loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

RC- Toeni ushirikiano magari yasikwame mpakani

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella amesema baada ya kufanya uchunguzi amebaini kuwa mpaka wa Lungalunga kwa upande wa Kenya haujafungwa ila wameongeza taratibu za kuvuka mpaka huo, hivyo amewataka maofisa wa Kituo cha Horohoro kutoa ushirikiano na kwa upande wa Lungalunga ili kulimaliza tatizo vizuri la kukwama kwa muda mrefu kwa magari ya mizigo yanayokwenda Mombasa, Kenya kutokea nchini.

Uchunguzi alioufanya Shigella umetokana na zaidi ya magari 10 ya abiria na magari 40 ya mizigo yaliyokuwa yakisafiri kwenda Mombasa nchini Kenya, kuzuiwa katika mpaka wa Lungalunga upande wa Kenya hadi abiria na madereva wapimwe virusi vya corona na kusubiri majibu kwa muda wa siku tatu.

Uamuzi huo umetokea usiku wa Jumatatu hadi Jumanne ambako hatua imesababisha baadhi ya Watanzania hao kugomea vipimo vya corona vya Kenya hadi kuwepo madaktari Watanzania.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya abiria waliokuwa wakienda Mombasa waligoma kupima na kuamua kurudi Tanga.

Pia, madereva hao wameshangazwa na hatua ya watu kutoka Kenya kupita katika mpaka wao kuingia mpaka wa Horohoro nchini Tanzania bila kuzuiwa.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Shigella alifanya ziara mpakani hapo kujionea hali halisi.

“Nawaomba maofisa wa Horohoro kutoa ushirikiano na wenzetu wa Kenya bila kuathiri taratibu za mipaka za Tanzania na Kenya ili kuondoa hii changamoto pamoja na kuweka tahadhari za kujikinga,”alisema.

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya madereva hao wamelalamika kuwa malori mengi yamebeba mizigo ya kuoza hivyo ni hasara kwao.

Wamesema kuwa tukio hilo la kushtukiza kwa upande wao limewaathiri kutokana na walipita katika mpaka wa Horohoro upande wa Tanzania wakiwa salama lakini cha kushangaza kwa upande wa Kenya wamezuiwa hadi wapimwe maambukizi ya virusi vya corona na wasubiri siku tatu.

Shauri Mwariko(34) kondakta wa basi dogo la Muni linalofanya safari zake kati ya Tanga na Mombasa alisema kuwa hali hiyo imewaathiri kutokana wengi wao wamebeba mizigo ya kuoza na wengi kutokana na tukio hilo wamegoma kupima virusi vya corona wameamua kurudi Tanga.

Faridi Abdallah ambaye anafanya safari ya kusafirisha mizigo ameomba viongozi wa Serikali ya Kenya na Tanzania wakae pamoja ili waweze kujadili suala hilo. Ofisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha Pamoja cha Mpaka wa Horohoro (OSBP), Singwa Mokiwa alisema kuwa wao kwa upande wa Tanzania hawakuwazuia madereva kupita kwenye mpaka wa Horohoro ila changamoto imetokea upande wa Lungalunga.

“Kwa upande wa Tanzania hakuna shida,wamevuka salama na sisi hatukujua kwa upande wa wenzetu na hii imewaongezea gharama za kuishi,”alisema.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jonathan Budeme alisema kutokana na hali hiyo inabidi kufanyike utaratibu wa kuwapima virusi vya corona kwa upande wa Horohoro na kuwapa cheti maalumu kabla ya kuvuka ili kuondoa usumbufu.

SHIRIKA  la Madini Nchini (Stamico) litaanza ...

foto
Mwandishi: Cheji Bakari, Horohoro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi