loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanaoficha sukari wafichuliwe

SUALA la upatikanaji wa sukari nchini limeendelea kuwa ni tatizo huku maeneo mengi wananchi wakitafuta bila mafanikio na wengine wakiipata kwa bei ya bei ya juu sana.

Pamoja na serikali kutoa bei elekezi na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Keneth Benges kusema kuna sukari ya kutosha nchini, kiuhalisia, hali ni tete. Tunasema hivyo kwa kuwa hakuna mkoa ambao haujaathirika. Karibu kila kona ya nchi kilio ni kile kile.

Hata hivyo, bado sababu hazijawekwa wazi, si kutoka Bodi ya Sukari au kiongozi yeyote kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kwamba sukari ipo, lakini kuna njama za baadhi ya wafanyabiashara ambao wanataka kupata faida maradufu.

Ndio maana Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari kwa uhakika anasema sukari ipo tena ya kutosha. Hata hivyo, hata yeye hawezi kujua sababu za kwanini sehemu kubwa ya taifa hili kuna tatizo la sukari.

Kwa sababau, walanguzi hawatumwi na serikali wala Bodi ya Sukari, bali wao kwa ulafi wao hawajali mateso wanayopata Watanzania wenzao, zaidi ya kuangalia matumbo yao.

Ni kutokana na ukweli huo, Benges akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki akawataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabainisha watu wanaoficha bidhaa hiyo kwa sababu za ulanguzi.

Pia Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya naye juzi alisikika akiwaomba wenye viwanda vya sukari kuwaonea huruma wananchi na kutowatesa kwa kutoonekana kwa bidhaa hiyo ambayo ipo ya kutosha. Akasema wazalishaji ni lazima wajue kuwa Watanzania ndio mtaji wao, hivyo wajitahidi sukari ipatikane kwa bei stahili.

Zipo juhudi za baadhi ya viongozi wa ngazi ya wilaya na mikoa ambao wameanza kuchukua hatua. Hawa wametembelea maeneo mbalimbali na kununua sukari bila wauzaji kuwatambua, wakawauzia kwa bei ya juu bila kufuata elekezi iliyotolewa na serikali.

Hawa tayari wamekamatwa. Tuna kila sababu ya kuwakumbusha na viongozi wengine wa ngazi hizo kwa nyadhifa zao kuchukua hatua stahiki maana ni ukweli ulio wazi kwamba sukari ipo ila imefichwa kwa makusudi.

Tunasema hivyo kwa sasabu kwa mujibu wa maelezo ya Benges, changamoto iliyopo ni kwamba wapo wafanyabiashara wameficha sukari kwenye maduka yao na kisha kuiuza kwa watu wanaowafahamu tu ambao wanajua kuwa hata wakiwauzia kwa bei kubwa hawatowafichua.

Benges anasema kati ya tani 40,000 za sukari zilizotakiwa kuingizwa nchini na viwanda vinne vya kuzalisha sukari, zaidi ya tani 30,000 zimeshaingizwa hadi sasa na kuongeza kuwa kiwango cha tani ya sukari kilichoingizwa nchini hadi sasa ni kikubwa ambacho kinaweza kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Serikali ilishatoa vibali kwa viwanda vya sukari vinne ambavyo ni Kilombero Sugar, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na TPC kuagiza tani 10,000 kila kimoja kutoka nje ya nchi kufidia pengo la uzalishaji.

Tunaamini, wananchi kwa kushirikiana na vyombo vya dola, wakitoa taarifa, zitawezesha walanguzi hawa kukamatwa ili sheria ichukue mkondo wake.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi