loader
LI GUAIQIONG: Mwanafunzi Mchina UDSM ‘anayeizimikia’ Tanzania

LI GUAIQIONG: Mwanafunzi Mchina UDSM ‘anayeizimikia’ Tanzania

“Wakati najiandaa kuja Tanzania mwaka 2017 baadhi ya walimu wangu, marafi ki na wazazi, walionesha wasiwasi waliposikia habari hizo. Walionesha wasiwasi kwa nini nilichagua kuja Afrika. Hawajawahi kufi ka Afrika, hivyo ufahamu mdogo kuhusu bara hili ni mdogo. Walihofu juu ya hali ya hewa, mafuriko, umasikini na magonjwa, lakini mimi nilipingana na mawazo na mitazamo yao na kusema nitaenda Tanzania.”

Hivyo ndivyo anavyosema raia wa China, Li Guaiqiong, nilipozungumza naye hivi karibuni. Walimu na marafiki hao wa Li hawapo peke yao, bali Wachina wengi hawalifahamu Bara la Afrika lilivyo na wanafahamu historia nyingi za nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupitia vitabu mbalimbali. Ukweli huo unaelezwa pia na Li mwenyewe.

Anafafanua kuwa alipata taarifa kuhusu Tanzania kupitia kitabu cha historia alichosoma ngazi ya sekondari. Anasema kwenye kitabu hicho, alijifunza juu ya uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa China, Mao Zedong.

Guaiqiong anasema kitabu hicho kilikuwa na picha nzuri yenye sura ya ukarimu na tabasamu zuri ya Mwalimu Julius Nyerere, jambo lililomfanya moja kwa moja kuamini kuwa tabasamu hilo, linaonesha kuwa hata wananchi wake, watakuwa na sura na roho nzuri kama ilivyo picha hiyo.

Anasema kusema ukweli hali aliyoiona baada ya kuwasili Tanzania mwaka 2017, haikuwa tofauti na ile aliyokuwa nayo kichwani akiwa kwao China. “Kusema ukweli kwa kipindi cha miaka miwili niliyoishi hapa Tanzania najisikia kama Mtanzania. Sijawahi kujiona nipo tofauti. Watu wengi hapa Tanzania ni wakarimu. Hii inanikumbusha kauli ya mwalimu wangu mmoja kule China, aliyeniambia chagua kwenda kufundisha Tanzania. Kwa hakika sijutii hata kidogo kauli yake ile,” anasema Li.

Kwa sasa Li ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ngazi ya Shahada ya Uzamili. Alikuja nchini mwaka 2017 kama mmoja wa walimu wa programu ya kujitolea.

Sababu za kuchagua Tanzania “Nakumbuka tulipomaliza mafunzo yetu kule China na kuanza kujiandaa kwenda kufundisha katika mataifa mengine duniani, mwalimu wangu mmoja aliniambia sehemu bora ya kwenda ni Tanzania, kwani ni nchi ya amani na pia ina uhusiano mzuri na China. Sikufikiria mara mbili, hasa nilipokumbuka kuwa ni kweli China na Tanzania ni marafiki wa siku nyingi, hivyo nikafanya uamuzi, nikachagua Tanzania,” anasema.

Anaeleza kuwa Septemba 2017 alipanda ndege kuja Tanzania, kuanza maisha yake mapya. Anasema alipofika Tanzania, alianza kuzoea taratibu hali ya mazingira na afanikiwa kupata marafiki wengi, hatua iliyomfanya kujiona kama yupo nyumbani kwao.

Upepo mwanana wa Dar Anasema kinachomfurahisha zaidi ni hali ya hewa ya Dar es Salaam. Anasema mwanzoni alidhani Dar es Salaam kuna joto kali la kuogopesha, lakini hali ilikuwa tofauti kwani jiji hilo lina mazingira mazuri na upepo wa kuvutia. Anasema amekuwa akijisikia fahari kwenda maeneo ya ufukweni wa Bahari ya Hindi na kufurahia upepo wa kutosha akiwa na baadhi wa jiji hilo.

Watanzania wafurahia maisha Anasema mbali na Dar es Salaam, ameweza kutembelea baadhi ya mikoa hapa nchini akiwa na marafiki zake na kufurahishwa na hali ya hewa ya mikoa hiyo.

Guaiqiong anasema huko mikoani, hali ya hewa ni nzuri na alibaini kuwa wananchi wengi, wanaendesha maisha yao ya kila siku kwa furaha, licha ya kukabiliwa na changamoto ndogo za umasikini

“Nilichoona ni kwamba ingawa watu wengi hawana fedha nyingi, lakini wanajitahidi kujipatia riziki yao kila siku. Wengi wao wanafurahia maisha kutokana na upendo na amani iliyopo,licha ya matatizo madogo madogo ya kiuchumi,” anasema.

Mifano ya ukarimu, upendo wa Watanzania Anasema kadri siku zilivyozidi kuongezeka tangu afike hapa nchini, taratibu alianza kuiga desturi za Kitanzania. Anasema amekuwa akifuatana na marafiki zake, wanafunzi wenzake darasani na walimu kila mahali. Kwa mujibu wa Guaiqiong, kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili alichoishi hapa nchini, ameweza kuishi maisha halisi ya Kitanzania na kuyafurahia.

Anasema kuna kipindi fulani alikwenda Rwanda na kukaa huko kwa siku tatu. Lakini, akiwa huko alitamani kurudi haraka Tanzania kutokana na uzuri wa Tanzania.

“Nawashukuru sana marafiki zangu Watanzania ambao kwa kipindi chote tangu nifike hapa, wamekuwa bega kwa bega na mimi na kunipa ushirikiano mkubwa ambao sikutegemea ungekuwa hivyo. Kwa sasa najiona kama nipo nyumbani China,” anaeleza.

Kwa mfano, anasema siku moja aliamua kwenda eneo la Posta katikati ya jiji la Dar es Salaam. Safari yake ilikuwa kufika Maktaba Kuu ya Taifa iliyopo jirani na Posta. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kwenda katikati ya jiji.

Aliposhuka kituo cha daladala cha Posta, alianza kutafuta ilipo Maktaba Kuu. Dada mmoja alimuona akihangaika, hivyo aliamua kutumia dakika kumi kumpeleka Li hadi Maktaba Kuu.

Dada huyo alifanya hivyo huku akiwaacha baadhi ya ndugu zake kituoni, jambo ambalo siyo watu wengi wanaweza kufanya hivyo. Guaiqiong anasema tukio la pili lilitokea kwenye michezo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anasema yeye ni mpenzi wa michezo. Kuna siku baada ya michezo, marafiki zake waliamua kuacha safari za kwenda kwao na kumsindikiza nyumbani, baada ya kuonesha wasiwasi kuwa akiwa peke yake asingefika.

Anatoa mfano mwingine kuwa wakati anafundisha masomo ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baadhi ya wanafunzi wake walikuwa na tabia ya kumpelekea chakula wanachotoka nacho majumbani kwao, wakimtaka aonje mapishi ya Kitanzania. Li anasema jambo hilo lilimfanya ajione kuwa alikuwa na bahati kubwa kuchagua kuja Tanzania.

“Siwezi kusahau kuna kuna siku nikiwa matembezini nilikutana na mfanyabiashara wa embe. Nilitamani embe na nikachukua moja. Lakini wakati natoa fedha mfukoni ili nimlipe, niligundua nilikuwa nimeisahau pesa nyumbani. Jambo la kushangaza yule muuza embe aliniruhusu kuondoka na embe hilo. Aliniambia nitamlipa siku nyingine nikipita mahali hapo. Huu ni ukarimu wa ajabu,” anaeleza.

Hali kadhalika, anasema kuna rafiki yake anaitwa Sebastian alimualika nyumbani kwao kwa ajili ya kusheherekea pamoja sikukuu ya Krismasi pamoja na familia yake. Guaiqiong anataja tukio lingine ni kuwa rafiki yake mwingine anaitwa Nasra, alimchukua na alisafiri naye hadi kwao mkoani Morogoro na kuishi naye huko kwa siku kadhaa akiwa kama sehemu ya familia hiyo.

“Niliwashirikisha rafiki zangu wa China kuhusu haya mambo. Walisema mimi natendewa mazuri yote haya kwa sababu naishi nao kama marafiki wa kweli na ndiyo maana wao wananitendea hivyo. Hata msimamizi wangu wa masomo UDSM aliniambia kuwa Tanzania unapata kuaminiwa pale unapoonesha uaminifu wako,” anasema mwanadada huyo.

Shughuli zake za ujasiriamali Mbali na masomo anayoendelea nayo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Guaiqiong anajishughulisha na ujasiriamali kupitia mgahawa wake uitwao ‘Breeze’ uliopo eneo la Kinondoni jijini Dar es Salaam. Mgahawa huo umetoa ajira kwa Watanzania 10, anaosaidiana nao kutoa huduma mbalimbali za vinywaji na vyakula vyenye asili ya Kitanzania.

Mgahawa huo hutoa huduma kwa Watanzania wanaofika hapo kupata vyakula mbalimbali na pia hutumiwa na raia wengi wa China, kutokana na eneo hilo kuwa sehemu ya kituo cha utoaji wa huduma zinazohusu taratibu za safari za China na mambo mengineyo.

Anasema janga lililopo sasa la virusi vya corona, limesababisha mgahawa huo kusimamisha shughuli zake wafanyakazi wake kukaa majumbani bila kazi yoyote. Hatua hiyo imemfanya Guaiqiong wakati mwingine kugawana kile kidogo anachokipata kutoka kwa ndugu zake na wafanyakazi wake ili waweze kuendesha maisha yao.

Shabiki wa timu ya Simba Ukiacha masuala mengine, kimichezo Guaiqiong ni mpenzi wa timu maarufu ya Simba na mara kwa mara amekuwa akienda Uwanja wa Taifa, kushuhudia mechi zinazochezwa na timu hiyo ya soka.

Anapokwenda uwanjani, huambatana na marafiki zake. Atoboa siri ya maisha Mwanadada huyo anasema katika maisha, jambo jema ni kutokukata tamaa. Pia, anawataka wasichana wenzake, kupambana usiku na mchana, kwa kufanya kazi zitakazowaingizia kipato chao kwa haki na halali ili waweze kuendesha maisha yao ya kila siku.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/62d23cce3d8ded697092b3b951cd0d39.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi