka mazingira katika hali ya usafi; kuharibu mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi na kuondoa maji yaliyotuama na kusafisha mifereji.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi