loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Amani itawale uchaguzi Burundi

KESHO wananchi wa Burundi, mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanafanya uchaguzi wao mkuu wa viongozi watakaoongoza taifa hilo kwa miaka mitano.

Uchaguzi huo wa wabunge, madiwani na urais, umekuwa na nguvu kwani atapatikana Rais mpya baada ya Rais Pierre Nkurunzinza kuacha kugombea tena baada ya kuongoza miaka 15.

Nkurunzinza alishika madaraka kuanzia mwaka 2005 alipochaguliwa na Bunge kutokana na vurugu zilizokumba nchi hiyo na kisha kuchaguliwa na wananchi mwaka 2010.

Hata hivyo, alipogombea muhula wa tatu mwaka 2015, alipingwa na baadhi ya wanasiasa na kusababisha ghasia na jaribio la mapinduzi ya serikali hiyo bila mafanikio hadi hivi sasa.

Uchaguzi huu unaelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni mwanzo mzuri wa amani Burundi hivyo kusaidia wananchi wake wanaoishi uhamishoni katika nchi mbalimbali kurejea nchini mwao na kujenga nchi, kwani wagombea wote wamekubalika katika jamii.

Katika uchaguzi huo, katika nafasi ya urais, wagombea saba watapigiwa kura ambapo Jenerali Evariste Ndayishimiye amnayetaka kumrithi Rais Nkurunziza, atapeperusha bendera ya chama tawala cha CNDDFDD.

Mgombea huyo wa chama tawala anakabiliwa na upinzani mkubwa wa Agathon Rwasa, mpinzani mkuu anayepeperusha bendera ya chama cha CNL ambacho kilisajiliwa mwaka mmoja uliopita kuma chama cha siasa.

Mgombea mwingine ni Domitien Ndayizeye, rais wa mpito kati ya mwaka 2003 na mwaka 2005, ambaye atapeperusha bendera ya muungano wa vyama vya Kira Burundi. Wengine ni Gaston Sindimwo wa Chama cha Uprona, Léonce Ngendakumana wa chama cha Sahwanya Frodebu na wagombea binafsi, Francis Rohero na Dieudonné Nahimana.

Wagombea hao na wengine wa ubunge na udiwani katika wiki tatu wamefanya kampeni na kueleza nia ya kuwaongoza wananchi wao.

Wamepewa nafasi ya kampeni licha ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa corona ambapo wananchi wamefuatilia kampeni zao jukwaani iwe katika vyombo vya habari au mikutanoni.

Kutokana na ahadi zao kwa wananchi, ni vema wananchi wakachagua viongozi stahiki kwa maendeleo ya nchi huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikihakikisha uchaguzi ni huru na haki.

Kutokana na migogoro na mapigano mengi nchini humo kutokea baada ya uchaguzi ni vema tume hiyo kuangalia changamoto au malalamiko yanayotolewa na wananchi.

Pia isikilize malalamiko ya wagombea wa vyama vya siasa na wengineo na kutolea ufafanuzi kuzuia kutokuaminiana kwao.

Lakini pia ni vema wananchi na vyama vya siasa Burundi kujenga tabia ya kuamini tume yao ya uchaguzi na kukubaliana na matokeo rasmi yatakayotangazwa na kisha kuendelea na shughuli za maendeleo baada ya uchaguzi na kuacha waliochaguliwa wakitimiza wajibu.

Malalamiko na vurugu baada ya uchaguzi yanasababisha kupoteza muda wa maendeleo na kuishia vurugu na watu kuishia kukamatwa na polisi na wengine kupoteza maisha hivyo ni vema wananchi wa Burundi uchaguzi huu kuwa tofauti kwa kumalizika washindi wakitangazwa.

KAMPENI za uchaguzi kwa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi