loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Udhibiti corona, nzige uende sambamba EAC

MATAIFA duniani kwa sasa yapo katika vita kali ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (covid-19) ambayo mpaka sasa imeua maelfu ya watu duniani, ikiwamo Tanzania.

Juhudi kubwa zimeelekezwa katika vita hiyo ili kuokoa maisha ya watu yanayoangamia kila siku kutokana na ugonjwa huo hatari unaoenea kwa kasi.

Ni jambo la kutia moyo na kuleta matumaini kuona mataifa yakiwamo ya Afrika Mashariki yanavyopambana kwa nguvu zote ili kuutokomeza ugonjwa huo hatari.

Lakini wakati mapambano dhidi ya maambukizi ya corona yakiendelea, tunapenda kukumbusha kwamba, mataifa yetu hasa ya Afrika Mashariki, yasisahau kwamba bado yanakabiliwa na mashambulizi ya wadudu wanaoharibu mazao aina ya nzige wa jangwani.

Ni bahati mbaya sana, kwamba mataifa ya Afrika Mashariki wakati yakiwa yanajipanga kuangamiza wadudu hao yalipovamia kwa mara ya kwanza, likaibuka hili la corona, hivyo kusababisha nguvu kuhamishwa kwenye kupambana dhidi ya ugonjwa huo.

Hivi karibuni, taarifa ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), ilieleza hali ya chakula katika Bara la Afrika, likisema baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zitakuwa na uhaba wa chakula kutokana na kukabiliwa na wimbi la pili la nzige wa jangwani lenye ukubwa mara 20 ya awamu ya kwanza iliyoanzia huko Ethiopia.

Shirika hilo linasema, katika wimbi la kwanza la uvamizi wa nzige, wadudu hao walitaga mamilioni ya mayai aridhini katika maeneo waliyopita, ambayo yataanza kutotolewa wakati wowote kuanzia sasa, hivyo kuzuka upya wimbi jingine kubwa la nzige kuliko la kwanza na kufanya uharibifu mkubwa kwenye mazao na mimea mingine.

Hivyo, tunapenda kuyakumbusha mataifa ya Afrika Mashariki kuwa, pamoja na mapambano makali yanayoendelea dhidi ya virusi vya corona, yasisahau wakati huohuo kuna vita nyingine ya kupambana na wadudu hawa waharibifu ili kujinusuru na baa la njaa.

Tunatoa wito kwa mataifa hayo kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya kupambana na wadudu hao, ikiwamo kuandaa dawa za kunyunyuzia, kuwaandaa wananchi jinsi ya kukabiliana na nzige hao, pamoja na kutambua na kutoa taarifa haraka kwa viongozi wao juu ya uwapo wa wadudu hao katika maeneo yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Pia tunashauri serikali kuandaa wataalamu wa kilimo wa kutosha na kuwapa mafunzo maalum ya kukabiliana na nzige mahali popote watakapoingia katika ardhi ya Tanzania kabla hawajaleta madhara kwa wakulima nchini.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi