loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Matumaini yamerejea, Watanzania tuchape kazi

WATU wa makundi tofauti wamezungumzia hotuba ya Rais Dk John Magufuli aliyoitoa Jumapili iliyopita akiwa mkoani Geita kwamba imeleta matumaini mapya.

Tayari shangwe na vigelegele vimesikika kwa wamiliki wa shule na vyuo, wamiliki wa baa, hoteli, wanamichezo na wafanyabiashara kutokana na kuwepo kwa dalili za wazi kabisa kwamba karibu maisha yanarudi kama yalivyokuwa awali.

Aidha viongozi wa dini kwa upande wao wamesema wamepokea kwa mikono miwili ombi la Rais Magufuli la kutenga siku tatu za ibada ya kumshukuru Mungu kwa matendo makuu aliyofanyia taifa katika vita dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Rais alihutubia taifa baada ya kushiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Chato mkoani Geita, ambapo alisema Mungu amejibu maombi waliyofanya Watanzania wakimuomba aliponye taifa dhidi ya maambukizi ya Covid-19, kwani sasa maambukizi na vifo vimepungua kwa kiwango kikubwa.

Tunaungana na Watanzania wote kufurahia hatua ya Taifa letu kuanza kurejea katika hali ya kawaida baada ya kusimama kwa baadhi ya shughuli baada ya ugonjwa wa corona kuripotiwa kuingia nchini katikati ya Machi, mwaka huu.

Tunafarijika kuona kuwa pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari lakini wananchi wameongeza bidii ya kushiriki katika mipango ya uzalishaji mali kama alivyoelekeza Rais kuanzia mashambani, viwandani, maofisini na katika maeneo mengine.

Tayari viongozi wa makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wamiliki wa shule, vyuo, wanamichezo na wafanyabiashara wameeleza kufurahishwa na hatua ya Rais Magufuli kufikiria kuruhusu shughuli mbalimbali zilizokuwa zimesimama kuendelea ikiwemo michezo kutokana na kupungua kwa maambukizi ya vifo.

Ni matumaini yetu kwamba baada ya Rais kutoa ahadi ya kuruhusu shughuli mbalimbali kurejea katika hali ya kawaida, wananchi wataendelea kuchukua tahadhari ili kuliepusha Taifa kurejea katika hali ya awali ya maambukizi.

Ili kuweza kufanikiwa katika hilo, wananchi waendelee kuzingatia maelekezo ya wataalamu ikiwemo kuepuka misongamano, kuosha mikono kwa maji yanayotiririka kila mara, kutumia vitakasa mikono, na tahadhari nyingine zote ambazo wamekuwa wakizichukua.

Licha ya hatua hizo ni vema pia wananchi wakaendelea kutumia tiba na kinga za asili kama kujifukiza kwa miti mbalimbali, kutumia malimao, tangawizi na vitunguu saumu, kwani tayari upo ushahidi kwamba njia hizo zimethibitisha kuwa na msaada mkubwa katika kukabiliana na makali ya virusi vya corona kwa kuvitokomezea mbali na mgonjwa kupona kabisa.

JANA gazeti hili liliongozwa na habari kuu iliyobeba kichwa cha ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi