loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waislamu zingatieni wito wa Bakwata kujikinga na Corona

MFUNGO wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaelekea ukingoni, hivyo kutoa fursa ya kuswaliwa kwa swala ya Idd el Fitr mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki inayokuja; na hiyo ni kulingana na kuandama kwa mwezi, kama ilivyo ada ya taratibu za dini hiyo.

Katika kuitekeleza ibada hiyo, Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti wametoa rai kwa waumini wa dini ya Kiislam, kuhakikisha wanaswali swala hiyo katika misikiti ya karibu na maeneo yao na hiyo ni baada ya kusitishwa kwa utamaduni wa kuswali swala hiyo viwanjani, kama tahadhari dhidi ya Corona.

Kwa mujibu wa viongozi hao wa Bakwata, Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zuberi na Shehe wa Mkoa wa Dar es Slaam, Alhad Mussa Salumu, kuswali swala hiyo katika misikiti ya karibu na maeneo wanayotokea waumini hao ni tahadhari kwa ugonjwa huo na kuitikia wito wa serikali wa kuepuka misongamano.

Ikumbukwe kuwa moja ya ushauri unaotolewa na wataalam wa afya ni muhimu wananchi kupeana nafasi, kama njia moja wapo ya kuepuka kuenea kwa ugonjwa huo, ambao tayari umeshapoteza maisha ya maelfu ya watu duniani kote, huku chanjo pamoja na tiba yake ikiwa bado haijapatikana hadi hivi sasa.

Katika kuhakikisha hilo linazingatiwa na mambo mengine yanayotolewa kama ushauri na wataalamu hao wa afya, viongozi hao wa Bakwata pia wamewashauri waumini wote kuvaa barakoa pindi wanapokwenda kuswali swala ya idd, lakini pia kuchukua ‘udhu’ majumbani mwao, bila kusahau kunawa mikono wanapofika msikitini au kupaka vitakasa mikono.

Binafsi nawapongeza viongozi wa Bakwata, kwa kutoa tahadhari hiyo hususani wakati huu ambapo taifa letu linazidi kuchukua hatua kadhaa za kukabiliana na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa Rais Dk John Magufuli, maambukizi ya ugonjwa huo yanazidi kupungua siku hadi siku, lakini amekuwa akisisitiza watanzania wote tuzidi kumuomba Mungu aendelee kutuepusha.

Tunaamini kuwa kila kitu kinawezekana, hasa kunapokuwa kuna nia ya dhati juu ya jambo hilo. Kuchukua tahadhari na kufuata ushauri mbalimbali, unaotolewa na wataalam wa afya na viongozi wetu, kutasaidia kuliacha taifa salama.

Ikumbukwe kuwa Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele, kwa kuwataka wananchi kuchukua tahadhari na kusisitiza kuwa ugonjwa haupaswi kuogopwa kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa mwenye mamlaka nao hadi sasa ni Mungu.

Watanzania hatupaswi kuwa waoga na corona, lakini jambo kubwa tunapaswa kumuomba Mungu usiku na mchana kila mtu kwa imani yake ili atuepushe nao wakati huu, ambao hata Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema huenda ukawa sehemu ya maisha yetu kwa kipindi kirefu.

Nimalizie kutoa rai kwa Watanzania na wananchi wote, kutekeleza agizo la kuchapa kazi la Rais Magufuli ili kuzidi kuujenga uchumi wa taifa hili, ambalo linapambana kujiinua kimaendeleo, likitekeleza miradi mbalimbali mikubwa ikiwemo ya kimkakati, kama moja ya hatua hizo za kujiimarisha kiuchumi.

KAMPENI za uchaguzi kwa ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi