loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tusisahau mapema corona ipo

NI takriban miezi miwili sasa imepita tangu Serikali ichukue hatua za awali za kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona kwa kufunga shule, vyuo na kuzuia mikusanyiko na misongamano.

Hatua hizo ziliambatana na kutao maelekezo ya kiafya kwa wananchi ya kuvaa barakoa, kuosha mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kutumia vitakasa mikono .

Aidha mamlaka zilienda mbele zaidi na kuagiza vyombo vya usafirishaji kuzinghatia matakwa ya kukabiliana na corona kwa kuhakikisha kwamba magari yanabeba idadi inayotakiwa ili kupunguza misongamano ndani ya mabasi.

Pamoja na maelezo yote hayo ya kiafya ambayo yaliitikiwa kwa nguvu kubwa sasa hivi inaonekana watu wanaacha taratibu kama vile ugonjwa huo umepungua au umetoweka kabisa.

Maelezo ya wataalamu na hata rais wetu Dk John Magufuli yanaonesha wazi kwamba ugonjwa huu utaendelea kuwapo kwa kipindi kirefu hivyo ni vyema watanzania wakachukua tahadhari zote huku wakiendelea kuchapa kazi.

Kutokana na ukweli huo tunapenda kuwakumbusha Watanzania kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya na wasifanye mchezo na ugonjwa huo pamoja na kwamba tunamuomba Mungu anyooshe mkono wake na kuuondoa.

Haitakuwa na maana kama serikali inapambana kuhakikisha kwamba zana zote za kujikinga zinapatikana kwa bei nafuu, watanzania wameshaanza kwenda tofauti kwa kuacha kuvaa barakoa hata kwenye msongamano na kwenye daladala na wasafirishaji nao kuanza kuwaongeza watu katika magari yao huku wananchi wenyewe nao wakiwafanya makondakta kuona kumbe inawezekana kuwatia watu wengi zaidi katika gari na maisha yakaendelea.

Tunapenda kukumbusha mamlaka husika kuwa huenda bila kubanwa wananchi hawa hawatajali afya zao hata chembe na wataendelea kuilalamikia serikali mambo yatakapokuwa magumu zaidi bila kuangalia wao wanajisaidia vipi.

Ni kweli hatuhitaji kuwa na hofu katika hili, lakini upo ukweli mkubwa zaidi, ukweli kuwa tusipofuata tahadhari tunazopewa na wataalamu pamoja na viongozi wetu jinsi ya kujihadhari na ugonjwa huu safari yetu ya kupambana nao itakuwa ngumu na yenye majeruhi wengi.

Shime watanzania tuhakikishe tuna kuwa askari katika maeneo yetu, tuzuie sisi wenyewe kabla ya vyombo vya dola mabasi kujaza kupita kiasi na inapotokea hilo tuzipe taarifa mamlaka ili madereva na makondakta wachukuliwe hatua kali kwani katika hili wao pia wanahatarisha maisha yao.

Pia inafaa kuanza kuweka sheria ndogo kwamba mtu asiyevaa barakoa asiingie katika usafiri wa umma na pia katika maeneo ya huduma ya umma, tunapokuwa wakali wenyewe hakika tutafika tukiwa salama zaidi na sio kufika tukiwa hoi.

Tunapoomba mkono wa Mungu wa uponyaji katika dua na sala zetu kila siku, pia tusikilize mamlaka ambazo zinatupa mwongozo wa namna ya kupigana vyema vita hii ambayo tumeshaishinda.

Tutambue kwamba corona ipo na inaua na ni wakati wetu sasa kuacha kufikiri kwamba haipo na hatuna sababu za kuchukua hatua za tahadhari, tufuate maelekezo ya wataalamu ambao ndio majemedari wetu ili tufike mwisho wa vita hii tukiwa na shangwe nyingi zaidi kuliko huzuni.

KUMEKUWAPO na habari za kufurahisha kuhusu mashirika zaidi ya ndege ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi