loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli na ‘nguvu ya mamba’, Nyerere na NAM

RAIS John Magufuli ndiye habari ya mjini na zaidi duniani hivi sasa. Hatua thabiti, msimamo imara, maono makubwa na diplomasia ya hali ya juu aliyoonesha katika vita dhidi ya virusi vya homa kali ya mapafu, Covid 19 vimemnyanyua. Siyo kwamba amekuwa habari ya mjini kwa kuwa ndiyo kaanza urais jana au juzi. Hapana.

Ni kwa sababu sasa anaongoza dunia kwa maono makubwa akiwaburuza hadi wazungu.

Huko nyuma kumekuwa na dhana potofu kwamba kila maono mazuri, uvumbuzi, utafiti wa kupigiwa mfano lazima uwe umefanywa na Mzungu au kwa usimamizi wa mtu mwenye ngozi nyeupe.

Lakini Mungu si Athumani. Covid 19 imeacha maajabu ya mwaka 2020 kwa Rais Magufuli kuongoza kwa busara, hekima, vita dhidi ya Corona kwa kukataa kufungia Watanzania ndani kudhibiti maambukizi akitofautiana na viongozi wa nchi nyingi duniani yakiwemo mataifa makubwa ya Ulaya na Marekani na hata Afrika walioamua kuwafungia raia wao.

Pia Rais Magufuli amejizolea umaarufu kwa kuwa wa kwanza kunusa harufu ya mchezo mchafu kuhusu ubora wa vifaa vya kupimia virusi vya corona akidai vina mushkeli na hata takwimu zinazotolewa zilikuwa haziakisi ukweli.

Rais huyo mwenye shahada ya Falsafa ya Kemia (phd) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye pia kitaaluma ni mwalimu wa masomo ya sayansi, ametumia vyema uzoefu wake wa utafiti wa kisayansi alioufanya chuo UDSM na Chama cha Ushirika Nyanza alikokuwa mkemia kwa kuagiza sampuli za wanyama na matunda zipimwe ambapo ilibainika vipimo vina hitilafu.

Hofu yake kuhusu vipimo vya corona ilikuja kuthibitishwa pia na wanasayansi wa Uingereza walioshitukia vipimo hivyo na kupeleka sampuli za corona maabara za Marekani ili kujiridhisha.

Ni wazi Rais Magufuli alikuwa ameishtua dunia na zaidi wanasayansi kwa kuwa wa kwanza kudai vipimo vya corona haviakisi ukweli kwa kila wakati kuonesha watu wameambukizwa.

Aligonga zaidi vichwa vya habari kwa kufanya Shirika la Afya Duniani (WHO) likubaliane naye dhana yake ya kukataa kufungia watu ndani na badala yake kuwaacha waendelee na kazi lakini wakichukua tahadhari ili uchumi usilale kabisa.

Halikadhalika WHO imeungana naye pale aliposema kuna haja ya kujiunza kuishi na ugonjwa huu kama dunia ilivyojifunza kuishi namagonjwa mengine kama surau na ukimwi.

Baada ya miezi mitatu na ushee, nchi nyingi za Afrika, Marekani na hata Jumuiya ya Ulaya (EU) zimefuata nadharia yake na kuagiza watu wao sasa waendelee kufanya kazi kwa tahadhari baada ya kubaini utaratibu huo una matatizo kwani unafanya wasizalishe mali na kutegemea kupewa fedha na chakula na serikali ambavyo haviwatoshelezi hivyo maisha kuwa magumu.

Pia nadharia zinaonesha kwamba kuwafungia ndani watu pia kunaweza kuwapunguzia kinga za mili yao, tofauti na wanapokuwa huru.

Wakati Sweden ikikubaliana naye kutofungia watu, Rais wa Marekani, Donald Trump naye alikubaliana naye akitaka watu waendelee na uzalishaji mali akipingana na wapinzani wake, Democrats waliotaka waendelee kufungiwa na kupitisha muswada wa fedha zaidi za kujikimu.

Matokeo yake yamekuwa ni watu waliokataa kuvumilia kuingia mitaani wakilazimisha kifungo kiondolewe wakikubaliana na Rais Magufuli kumtanguliza Mungu kwa maombi ili kushinda. Wakati serikali za majimbo mengi Marekani pia zikilegeza masharti ili watu waendelee kuzalisha, Afrika Kusini, Rais Cyril Ramaphosa amebanwa na kusema yuko tayari kushitakiwa na ambao wanadhani kufungia watu ndani si mwafaka.

Huko Kenya moto umewaka kwa makundi ya watu kuingia mitaani kudai wasifungiwe baada ya zoezi la kuwapa chakula na fedha kutoenda vizuri licha ya nchi hiyo kuwa moja ya nchi za Afrika zilizokopeshwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) dola bilioni moja kwa ajili yao.

Ni wazi, nadharia ya Rais Magufuli kutofungia watu, kuagiza wamwombe Mungu siku tatu awaepushe na corona na kumshukuru pia kwa kusikiliza kilio chao, kutaka wanywe na kujifukize dawa za asili, kutofunga mipaka na majirani imethibiti.

Amethibitisha kuwa anaona mbali na Afrika inaweza kutoa viongozi wanaoweza kuongoza dunia kwa maono makubwa ya kusaidia nchi nyinginezo.

Ndio maana haishangazi mtandao mmoja ulipoandika ‘Magufuli anapoona mbali zaidi akiwa amekataa yale ambayo WHO na wengine wanayaona baadaye wakiwa wima.’

Anaendeleza rekodi za Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere aliyeongoza mapambano ya vita ya kupigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), kuundwa kwa Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika (AU), mwanzilishi wa Nchi Zisizofungana na Upande wowote (NAM) na Tume ya Kusini.

Nyerere aliondoka akiacha rekodi ya kuwa mmoja wa watu mashuhuri duniani, jasiri walioongoza mapambano yenye sifa ya kimataifa kukomboa nchi, watu kutoka ukoloni, ukoloni mamboleo, umaskini na madeni yao.

Alizipigania nchi maskini duniani akianzisha Tume ya Kusini iliyopigania maslahi ya nchi hizo akitaka zifutiwe madeni na nchi tajiri na hadi anafariki, alikuwa amefanikiwa kiasi kikubwa.

Wanaokumbuka umakini wake hata katika diplomasia ya kimataifa wanajua alivyoweza kushawishi Rais Frederick Chiluba amwachie rais wa zamani wa Zambia, Keneth Kaunda aliyekuwa amegoma kula kwa Nyerere kwenda huko akisema anataka kula chakula na Kaunda.

Wanajua Dk Salim Ahmed Salim aliyekuwa Katibu Mkuu OAU alivyotetemesha dunia kwenye uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kiasi cha kufanya UN iamue kumchagua Boutros Ghali wa Misri baada ya Marekani kumkataa mteule wa Nyerere, Dk Salim ikihofu nguvu ya Tanzania UN angepita.

Ni historia kama hiyo inaenda kujirudia sasa Rais Magufuli anavyozidi kujipambanua kama kiongozi mwenye maono makubwa, mtetezi wa maslahi ya Tanzania na dunia nzima akisisitiza umuhimu wa diplomasia kwa kusema hafungi mipaka yake I;I majirani wasije kufa njaa (hata kama wenyewe wanatangaza kuifunga yao) kwa kuzingatia jiografia ya Tanzania inayopakana na bahari.

Lakini nguvu, hekima, ujasiri, uzoefu, elimu ya rais Magufuli kufanya haya yote anaipata wapi? Makala haya yanalenga kuchambua asili ya nguvu hizo ikirejea historia yake katika siasa, mapito yake hadi alipofikia urais, changamoto alizopitia miaka hii mitano na nini kifuatacho

Wakongomani huwa wana usemi wa Kiswahili wa ‘nguvu ya mamba ku mayi’ wakimaanisha nguvu ya mamba iko majini yaani mamba ili aweze kumkamata mtu au mnyama ambaye ni windo lake, lazima awe ndani ya maji ndipo mkia wake uweze kuwa na nguvu ya kupiga na kumrusha.

Kama ilivyo kwa mamba wa Wakongomani, hata nguvu, uwezo, busara, hekima, ujasiri wa Rais Magufuli unatokana na vitu vingi vikiwemo elimu, taaluma ya ualimu, kupenda utafiti, ujasiri, malezi, ucha Mungu, washauri wake, hazina ya viongozi wastaafu wanaomshauri, mahusiano yake na watu, viongozi wenzake.

Vingine ni dira ya uchumi wa viwanda, ujenzi wa miundombinu ya kimkakati, nidhamu, uimara vyombo vya ulinzi na usalama, kumcha Mungu, kupenda haki, kusimamia ukweli, mabadiliko ya siasa za kimataifa na kikanda.

Kwa ufupi, haiba nzuri ya Rais Magufuli katika uongozi wake inasadifiwa na mambo mengi. Je, ni vipi mambo yaliyotajwa hapo juu na mengine yanajiakisi katika utendaji wake kiasi cha kumpa sifa ndani na nje ya nchi. Usikose makala ijayo.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi