loader
Mbunifu mavazi aliyeajiri watu 17

Mbunifu mavazi aliyeajiri watu 17

“MWANZO wazazi wangu hawakukubaliana na maono yangu ya kuwa mvishaji. Kutokana na utashi na ari yangu ya kupenda sana mambo ya urembo, mapambo na mavazi , nilijiona tofauti sana nikawaomba wazazi wangu wanielewe. Ilikuwa taabu kidogo. Wao walitaka nijiendeleze zaidi kielimu niajiriwe.

“Walihitaji nipate elimu itakayoendana na thamani ya shule ya sekondari niliyosoma , walitaka mtoto atakayefanya kazi za ajira inayoendana na elimu, inayoendana na thamani ya fedha walizowekeza katika elimu yangu,” anasema Saida Msuya.

Hapa Morogoro anajulikana sana kama Mama Halima kutokana na kampuni yake ya Mama Halima African Fashion Limited.

Saida anasema kampuni hiyo ni ndoto yake lakini haikuja kwa urahisi kutokana na wazazi wake kumfikiria kivingine.

Pamoja na misukosuko yote ya wazazi kutomwelewa yeye aliona mafanikio ya maisha yake yalitegemea zaidi utekelezaji wa ndoto yake ambayo imejikita katika fani ya sanaa ya ubunifu mavazi , urembo na mapambo kupitia sekta ya ushonaji.

Mama huyo anasema katika mazungumzo kwamba ilibidi atumie maarifa zaidi kushawishi wazazi wake ili aweze kutimiza ndoto yake hiyo kwa kuwataka kwa makusudi wamuwezeshe kujifunza elimu ya ushonaji wa nguo.

“Wazazi wangu baada ya kutafakari kwa kina walikubali na kunipeleka Chuo cha Ufundi Nguo cha Mindu Tailoring Mart (kwa sasa maaarufu kama Heriet Tailoring Mart)…hapo ndipo nilipoanzia utekelezaji wa ndoto yangu kutoka katika kutengeneza mwanasesere hadi kuwa mmiliki wa kiwanda cha kuvisha jamii,” anasema Saida au mama Halima. Filosofia yake

Anasema anasimama kwenye filosofia ya kuwa maisha hayaishi katika kufanya kazi za ajira rasmi zinazotokana na elimu ya sekondari ama elimu ya vyuo vya juu ila maisha ni endelevu yanatokana na bidii na uthubutu na utekelezaji bila ya kufikiri maslahi na mafanikio ya muda mfupi.

“Ninaamini nguvu ya kupambana na umasikini kwa kukusanya nguvu za kiutendaji na kutafasiri kazi zaidi kuelekea katika mafanikio, hakuna mafanikio bila ya kufanya kazi,” anasema Saida.

Anabainisha kuwa kaulimbiu kwenye majukumu yake ni huduma bora , uaminifu , uadilifu kazini kwa wakati sahihi , huku akisimamia maono ya ubunifu na ushonaji wa nguo kwa kutumia rasilimali zinazopatikana nchini.

Saida anasema lengo lake mahususi ni kukuza na kuimarisha sekta ya viwanda vidogo vya nguo kwa wazawa ili kupunguza utegemezi wa nguo zinazotoka ughaibuni kwa kutumia rasilimali za hapa nchini pamoja na kuuza bidhaa zake kwenye soko la kimataifa.

Saida au mama Halima ni nani?

Jina maarufu la Mama Halima linatokana na mwanawe wa kike na ndilo linaloakisi kazi yake katika sekta ya ubunifu ushonaji na uuzaji wa nguo katika jamii.

Alizaliwa mwaka 1978 akiwa ni mtoto wa pili katika familia ya bwana na bibi Zera Msuya.

Alipata elimu ya awali katika Shule ya Kituo cha Roho Mtakatifu, Kata ya Kiwanja cha Ndege , Manispaa ya Morogoro na kuendelea elimu ya msingi katika shule ya Msamvu tangu mwaka 1986 hadi mwaka 1992 na masomo ya Sekondari aliyapata katika Shule ya Sekondari ya Forest Hill na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1996.

Saida anasema baada ya kumaliza elimu ya sekondari, kutokana na utashi na ari aliyokuwa nayo tangu akiwa mtoto ya kupenda sanaa ya urembo wa mapambo na mavazi aliwaomba wazazi wake wamtafutie chuo cha kujifunza masuala yanayohusiana na mawazo yake licha ya wao kuwa na mawazo tofauti.

Mafanikio yake Anasema baada ya kumaliza masomo ya sekondari mwaka 1996 , mwaka uliofuatia (1997) alijiunga na Chuo cha Ufundi Mindu Tailoring Mart na kufanikiwa kuhitimu kwa kiwango cha juu cha umahiri na kuzawadiwa cheti maalumu.

“Mwaka 2003 nilianza kazi ya ushonaji nikiwa nimejiajiri binafsi kwa kuanza na mashine moja niliyoipata kwa mtaji toka kwa wazazi wangu,” anasema.

Saida anasema kutokana na kufanya kazi kubwa , bidii , uaminifu alifikia kiwango cha kufanya kazi kubwa na amefanikiwa kutoa ajira kwa mafundi wengine hadi kufikia mashine tano.

“Nikawa na wanafunzi watano ambao niliwaajiri ilipofikia mwaka 2005 , nilipata timu ya wachapa kazi kwa viwango vya juu, “ anasema.

Saida anasema mwaka huo huo ndipo wazo la kuanzisha Kampuni ya Mama Halima African Fashion Limited lilianza na baadaye alianzisha kampuni hiyo akiwa Mkurugenzi wa kwanza kushika nafasi hiyo anayoendelea nayo hadi sasa.

Anavyojiimarisha

Saida anasema katika kujiimarisha kwenye sekta hiyo hakuridhika na ujuzi alioupata awali katika fani hiyo, hivyo ilibidi apate mafunzo zaidi yanayoelekeza jinsi ya kufanya biashara kiufanisi zaidi na anaongezakuwa mwaka 2009 alihudhuria mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa biashara yaliyotolewa na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO).

“Mafunzo haya yaliniwezesha kuongeza idadi ya mafundi katika kiwanda na pia kuanzisha Kampuni Tanzu ya Mama Halima African Fashioni iliyojikita katika masuala ya upambaji na harusi, pia kuanzisha kampuni tanzu iliyojikita katika ushonaji wa mavazi ya harusdi au sherehe mbalimbali ijulikanao kama Zera Wedding Dress,” anasema .

Pia anasema kupitia mafunzo aliyopata yalimwezesha kufanya biashara za kimataifa kwa kuanzia Bara za Asia ( China )na shughuli kuu ikiwa ni kupeleka bidhaa za Kitanzania na zile zinazozalishwa katika kwanda chake na kuleta bidhaa toka China zinazouzwa katika duka lake la Zera Wedding Dress.

Hata hivyo anasema pamoja na hatua kubwa aliyopiga bado ana ndoto ya kufanikiwa zaidi na ndio maana anajiendeleza na kujipatia ujuzi zaidi kwa kujiwekea mkakati wa kutafuta na kushiriki katika mafunzo mbalimbali .

“Nimeshiriki mafunzo yaliyotolewa na mashirika mbalimbali kama vile SIDO, TCCIA, TWCC, TAN- TRADE, TASWE, BDG, NMB na CRDB,” anasema.

Atoa ajira

Saida anasema hivi sasa ameajiri wafanyakazi 17 kati yao 11 ni washonaji wakiwemo wanaume na wanawake , pia watatu ni wauzaji na wengine watatu wanafanya kazi ya kusambaza bidhaa zao nje.

“Kwa sasa kupitia kampuni zangu nimeweza kuajiri jumla ya wafanyakazi 17 ambao wapo katika idara za utawala , biashara , ushauri na mafunzo ya washonaji na wabunifu,” anasema.

Vile vile anasema wapo waliopata ajira za moja kwa moja ,lipo kundi kubwa la wamamitindo ambao hupata ajira za muda mfupi hasa wakati wa matamasha ya maonesho ya mitindo na biashara.

Saida anasena anasema pia kampuni yake imekuwa na mahusiano na wafanyabiashara wa nchi za Afrika , Ulaya na Marekani na kuzitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Zimbabwe , Namibia , Marekani na Uingereza.

Kwa mujibu wa mama huyo, anatumia malighafi vikiwemo vitenge vinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini na pia kutoka nje nchi kama Uganda , Kenya , Dubai, Nigeria , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na China.

Matunda ya kazi

Kutokana na ufanisi wa kazi zake Saida ameweza kujinyakulia tuzo zikiwemo za ushiriki wa maonesho ya kibiashara na mikutano ya kibiashara na ushiriki wa mashindano ya nafasi ya kijamii katika huduma na kujitoa kwa manufaa ya jamii.

Saida anazitaja tuzo alizopata za kitaifa kuwa ni pamoja na Tuzo ya Thamani ya Mwanamke na Ajira Binafsi , Mjasiriamali Bora, Mwanamke Sahihi na ya uongozi na pia kushiriki katika michango ya ujenzi wa jamii na utoaji wa huduma kwa kutoa misaada kwa jamii .

Anasema pia amekuwa akitoa mchango kwa kuendeleza jamii kwa kuwasaidia kukuza ujuzi , kujiimarisha kiuchumi na ujuzi kupitia Mama Halima African Fashion kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Ujerumani (SES) lenye programu ya muda mrefu ya kutoa elimu na mafunzo ya ushonaji nguo katika mkoa wa Morogoro.

“Kwa ufadhili wa SES tunatarajia kutoa elimu ya ushonaji na ubunifu kwa washiriki 18 mwaka huu,” anasema na anaongeza kuwa ili kuimarisha na kuuthaminisha ubunifu wa mavazi kulingana na mahitaji maalum amempeleka nchini India mwanawe Halima kwenye masomo ya miaka mitatu kuanzia Januari 2019, anasomea masuala ya ubunifu wa mavazi .

Mteja wake mmoja zaidi ya miaka 10 , Rosemary Semunyu ambaye alikuwepo eneo la kiwanda chake anamuelezea Saida au mama Halima kuwa ni mtu anayewajali wateja wake na bidhaa zake zina ubora na ushonaji wake unafanyika kulingana na hitaji la mteja wake .

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6d59102a4123d071c56611ce9e8893a9.JPG

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi