loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sheria huduma ndogo za fedha suluhu riba kubwa

WANANCHI wengi, hususani wa kipato cha chini, wamekuwa wakihitaji fedha ili kuzitumia kama mitaji kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali.

Lakini kundi hili limekuwa likiathirika na huduma zitolewazo na taasisi za huduma ndogo za kifedha kutokana na riba kubwa za mikopo zitolewazo na taasisi hizo.

Wamekuwa pia wakiibiwa kwa njia za mitandao mbalimbali huku wakisumbuliwa na utaratibu mbovu wa ukusanyaji wa madeni ambao umekuwa ukisababisha wananchi kupoteza mali zao.

Katika kumkomboa mwananchi na changamoto za huduma ndogo za fedha, Serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na kanuni mahsusi za biashara ya huduma ndogo za fedha za mwaka 2019 kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa sheria husika.

Lengo ni kuhamasisha ukuaji na uendelezaji wa sekta hiyo. Sheria na kanuni zilitangazwa kuanza kufanya kazi Novemba 1, mwaka jana 2019.

Benki Kuu ya Tanzania imepewa jukumu la kusimamia taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha nchini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kama Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na serikali za mitaa.

Ili kufanikisha jukumu hili kwa ufanisi zaidi, Benki Kuu ilikasimisha mamlaka na majukumu yake kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kupitia Tangazola Serikali (GN.887). Tume ambayo kwa mujibu wa sheria ya vyama vya ushirika namba 6 ya mwaka 2013 inasimamia vyama vya ushirika ikiwemo vyama vya akiba na mikopo (Saccos).

Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Usimamizi na Udhibiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Collins Nyakunga, akizungumza wakati wa mafunzo ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha kwa viongozi na watendaji wa vyama vya akiba na mikopo (Saccos) jijini Dar es Salaam hivi karibuni, alitoa wito kwa vyama kuwa na uelewa wa Sheria ya Vyama vya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013.

Pia alivitaja kuwa na uelewa kuhusu Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha namba 10 ya mwaka 2018, miongozo na kanuni husika za ushirika.

“Viongozi na watendaji ni lazima kuzijua na kuzifuata sheria, kanuni na taratibu za ushirika ili kuhakikisha kuwa mnatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na usahihi bila kukinzana na taratibu za kisheria. Kwa kufanya hivyo, mtavisaidia vyama kuwa endelevu, kujenga na kuongeza imani kwa wanachama wenu,” anasema Nyakunga.

Wakati wa mafunzo hayo Mrajis Msaidizi anayeshughulikia usimamizi wa vyama vya ushirika wa vyama vya kifedha wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Josephat Kisamalala anasema watoa huduma ndogo za kifedha wamegawanyika katika madaraja manne; daraja la kwanza ni taasisi zinazopokea amana, daraja la pili ni taasisi zisizopokea amana, wakopeshaji binafsi pamoja na watoa huduma kwa njia ya mtandao.

Daraja la tatu anasema ni Saccos na daraja la nne ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kama vile benki za Maendeleo vijijini (Vicoba).

Akieleza masharti ya kanuni zahuduma ndogo za fedha daraja la tatu hususani Saccos, Kisamalala anafafanua kuwa kwa sasa vyama hivyo vitakuwa vikifanya kazi kwa kuzingatia masharti maalumu yanayozingatia kulinda maslahi ya wanaushirika.

“Kutakuwa na makundi mawili ya leseni; Saccos zenye leseni daraja A na daraja B, kiwango cha chini cha mtaji kwa Saccos zenye leseni daraja A ni Sh milioni 10 na leseni daraja B ni Sh milioni 200. Saccos haitaruhusiwa kutoa huduma ndogo za fedha pasipo kuwa na leseni ya utoaji wa huduma hizo kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma ndogo za fedha.” anasema.

Kwa mujibu wa Kisamalala, Iwapo Saccos itashindwa kufikia kiwango cha chini cha mtaji, Saccos hiyo itapaswa kuwasilisha mpango wa kuongeza mtaji ndani ya siku 60 tangu ishindwe kufikia mtaji huo kwa msimamizi,” anasema.

Shughuli za Saccos daraja A Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ndogo za Fedha, shughuli zinazoruhusiwa kufanyika katika Saccos daraja A ni pamoja na kupokea hisa za uanachama za hiari, kupokea akiba na kutoa mikopo kwa wanachama, kufanya uwekezaji, kufanya shughuli nyingine zitakazoidhinishwa na Benki Kuu au mamlaka kasimishwa.

Shughuli za Saccos daraja B Shughuli zinazoruhusiwa kufanywa na Saccos zenye leseni daraja B ni pamoja na shughuli zote zilizoruhusiwa kwa Saccos zenye leseni daraja A.

Hata hivyo, shughuli zaingine za daraja hili ni kupokea amana kutoka kwa wanachama wake, kutoa mikopo shirikishi, kutoa mikopo ya karadha, huduma za uwakala wa bima ndogo, uwakala wa benki, uwekezaji wa mitaji, kutoa kadi za malipo (debit card), kufungua matawi na milango ya huduma na shughuli nyingine zitakazoidhinishwa na Benki Kuu au Mamlaka Kasimishwa.

Yasiyoruhusiwa kufanywa na Saccos Wanaushirika wanatakiwa kuzingatia kanuni na masharti yaliyowekwa ili kuendana na matakwa ya sheria na taratibu za huduma ndogo za fedha. Saccos hazitakiwi kuendesha akaunti ya hundi kwa wanachama, kupokea amana kwa wasio wanachama, kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni.

Vilevile, Saccos hazitakiwi kufanya shughuli za biashara za nje, shughuli za udhamini, kutoa Credit Cards, kuhamisha fedha na kutoa oda za malipo.

Utoaji Leseni Katika kuboresha utendaji, Saccos zote zinahitajika kuwa na leseni kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ndogo za Fedha. Utaratibu unaelekeza leseni zote zitatolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Makao Makuu ya Tume ambapo, Warajis wasaidizi wa mikoa na maafisa ushirika wa wilaya watasaidia kutoa maelekezo na kufanya tathmini ya maombi ya leseni zilizoombwa na Saccos.

Maombi yote ya leseni yataombwa kwa njia ya mtandao (Saccos License online Application System).

“Leseni zitatolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini mara baada ya kufanyika kwa tathmini ya maombi hayo kwa kina. Ofisi za mikoa na wilaya zitahakikisha zinatoa maelekezo kwenye vyama na kuhakikisha Saccos zote zilizopo katika maeneo yao zinatekeleza matakwa ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha,” anasema Kisamalala.

Anasema mfumo wa utoaji leseni unaenda kuongeza ufanisi kwa kusaidia upatikanaji wa ripoti za vyama vilivyoomba leseni, zilizopata leseni, kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanaushirika popote walipo kupitia mifumo ya Tehama.

Hivyo anawataka wanaushirika kupata huduma kwa haraka bila kulazimika kusafiri kutoka eneo lake. Kwa upande wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, mfumo huu utasaidia kuboresha taarifa za waombaji leseni wakati wowote zinapohitajika kutokana na kanzidata zenye taarifa sahihi.

Aidha, Kisamalala anasema ili kuimarisha na kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa vyama vya akiba na mikopo nchini hususan katika kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, Tume tayari imeshafanya mafunzo kwa viongozi na watendaji kwa Saccos 755 zikiwa na viongozi na watendaji 1,350 na maofisa 119.

Mafunzo hayo yamefanyika katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Mbeya, Singida, Korogwe, Songwe, Shinyanga, Ruvuma, Kilimanjaro, Dar es salaam, Pwani, Iringa na Arusha.

Mrajis huyo anafafanua kuwa mafunzo hayo yatakuwa ni endelevu kulingana na mahitaji ya wadau. Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Chama Kikuu cha Akiba na Mikopo (SCCULT), Hassan Mnyone akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo anapongezwa kutungwa kwa sheria hiyo kwa kuwa inaenda kuongeza tija katika vyama vya kifedha kutokana na malengo ya kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha.

Anataja huduma hizo kuwa ni kutoa riba na gawio, kutoa taarifa na takwimu zinazohusu uendeshaji wa taasisi kwa wakati pamoja na kuweka utaratibu wa ukusanyaji wa madeni.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Agnes Lubuva

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi