loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vifo vya vigogo vyatikisa

SERIKALI na Watanzania wamepata pigo kubwa kuondokewa na watu mashuhuri waliowahi kuwa viongozi katika sekta binafsi na umma na kuleta mchango chanya kwa jamii wakiwamo majaji wakuu wawili wastaafu, Augustino Ramadhani (75) na Ali Haji Pandu.

Viongozi wengine waliofariki kwa nyakati tofauti katika kipindi cha siku mbili zilizopita, ni Jaji mwingine mstaafu Mussa Kwikima, Mkurugenzi mstaafu wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote, Wakili Gaudious Ishengoma na mdogo wa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, Ben Lowassa.

Rais Dk John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Jaji Mkuu mstaafu Ramadhani, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, watumishi wa mahakama na waumini wa Kanisa la Anglikana kwa kifo hicho.

Wakati familia zikisubiri ripoti ya vipimo vya kitabibu ili kuruhusu maziko yao kuendelea kwa uangalifu na tahadhari kubwa ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, aliyewahi kuwa Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah, alizikwa juzi usiku na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda alizikwa jana wilayani humo.

Taarifa fupi ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma iliyosambaa jana katika mitandao ya kijamii ilithibitisha kifo cha Jaji Augustino Ramadhani na baadaye gazeti hili lilipata taarifa pia kutoka kwa familia yake.

Mtoto wa marehemu Jaji Ramadhani (75), Brigdet Ramadhani aliliambia gazeti hili kwa simu jana kuwa, ni kweli baba yao alifariki jana saa mbili asubuhi katika Hospitali ya Aga Khan kutokana na shambulio la moyo, lakini alikuwa akisumbuliwa na tatizo la tezi dume kwa zaidi ya miaka 10.

“Ni kweli baba amefariki leo kati ya saa moja hadi saa mbili asubuhi lakini ameugua kwa muda mrefu zaidi ya miaka kumi tezi dume. Februari 18, mwaka huu hali ilibadilika akalazwa Aga Khan kwa wiki mbili, kisha akapelekwa Nairobi kwa wiki tatu, akarudi nyumbani akiwa anaendelea vizuri…juzi akapata heart attack (shambulio la moyo) na asubuhi akafariki,” alisema Bridget akifafanua kuwa baba yao ameacha mke, watoto wanne (wawili wa kike na wawili wa kiume) na wajukuu watano.

Wasifu wa Jaji Ramadhani Alizaliwa Desemba 28, 1954 Kisima-Majongoo, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya watoto wanane wa Mwalimu Mathew Ramadhani na mkewe Mwalimu Bridget Masoud.

Alisoma Shule ya Msingi Mpwapwa kuanzia mwaka 1952-1953 na baadaye Town School ya Tabora kuanzia mwaka 1954-1956. Mwaka 1957 hadi 1958 alisoma shule ya “Kaze Hill” (sasa Itetemia) pia Tabora na kutokana na baba yake kurejeshwa tena Mpwapwa, alimalizia elimu ya msingi wilayani humo mkoani Dodoma.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi na kufaulu vizuri, alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tabora Boys kuanzia mwaka 1960-1965. Alijifunza kupiga piano akiwa katika shule hiyo akirithi kipaji cha babu yake ambaye pia alirithi jina lake, Augustino Ramadhani. Alijifunza pia mpira wa kikapu na aliumudu.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea fani ya sheria akiwa mmoja wa Watanzania wa mwanzo kusoma kozi hiyo. Akiwa chuoni hapo alikumbwa na kashikashi la mgomo wanafunzi wakipinga masharti ya kujiunga kwa lazima na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ingawa hakugoma, lakini aliathiriwa na mgomo huo na kufukuzwa chuo, alirejeshwa Julai 1967 na kuhitimu mwaka 1970.

Mwaka 1978 alipata Shahada ya Uzamili ya Sheria za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (USDM). Ana shahada ya Uchungaji aliyoipata katika Chuo Kikuu cha London nchini Uingereza mwaka 2004. Machi 1970, baada ya kumaliza shahada ya kwanza chuo kikuu, alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Baada ya miaka mitano, alifunga ndoa Novemba Mosi mwaka 1975 na Saada Ramadhan Mabrouk. Aliteuliwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1978. Hata hivyo, alirejeshwa JWTZ mwaka 1979 na alishiriki vita ya Kagera jukumu lake kubwa likiwa kuendesha mahakama za kisheshi.

Aidha, Januari, 1980, aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar akiwa Luteni Kanali. Alihudumu cheo hicho hadi mwaka 1989 Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alipomteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania. Jaji Ramadhani alistaafu rasmi JWTZ mwaka 1997 akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali na kuagwa kwa heshima zote za kijeshi. Mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Aliteuliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) mwaka 2002 hadi 2007. Aliwahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2007. Mwaka 2007, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania hadi Desemba 2010 baada ya kufikisha miaka 65, muda wa kustaafu kwa lazima kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Jaji Mkuu mstaafu mwaka 2010 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu. Alipopata nafasi ya kutumika kama jaji aliondoka kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Baada ya kustaafu alirejea CCM Septemba 2011 katika Tawi la CCM, Oysterbay jijini Dar es Salaam na mwaka 2015 alikuwa miongoni mwa wanaCCM walioingia katika kura za maoni kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano.

Mwaka 2012 alitunukiwa Tuzo Maalumu ya Dk Martin Luther King na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt kutokana na utumishi wake uliotukuka na hivyo kuwa Mtanzania wa 13 kupokea tuzo hiyo. Aidha, mwaka huo, Rais Kikwete alimteua Jaji Ramadhani kuwa Makamu Mwenyekiti Tume ya Katiba na alitoa mchango mkubwa kwa tume hiyo.

Ni Mchungaji wa Kanisa la Anglikana. Alitawazwa kuwa Mchungaji wa Anglikana Dayosisi ya Zanzibar Kanisa la Minara Miwili, Unguja Desemba mwaka 2013. Mbali na uchungaji, ni mpiga piano kanisani. Rais Kikwete pia alimtunuku Jaji Ramadhani Nishani Maalumu ya Utumishi Uliotukuka katika maadhimisho ya miaka 53 ya Uhuru Desemba 9, 2014.

Septemba 2014, alichaguliwa kuwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu baada ya kuonesha uwezo mkubwa akiwa jaji wa kawaida wa mahakama hiyo.

Alihudumu hadi alipomaliza muda wake Septemba 2016. Rais Magufuli amlilia Kutokana na kifo hicho, Rais Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia yake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Juma na waumini wa Kanisa la Anglikana kufuatia kifo hicho. Amesema Jaji Mkuu mstaafu Ramadhani atakumbukwa kwa utumishi uliotukuka kwa nchi yake, ulioshadidishwa na umahiri wake, ukweli, uchapakazi, uzalendo wa kweli, na ucha Mungu.

“Nakumbuka nilipokwenda kumuona hospitali mazungumzo yake yalikuwa ni ya kumtumaini na kumtegemea Mungu, kwa hiyo na mimi namuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina,” alisema Rais Magufuli katika taarifa iliyotolewa na Ikulu toka Chato mkoani Geita.

Jaji, Mwasisi wa CUF Wananchi na wanasiasa wa vyama vya CCM, CUF na ACT-Wazalendo wameshiriki katika maziko ya aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kwanza mzalendo wa Zanzibar, Ali Haji Pandu. Pandu pia mwanzilishi wa Taasisi ya Kamahuru iliyozaa Chama cha Wananchi (CUF). Jaji Mkuu Pandu (82) alifariki nyumbani kwake Magomeni mjini Unguja juzi na kuzikwa kijijini kwake Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja jana.

Maiti ilisaliwa Msikiti Al-noor uliopo Mombasa kwa Mchina na kuhudhuriwa na viongozi na wanasiasa akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Maalim Seif Sharif Hamad, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Othman Makungu na wananchi wengine kabla ya maiti kupelekwa kijijini kwao kwa mazishi.

Pandu alikuwa Jaji Mkuu wa Kwanza mzalendo katika miaka ya 1970 hadi 1978 akiwa pia Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi. Alikuwa pia Waziri wa Maji, Nishati na Ardhi katika miaka ya 1984 hadi mwaka 1988 wakati alipofukuzwa CCM na wenzake wanane kwa madai ya kukiuka masharti ya chama na serikali.

Mwanasiasa aliyekuwa Mwakilishi wa CUF Jimbo la Mji Mkongwe na sasa yupo ACT-Wazalendo, Ismail Jussa alimtaja Pandu kuwa kiongozi aliyesaidia kwa kiasi kikubwa katika harakati za kisiasa na demokrasia Zanzibar hadi kuingia kwa mfumo wa vyama vingi. Atakumbukwa katika miaka ya 1972 ndiye aliyesikiliza kesi ya uhaini ya mauaji ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume aliyeuawa kikatili Aprili 7, 1972 Kisiwandui na wapinga maendeleo.

Kesi ya uhaini namba 292 ilianza kusikilizwa Jumatatu Mei 14, 1973 na Jaji Mkuu Pandu na kuendeshwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wolfgang Dourado pamoja na msaidizi wake Ussi Khamis Haji. Kesi ilimalizika Mei 15, 1974 ambako washtakiwa 43 walihukumiwa adhabu ya kifo, huku washtakiwa 11 wakihukumiwa kwenda jela miaka 15, na 16 waliachiwa huru baada ya kukosekana ushahidi na mmoja kufariki dunia wakati akiwa kizuizini.

Jaji Kwikima Chama cha ACT Wazalendo katika ukurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii kiliweka taarifa rasmi ya kifo cha Jaji mstaafu Mussa Kwikima (81). Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema kifo hicho kimetokea juzi Aprili 27, mwaka huu katika Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam.

Shaibu katika taraifa hiyo alisema hadi mauti yanamkuta Jaji Kwikima alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini na Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya ACT Wazalendo. Aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Mshauri wa Chama. Mtoto wa marehemu, Athumani Kwikima alieleza kuwa baba yao alifanyiwa upasuaji wa tezi dume Juni mwaka jana na wiki mbili zilizopita alikuwa mkoani Tabora akiwa mzima wa afya. “Jumapili wiki iliyopita alikuja kwa kaka yangu Upanga, Dar es Salaam kwa kliniki.

Lakini alianza kujisikia vibaya na Jumatatu alivyopelekwa Hospitali ya Kairuki, alikutwa sukari imepanda hadi 30. Madaktari walifanikiwa kuishusha hadi 14.5 wakashauri asirudi Tabora kwanza.

“Juzi saa tisa usiku akaanza kutetemeka na tulijaribu kumpa soda lakini alitapika sana, akakimbizwa hospitalini Kairuki na madaktari wakasema alishafariki. Baba hakuwa na historia ya ugonjwa wa kisukari kabisa. Tunasubiri taarifa ya serikali kuona utaratibu wa maziko uweje,” alisema Athumani.

Kamote wa CTI afariki Uongozi wa CTI jana ulitangaza kifo cha mkurugenzi wao mstaafu, Hussein Kamote (66) aliyefariki Aprili 26, 2020. Kwa mujibu wa CTI, Kamote alistaafu ya ukurugenzi mwaka 2015 na alishiriki katika mijadala kutaka Tanzania kuwa nchi yenye ushindani safi wa kibiashara na amzingira bora ya kibiashara nchini.

Mtoto wa marehemu, Kibaja Kamote aliliambia gazeti hili jana kuwa baba yake alikuwa na tatizo la kisukari la muda mrefu na wiki moja ilitopita alitibiwa UTI na kupona, lakini ghafla sukari ilipanda hadi 16 na alitibiwa katika Zahanati ya Serikali ya Chanika na binafsi ya Glory to God, Kigogo ambako walifanikiwa kuishusha hadi 15.

“Juzi (Jumapili) saa tisa alfajiri kuamkia Jumatatu (juzi) hali ilibadilika akiwa nyumbani tunamfanyia dua. Alikuwa akipumua kwa shida sana na saa 10 alfajiri akakata kauli. Tulitoa taraifa Serikali ya Mtaa kwa utaratibu wa sasa lazima serikali ihusike na tulielekezwa kumpeleka Amana.

“Tunasubiri vipimo vya hospitali ili tujue utaratibu wa maziko, tulitamani akazikwe kijiji kwake Kilometa Saba, Muheza, Tanga,” alisema Kibaja na kubainisha baba yake ameacha mke, watoto saba na wajukuu wawili.

Wakili Ishengoma Simanzi imetanda tena katika fani ya sheria na jamii kwa ujumla baada ya taarifa za kifo cha Wakili maarufu Gaudiosus Ishengoma aliyefariki juzi saa 5 usiku katika Hospitali ya Aga Khan baada ya kuugua kwa muda mfupi. Mdogo wa marehemu, Steven Ishengoma alisema kaka yake alianza kujisikia kuishiwa nguvu na homa kali Ijumaa Aprili 24 na hali ikawa mbaya juzi na kukimbizwa hospitalini kabla mauti kumfika.

Enzi za uhai wake alifanya kazi serikali kama Mwanasheria wa Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha kabla ya kuacha na kuwa wakili wa kujitegemea. Alikuwa akiishi Tabata, Dar es Salaam na ameacha mke na watoto watatu. Alisema maziko yanasubiri ripoti ya kitabibu. Alikuwa shabiki mkubwa wa Klabu ya Yanga.

Mdogo wa Lowassa Msemaji wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Abubakar Liongo alithibitisha kiongozi huyo kufiwa na mdogo wake, Ben Lowassa aliyefia Hospitali ya Aga Khan juzi usiku kwa tatizo la shinikizo la damu na maziko yalikuwa yakisubiri ripoti ya madakatri ili shughuli za mazishi ziendelee. Shah, Mmanda, Naibu Meya wazikwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda aliyefariki Aprili 26, alizikwa jana eneo la Pemba Mvita katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Maziko yake yalihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa na wanafamilia wachache ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Mtoto wa marehemu, Herman Mmanda alisema Mtwara wameiacha na alama kubwa ambayo hawatakaa na kuisahau katika maisha yao yote. Aliishukuru uongozi wa mkoa huo kwa kwa jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika juu ya mzee wao ikiwemo kuuguzwa hadi shughuli zote za mazishi hayo.

Mzishi hayo yameendeshwa na Padri kutoka Jimbo Katoliki la Mtwara, Nickson Mbila. “Tulikupenda Mungu amekupenda zaidi pumzika kwa amani kwani “Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina la Bwana lihimidiwe.”

Aidha, taarifa za ndugu wa karibu wa aliyekuwa Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah zilieleza kuwa alizikwa juzi usiku jijini Dar es Salaam kwa usimamizi wa serikali.

Mazishi ya Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Ishihaka Sengo aliyefariki juzi yamefanyika jana saa 10 jioni katika makaburi ya Kibwe yaliyopo Kata ya Mlimani yakihusisha watu wachache.

Imeandikwa na Gloria Tesha (Dar), Khatib Suleiman (Z’bar), Sijawa Omari (Mtwara) na John Nditi (Moro).

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi