loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tusiwasahau wenye ulemavu kwenye vita ya corona

MAPAMBANO dhidi ya virusi vya corona yanaendelea nchini na duniani kote ambako wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari dhidi ya kusambaa virusi hivyo vinavyosababisha homa ya mapafu (COVID -19).

Wakati kila nchi ikipambana na hali yake dhidi ya corona, jamii, mamlaka za serikali na wadau kwa pamoja tunajukumu la kuhakikisha watu wenye ulemavu katika jamii zetu nao wanapata elimu hiyo sawasawa na kuchukua hatua.

Nasema hayo kwa sababu, imezoeleka katika majanga au mambo mengi yanayoendelea, kundi hilo likaachwa nyuma. Kwenye mapambano haya ni vyema wahitaji kama hawa wakapewa kipaumbele cha kwanza ikiwemo elimu, na misaada ya vifaa vya kujikinga ili nao wachukue tahadhari.

Tunaelewa kwamba kwenye kundi hilo wapo wa aina tofauti, wapo wenye ulemavu wa kusikia, wasioona, na wengine kama hao, ambao wanapaswa kusaidiwa kwa karibu ili nao wachukue tahadhari. Kundi hilo liko kwenye hatari zaidi kwani mara nyingi huitaji kugusa kitu ndipo wafahamu kama wanapotembea au kupita ni eneo salama.

Wakati huo huo tunaambiwa kuwa tuepuke kushika vitu au kugusana na watu kama njia mojawapo ya kujikinga na corona. Sasa kwa ndugu zetu hawa, kwao ni changamoto, sio wote wenye vifaa vya kuwasaidia kutembea kama fimbo zao maalum kwa wale wasioona hivyo wakati mwingine huitaji msaada wa mtu kumvusha au kumuongoza kwa kumshika.

Sasa basi tuwasaidia vifaa na elimu pia wapate ili iwe rahisi kwao kuchukua tahadhari wakati huu na kujiepusha na uwezekano wa kuambukizwa au kuambukiza wengine corona.

Tumeona siku chache zilizopita, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), wakitoa msaada wao vifaa kinga kwa Chama cha Wasioona Tanzania ili kuwawezesha kujikinga na corona. Vifaa hivyo ni pamoja na barakoa,vitakasa mikono, ndoo za kunawia mikono na sabuni viaa ambavyo vitasaidia wenzetu hao kujikinga dhidi ya corona.

Tunajua Tanzania ni kubwa, vifaa hivyo haviwezi kuwafikia wote, hivyo basi nitoe rai kwa wadau wengine hata jamii na vikundi mbalimbali kuendelea kuguswa kusaidia makundi muhimu ya kipaumbele kama hayo katika jamii ili vita ya corona ifanikiwe. Hatuwezi kupigana vita hii ili hali tumewaacha nbaadhi ya wenzetu wenye uhitaji nyuma ambao wanahitaji sisi tuwasaidie kwenye vita hivi.

Tukumbuke kwamba hatuwezi kuwa salama wakati baadhi yetu wako shakani na wanaoweza kuwanusuru ni sisi kwasababu hao ni ndugu zetu na vita hii ni lazima tupambane pamoja bila kujali maumbile yetu .

Kama OSHA wamefanya jambo juu yao, hata sisi tunaweza kufanya kitu kwa ndugu zetu, tuchukue hatua kwa sababu ulemavu unaweza kumpata yeyote kati yetu kwa wakati wowote bila kuchagua hali yake.

KAMPENI za uchaguzi kwa ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi