loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dola mil 1.5 kuboresha lishe kanda ya kati

SERIKALI ya Japan imetoa Dola za Marekani milioni 1.5 kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) kuunga mkono mradi wa miaka minne wa Boresha Lishe wa maeneo ya vijiji vya kanda ya kati nchini.

Mradi wa Boresha Lishe uliozinduliwa mwaka 2017 unalenga kuimarisha lishe kwa wanawake na watoto 30,000 kwa kuhamasisha mabadiliko chanya ya tabia za lishe, kuhimiza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na ugawaji wa chakula lishe maalumu kwenye wilaya za Bahi na Chamwino kwa Mkoa wa Dodoma, na wilaya za Ikungi na Singida Vijijini kwa Mkoa wa Singida.

“Kwa hapa Tanzania, Serikali ya Japan imekuwa ikitoa misaada kwa sekta mbalimbali,” alieleza Balozi wa Japan nchini, Goto Shinichi.

“Mchango huu maalumu umetolewa kwa ajili ya wanawake na watoto wa vijijini, kwa ajili ya kuunga mkono kaulimbiu ya ‘Hakuna kumwacha mtu nyuma’ ya Mpango wa Maendeleo Endelevu wa 2030 kwa kuzingatia dhana ya msingi ya usalama wa mwanadamu. Msaada huu utasaidia kuboresha lishe na kuongeza kipato kwa makundi haya maalumu,” alifafanua Balozi Shinichi.

Mradi wa Boresha Lishe unajikita kwenye kuongeza uelewa kuhusu masuala ya lishe, upatikanaji wa vyakula mchanganyiko na usafi maji, mtu binafsi na mazingira (WASH).

Pia unajengea uwezo jamii wa namna ya kuongeza uhakika wa lishe na chakula kwenye kaya kwa kufuga wanyama wadogo, kulima mazao mchanganyiko na kuwaunganisha wanawake kwenye vikundi vya akiba na mikopo vijijini (Vicoba) ili kusaidia upatikanaji wa mitaji.

Kwa ushirikiano na Japan, WFP inasambaza na kuweka vibanda vya huduma za umeme wa jua kwa vikundi 40 vya Vicoba vinavyosimamiwa na mradi huu wa Boresha Lishe.

Vibanda hivyo vinatoa huduma za kuchaji simu na vifaa vingine vya umeme kwa malipo kidogo, na hivyo kuongeza kipato kwa Vicoba na wanachama wake.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi