loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rais Rajoelina: Dawa inaponya Covid-19 wiki baada ya kuinywa

HIVI karibuni, kituo cha redio (Radio France Internationale- RFI) pamoja na Televisheni ya serikali ya Ufaransa (France 24) kilifanya mahojiano na Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina.

Ni mahojiano ya kwanza kushiriki tangu atangaze ugunduzi wa dawa ya Covid-Organics inayotibu homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Yafuatayo ni mahojiano hayo yaliyoongozwa na waandishi Christophe Boisbouvier na Marc Perelman yaliyotafsiriwa na gazeti hili: Christophe Boisbouvier: Habari za asubuhi Ndugu Rais. Rais Rajoelina: Nzuri, nina furaha ya kuwa mgeni wenu, hususani katika kipindi hiki cha vita dhidi ya corona.

Marc Perelman: Tutazungumzia kuhusu suala hili ambalo umeliita ‘vita’ dhidi ya Covid-19. Zaidi ya kufungiwa ndani, uvaaji wa barakoa, kutokaribiana, Madagascar imekuwa maarufu kwa kutumia Covid- Organics, dawa mbadala iliyotokana na mmea wa artemisia, unaojulikana kwa kutibu malaria.

Umeshapeleka dawa hii kwa nchi mbalimbali za Afrika lakini una uthibitisho kwamba inafanya kazi hapa nyumbani, kwamba inatibu wagonjwa wa Covid-19? Rais Rajoelina: Kimsingi, kweli tumezindua dawa ya asili inayotokana na mmea unaotibu.

Itakumbukwa kwamba katika Madagascar tumezoea kuitumia na asilimia 80 ya idadi ya watu inajitibu kwa kutumia tiba asilia. Kama nilivyosema, Covid-Organics ni tiba na kinga dhidi ya Covid-19 ambayo inafanya vizuri.

Licha ya hivyo, ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Utafiti cha Malagasy (IMRA) chenye hadhi ya kituo cha utafiti kinachotambulika na Umoja wa Afrika.

Nataka nioneshe kwamba IMRA ni kituo cha tiba na dawa kilichoanzishwa mwaka 1957 na Profesa Rakoto Ratsimamanga, ambaye ni bingwa katika sayansi ya Afrika. Umezungumzia ‘uthibitisho’ na mimi awali nilisema ‘vita’.

Hali ya dunia leo inaonesha kuna watu takribani 300,000 waliofariki. Je ni sawa kudharau tiba mbadala? Na tunapokuwa kwenye vita, ni uthibitisho gani tunaweza kuonyesha na kuutoa katika wakati huu? Kimsingi, kupona kwa watu wetu wanaoumwa, kwa sababu izingatiwe kwamba leo, katika Madagascar, tuna wagonjwa 171 ambao kati yao 105 wamepona.

Kama uthibitisho, nataka kuwaambia kwamba wagonjwa waliopona walitumia hii Covid-Organics (pia tunaiita Tambavy CVO). Kwa ufupi, afya za wagonjwa waliotumia Tambavy CVO ilianza kuboreka ndani ya saa 24 baada ya kunywa dawa hiyo kwa mara ya kwanza. Kupona kabisa kwa wagonjwa hao kulionekana baada ya siku saba au hata siku 10 baada ya kunywa Tambavy CVO.

Hii dawa ni ya asili, isiyo na sumu. Christophe Boisbouvier: Siyo kila mtu anashawishika na uthibitisho unaozungumzia. Na siyo kila mmoja.

Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na zaidi ya hao, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), ofisi ya WHO katika Afrika, imehadharisha hivi karibuni dhidi ya tiba hiyo ya kusadikika.

Siyo tu kwamba WHO inahofia ufanisi wa Covid-Ogranics, lakini inahofia athari kwa watu watakaokunywa dawa hiyo? Rais Rajoelina: Kimsingi unanukuu onyo la Dk (Matshidiso) Moeti dhidi ya matumizi ya Covid-Organics.

Nataka niulize swali: Je, Mediator (dawa ya kutibu kisukari inahusika kwa vifo vya watu nchini Ufaransa) iliidhinishwa? Na swali langu leo ni: watu wangapi walikufa kutokana na dawa ya Mediator?

Unajua kama ilivyo kwa kila mtu kauli ya Profesa Bernard Debre na Philippe Even, waliwasilisha takribani dawa 58 zilizotengenezwa katika maabara kubwa ambazo siyo tu hazitibu bali kwa maneno yao, ni hatari. Dawa hizi zimekuwa na zinasambazwa Afrika na sijawahi kusikia Dk Moeti au WHO wakiotoa tamko la kutoidhinisha matumizi ya dawa hizo.

Sasa, kama nilivyosema awali, tunatumia njia za kuchemsha mmea wa dawa kwenye maji kukamua kile kinachohitajika. Ni dawa yetu ya asili inayofahamika na inatambulika kwa matokeo yake.

Kuna mengi ya kuzungumza kwa dawa hii ya artemisia. Umeniuliza swali lakini bado nina swali la kukuuliza: Isingelikuwa Madagascar, lakini ikawa nchi ya Ulaya ambayo ndiyo imegundua dawa, kungekuwapo na wasiwasi mwingi? Sidhani.

Ninachoweza kusema leo ni kwamba kwa suala la wagonjwa waliopo Madagascar na pia wale waliochukua hizi dawa, kwa kweli Tambavy CVO, tuna uthibitisho kwamba tumewatibu wagonjwa wetu.

Marc Perelman: Kwa kweli, tutachukua mfano wa Ufaransa. Shirika la Taifa la Usalama wa Dawa hivi karibuni limechapisha onyo kuhusu kununua bidhaa zilizotokana na Artemisia likisema kwamba vitu vya kimatibabu vilivyomo ni vya uongo na hatari.

Je, unahisi kwamba wasiwasi huo au shutuma zinatoka Magharibi au pengine hata kutoka kwenye ushawishi wa dawa za kimagharibi? Rais Rajoelina: Yawezekana ulimwona au kumfuatilia Profesa Montagnier aliyetoa tamko kwamba artemisia inatibu virusi vya corona na bado amepokea Tuzo la Nobel ya Sayansi na Tiba.

Hili ni jambo moja. Lakini pia unaweza ukawa unafahamu kwamba utafiti wa Profesa Tu Youyou wa China aliyechuja artemisinin kutoka kwenye artemisia. Kwa hiyo, leo sielewi kwa nini yawepo maswali mengi, kwa nini matatizo makubwa? Lakini tatizo kubwa leo la Covid-Organics siyo kanuni yake.

Siyo uelewa wa kitabibu ambao tunajifanya hatuujui. Watu wanasema mambo mabaya kuhusu dawa hii wakati inafanya kazi nzuri ya kuokoa maisha sasa hivi. Katika vita hii, wanataka kutupunguza kasi.

Wanataka kutukatisha tamaa au hata kutufanya tusisonge mbele. Marc Perelman: Hao ni akina nani? Rais Rajoelina: Lakini hakuna kitakachotuzuia kusonga mbele, iwe ni nchi au shirika. ‘Hao’, umezungumzia mashirika machache awali kama vile Shirika la Afya Duniani.

‘Sisi’ ndiyo Madagascar. Sisi ni nchi huru na tupo hapa kusaidia watu wetu, idadi ya watu wetu, ili tusiwe waathirika wa kweli au kufa kutokana na janga hili. Christophe Boisbouvier: Kwa kweli, kile ambacho kila mtu anakuuliza ni majaribio ya kitabibu.

Ulitaja Taasisi ya Utafiti ya Malagasy (IMRA), lakini kwa sasa, taasisi hii imefanya uchunguzi wa kitabibu tu na siyo majaribio ya kitabibu. Kwa hivyo ni lini utafanya vyote na nani atafanya? Rais Rajoelina: Kwa hiyo, isije mtu akachanganya majaribio na uchunguzi. Kwa sasa, tunapozungumzia Tambavy CVO, tuna dawa ya asili iliyoboreshwa.

Tunapozungumzia dawa iliyoboreshwa, mfumo wa uthibitisho ni tofauti na ile ya dawa. Hatufanyi majaribio ya kitabibu bali uchunguzi wa kitabibu, kulingana na mwongozo uliotolewa na WHO. Na ndiyo tulichofanya.

Tumefanya uchunguzi wa kitabibu. Itifaki ya uchunguzi inapaswa kuzingatiwa na tuliangalia na kufanya uchunguzi wa kitabibu juu ya athari na hali ya afya ya wagonjwa wa Covid-19.

Kwa hivyo leo, tumezingatia viwango vya maadili vinavyotambuliwa kwa uchunguzi na utafiti wa kitabibu. Christophe Boisbouvier: Lakini Alhamisi iliyopita ulitangaza kwamba majaribio ya kitabibu yataendeshwa hivi karibuni. Kwa hiyo hayatafanyika? Rais Rajoelina: Kuna vitu viwili. Hakuna kuchanganya. Kuna itifaki nyingi ambazo tumezizingatia.

Kwanza kabisa, kama ilivyo kwa kila nchi duniani, tunakabiliwa na janga. Tunatakiwa kutafuta suluhisho kwa kutibu wagonjwa. Na pale Profesa (Didier) Raoult alipotangaza ufanisi wa klorokwini na azithromycin, tulizitumia na napenda kumshukuru kwa sababu bila pendekezo hilo la suluhisho, tusingeweza kuwahudumia wagonjwa wa kwanza wa virusi vya corona. Isitoshe, sote tunafahamu dozi kubwa ya klorokwini ina athari.

Tiba hii ni hatari na inahitaji uchunguzi mkubwa wa kitabibu. Itifaki nyingine tuliyozingatia kwa Tambavy CVO ni misingi ya uchunguzi na utafiti wa kitabibu kulingana na mapendekezo ya WHO. Idadi kubwa ya wagonjwa wapya waliokunywa dawa walifuatiliwa na matokeo yapo. Kwa sasa hakuna vifo katika Madagascar.

Tumewatibu wagonjwa wetu. Lakini ulizungumzia awali kuhusu majaribio ya kitabibu. Kwa vyovyote, tuna itifaki ya kitabibu kuhusu dawa katika mfumo wa sindano, tofauti na dawa ambayo tumeipendekeza hivi karibuni. Hii ni sehemu ya mtangamano wa kikanda na ushirikiano wa madaktari na wanasayansi wa Marekani na pia katika Bahari ya Hindi.

Marc Perelman: Taasisi ya Utafiti ya Malagasy imekataa kuweka wazi mchanganyiko halisi wa Covid-Organics kwa sababu tunafikiri kwamba hii taasisi haitaki kuwahiwa na washindani kabla ya kuwa na haki miliki. Lakini watu wengi wa vijijini nchini hapa hawawezi kufikia dawa hii.

Hivyo wanaweza kutengeneza dawa wenyewe na hivyo kujilinda, unaweza kutuambia kilichoongezwa kwa Artemisia; mimea mingine miwili iliyotengeneza Covid-Organics? Rais Rajoelina: Kimsingi, Covid-Organics imejikita kwenye mimea ya kitabibu.

Nyingi ni artemisia ambayo ni hadi asilimia 62 lakini pia na mimea ya dawa ya Malagasy. Haiwezekani kufichua leo. Hii ndiyo matokeo ambayo tunatarajia leo na zaidi ya hayo, kweli tutazindua uchunguzi wa kitabibu katika ngazi ya kikanda kwa sasa.

Kama unataka, tunayo kanuni yetu. Na kama nilivyokuambia awali, tunafanya kazi na Taasisi ya Utafiti Malagasy. Ningependa kukuonesha zao la Madecassol iliyozalishwa leo na Bayer inafanya ziwepo dawa zipatazo 100. Na hii ni matokeo ya utafiti wa IMRA. Na ni dawa iliyotengenezwa mwaka 1961. Hii inakufahamisha kwamba, hatupaswi kubeza wanasayansi wa Afrika na Madagascar.

Tupo hapa na ni kweli leo kuna maswali yanayojitokeza: kwa nini, kuna tatizo gani la Covid- Organics? Nafikiri tatizo ni kwamba inatoka Afrika. Na hatuwezi kukubali, kupokea kwamba nchi kama Madagascar, ambayo ni nchi ya 63 kwa umasikini duniani, imeweza kutengenza kanuni na kupata Tambavy CVO kuokoa dunia.

Lakini hii ni vita. Si vita ya kijeshi au nguvu ya kiuchumi ambayo imekuwa ikifanyika. Lakini Mungu na Bwana ametupa mimea ya dawa kusaidia nchi nyingine na dunia nzima kupambana na maradhi.

Christophe Boisbouvier: Unaomba Ufaransa irudishe visiwa vile vinne vilivyo mbali na pwani yako. Tume ya pamoja iliundwa mwaka mmoja uliopita. Lakini Oktoba 2019, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alikwenda kwenye moja ya visiwa hivi na kusema: “Hii ni Ufaransa”.

Je, suluhisho litaweza kupatikana kati ya nchi mbili kati ya sasa na Juni 26 wakati nchi yako ikiadhimisha miaka 60 ya uhuru? Rais Rajoelina: Matamanio yetu kwa kweli ni kupata suluhisho kwa kurudisha visiwa hivi kwa Madagascar. Mkutano wa pili wa tume ya pamoja ulikuwa umepangwa mwishoni mwa Machi. Lakini uliahirishwa kwa sababu ya maambukizi ya cororna.

Lakini nina imani na uhakika katika uwezo wetu tutafukia suluhisho la haraka na kukidhi maombi yetu ya kurudishiwa. Christophe Boisbouvier: Urejeshaji au makubaliano ya ushirikiano na Ufaransa kuongoza? Rais Rajoelina: Tunataka uhuru wa hivi visiwa. Na tunazungumzia kuhusu urejeshaji.

Makala haya yamepatikana kwenye tovuti ya ubalozi wa Madagascar nchini Ujerumani (https://www. botschaft-madagaskar.de/) na kutafsiriwa na mwandishi wa gazeti hili, STELLA NYEMENOHI.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi