loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Chakula cha kutosha muhimu kukabili corona

KATIKA kukabiliana na athari zitokanazo na ugonjwa wa Covid-19, Wizara ya Kilimo imekuja na mikakati kadhaa ikiwamo kununua tani 735,000 za nafaka kwa ajili ya dharura, zitakazotosheleza nchi kwa miezi mitatu.

Hayo yameleezwa bungeni na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati wa kuwasilisha hotuba ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Waziri Hasunga amesema kutokana na kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa huo, wizara hiyo inatarajia kutumia nyongeza ya Sh bilioni 217.5 kununua tani 435,000 kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Amesema Wizara ya Kilimo imefanya tathmini na kubaini kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2019/2020, haujaathirika kwa kuwa pembejeo zimeshawasili nchini.

Amesema mazao ya asili ya biashara ambayo ni pamba, korosho na kahawa, misimu yake ya mauzo imeishia Machi 2020 na hivyo kutoathirika na ugonjwa huo huku kwa zao la tumbaku wakulima wameshafunga mikataba na wanunuzi kwa ajili ya msimu 2020/2021.

Hasunga amesema mazao ambayo yameonesha dalili za kuathirika ni chai na mazao ya bustani, ambayo masoko na usafirishaji wake nje ya nchi umeathirika.

Amesema pia kama ugonjwa huo utaendelea kwa muda mrefu, unaweza ukaathiri soko la pamba ambalo msimu wake wa mauzo unaanza Mei na upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa msimu wa 2020/2021 hususan mbolea na viuatilifu, ambavyo vinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Amesema pia kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, uzalishaji wa chakula umeendelea kuimarika na kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 121 na kuwa na wastani wa ziada ya tani 2,798,700.60.

Kwa dhati tunapenda kupongeza hatua hizi za serikali kupitia Wizara ya Kilimo, kuhakikisha kuwa wakati taifa linapambana na janga la corona, kunakuwa na akiba ya kutosha ya chakula.

Ni jambo la kujivunia kuona kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, imewezesha mazingira mazuri ya kilimo, hatua ambayo imefanya kuwepo kwa akiba ya kutosha ya mazao lakini pia imewezesha kuimarika kwa bei za mazao za ndani.

Ni kweli kuwa upo uwezekano wa ugonjwa wa corona kuendelea kuwepo, lakini matumaini yetu ni kwamba ununuzi wa tani hizo za chakula, utasaidia kutuvusha hadi katika kipindi ambacho tayari mazao mapya yatakuwa yamekomaa na kuingia katika hazina ya akiba ya taifa ya chakula.

KUMEKUWAPO na habari za kufurahisha kuhusu mashirika zaidi ya ndege ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi