loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kasi kufikia uchumi wa viwanda inaridhisha

WIZARA ya Viwanda na Biashara imeeleza uwepo wa vipaumbele 10, vitakavyoharakisha safari ya taifa letu kuelekea uchumi wa kati, unaotokana na viwanda ifikapo mwaka 2025.

Pamoja na kuwepo kwa mikakati mbalimbali, pia wizara hiyo imeeleza uwepo wa mkakati wa kuendeleza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kimkakati na vya kielelezo nchini.

Mikakati hiyo imeainishwa na Waziri wa wizara hiyo, Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2020/21 bungeni mjini Dodoma.

Waziri Bashungwa amesema vipaumbele vingine vilivyopo ni kufufua viwanda vilivyobinafsishwa, kupanua na kukarabati vilivyopo na kuchochea au kuhamasisha uwekezaji au uanzishwaji wa viwanda vipya.

Vingine ni kuendeleza miundombinu ya msingi na saidizi ya maeneo ya uwekezaji na huduma ya viwanda kwa wawekezaji na wajasiriamali na uendelezaji na uwekezaji katika maeneo maalumu ya uwekezaji na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Pia, upo mkakati wa kuendeleza taasisi za utafiti na maendeleo ya teknolojia ya viwanda na kuvutia na kuchochea matumizi ya teknolojia ya kisasa na kulinda viwanda na biashara za ndani dhidi ya ushindani usio haki.

Pia kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapa elimu na mitaji, kuendeleza biashara na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi.

Kwa namna Waziri Bashungwa alivyowasilisha mikakati hiyo ndani ya Bunge; ni ukweli usiopingika kuwa ahadi ya Rais John Magufuli ya kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati unaotokana na ujenzi wa viwanda, itafikiwa bila shaka yoyote kabla au ifikapo mwaka 2025.

Tunasema hivyo kutokana na uhalisia, uliojionesha katika miradi ya kimkakati, ambapo karibu miradi yote ni ile inayochochea ukuaji wa uchumi na ukuzaji wa ajira kwa kiwango kikubwa katika nchi yetu.

Imani yetu kwamba taifa letu litaweza kufikia hatua hiyo, inapata nguvu zaidi kutokana na ukweli kuwa katika kipindi cha karibu miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano, kasi ya ujenzi au ufufuaji wa viwanda vikiwemo viwanda vidogo na vya kati imekuwa kubwa, hatua ambayo imewezesha kuongezeka kwa bidhaa za ndani na kupunguza wigo wa kuagiza bidhaa kutoka nje.

Kutokana na sababu hizo na nyingine anuai, tunashawishika kusema kuwa kasi kuelekea uchumi wa kati wa viwanda inaridhisha.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi