loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vitunguu saumu, limao na tangawizi zinavyosaidia kukabili corona

UWEZO wa mwili kupambana na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) maarufu kama corona unategemea hali ya afya na lishe ya mtu.

Mwili wa mtu mwenye afya na lishe bora, huwa na uwezo mkubwa wa kupambana na maambukizi ya virusi hivyo na hivyo, kumfanya mhusika kupata athari kidogo inapotokea amepata maambukizi.

Kinyume chake, hali duni ya lishe hudhoofisha kinga ya mwili na hivyo, mtu apatapo maambukizi ya virusi vya corona, mwili wake huwa na uwezo mdogo wa kupambana navyo hali inayosababisha kupata madhara makubwa kiafya ikiwemo kuchelewa kupona na baadhi ya waathirika kupoteza maisha.

Kimsingi, corona ni tatizo linaloshambulia karibu dunia nzima na ndiyo maana, wataalamu mbalimbali wanasema ili kukabili tatizo hilo na kupata ushindi halisi mapema, nguvu ya mshikamano inahitajika.

Hata hivyo, kama alivyonukuliwa Rais John Magufuli Jumapili iliyopita wakati akizungumza akiwa Chato, kutokana na mazingira tofauti, kila nchi pia ina mbinu za kupambana na tatizo hili ingawa umuhimu wa ushirikiano unabaki palepale.

Hii ni kusema kuwa, mbinu zinazotumika Marekani, Uingereza, Italia, Hispania au nchi yoyote duniani, siyo lazima hizohizo na kwa namna hiyohiyo zitumike katika nchi nyingine; mathalani Kenya, Burundi, Uganda, Zambia au Tanzania.

Hadi wakati makala haya yanaandaliwa, takwimu kutoka vyanzo mbalimbali vikiwamo vya kimtandao zilikuwa zinaonesha kuwa, duniani kote kumeripotiwa wagonjwa 4,989,095 na vifo 324,966.

Waliopona ni 1,959,260. Nchini Tanzania, takwimu zilizotolewa na serikali zinaonesha kuwa watu walioambukizwa virusi hivyo ni 509 huku watu 21 wakifariki dunia.

Baadhi ya dalili za ugonjwa wa Covid-19 ni pamoja na homa kali, mafua, kikohozi kikavu, mwili kukosa nguvu, vidonda kooni na kupumua kwa shida. Njia kubwa za kuepuka maambukizi ya virusi vya coroni ni hasa kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono, kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji tiririka kwa muda usiopungua sekunde 22, kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano, kukaa umbali usiopungua mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine na kuvaa barakoa.

Wataalamu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) wanasema, mtu yeyote anaweza kuambukizwa ugonjwa huu endapo hatafuata maelekezo ya wataalamu wa afya haijalishi kinga ya mwili wake ni imara au dhaifu, lakini madhara ya ugonjwa huo hutofautiana miongoni mwa watu.

Wanasema kupona kwa mtu husika kunategemeana na uwezo wa kinga yake ya mwili katika kupambana na maambukizi. Kinga hiyo inachangiwa na ulaji wa lishe bora kutoka katika makundi matano.

Makundi hayo ni ya vyakula vya asili ya nafaka, mizizi na ndizi mbichi ambavyo huupa mwili nishati lishe au nguvu na joto; kundi lingine ni la vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde vinavyoupatia mwili protini kwa wingi; kundi la mbogamboga ambalo huupa mwili madini na vitamini; kundi la matunda ambalo huupa mwili madini na vitamini na kundi la sukari, mafuta na asali ambalo huupatia mwili nishati lishe kwa wingi.

Pamoja na mambo mengine, wataalamu wa lishe wanasema ni muhimu kujua matumizi sahihi ya viungo na matunda katika kupambana na dalili ndogondogo zinazoambatana na maambukizi ya corona. Ofisa Utafiti wa TFNC, Victoria Kariathi anasema, ili kuimarisha kinga ya mwili wa binadamu, ni lazima ulaji wa matunda yenye vitamini C kwa wingi uzingatiwe sambamba na kula vyakula kutoka katika makundi yote matano.

Kariathi anasema yapo matunda mengi yenye vitamini C ambayo mtu anaweza kuyatumia katika kupambana na ugonjwa wa covid-19 na kuupatia mwili faida nyingine.

“Matunda yenye vitamini C kwa wingi husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuharakisha uponyaji. Aina za matunda haya ni kama mapera, maembe, mananasi, ukwaju, mabungo, ubuyu, zabibu na jamii ya machungwa kama vile machenza, machungwa, malimao, ndimu na madalansi,” anasema Kariathi.

Anafafanua kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwamba matumizi ya matunda yenye vitamini C kwa wingi huzuia au kutibu Covid 19, lakini ni dhahiri hupunguza baadhi ya dalili zinazotokana na ugonjwa huo sambamba na kuboresha kinga ya mwili.

“Watu wamezoea matunda yenye vitamini C kwa wingi ni malimao na machungwa, lakini matunda yapo mengi sana ambayo yanapatikana kwenye jamii zetu na yana virutubisho vingine muhimu ikiwemo vitamini A, D na madini ya Calcium na Manganese ambayo ni muhimu katika kuimarisha kinga mwili,” anasisitiza.

Pia anasema matumizi sahihi ya matunda hayo yanapaswa kuzingatiwa hivyo, wanashauri kutumika zaidi kwa matunda halisi kuliko sharubati (juisi) kwani mtumiaji atapata faida nyinginezo katika tunda husika kama vile nyuzinyuzi. Anasema endapo matunda hayo yatachemshwa kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza vitamini C iliyopo hivyo, inashauriwa kula matunda na sharubati bila kuchemsha.

“Kwa mfano mtu ana vidonda vya tumbo na anaona hawezi kunywa sharubati ya limao isiyochanganywa na kitu chochote au kula tunda lenyewe, anashauriwa kula matunda mengine yenye vitamin C kwa wingi kama mapera, machungwa, zabibu na mengine,” anaeleza Kariathi.

Anaongeza: “Endapo utatengeneza sharubati, epuka kuongeza sukari na ikiwezekana usiichuje ili kupata faida nyingine. Pia, inashauriwa kula matunda haya mara kwa mara kwani vitamini C ni kati ya vitamini ambazo huyeyushwa na maji na haihifadhiwi mwilini kwa muda mrefu.”

Mtaalamu huyo anasema inashauriwa kutumia matunda hayo kwa kiasi kwani yana tindikali ambayo huweza kuleta madhara mwilini. Limao Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe wa TFNC, Sikitu anasema unapokata kipande cha limao na kuchanganya kwenye chai ya moto kuna uwezekano mkubwa wa kuondoa vitamini C vilivyopo.

“Tunashauri limao liliwe kama tunda... pia unaweza kukamua na kunywa maji yake. Unapotumia maji ya moto ile vitamini C iliyopo inaharibika hivyo unapata virutubishi vingine. Tungependa kama mtu anataka kula limao au ndimu, basi alitumie kama lilivyo,” anasema.

Mdalasini Akielezea matumizi ya viungo katika kukabiliana na ugonjwa huo, Kariathi anasema miongoni mwa viungo ni mdalasini ambao hutokana na magome ya mmea wa mdalasini.

Anasema mdalasini hutumika bila kusagwa au kwa kusagwa na wanasayansi wanaamini harufu nzuri iliyopo kwenye mmea huo, hutokana na chembechembe zenye faida kubwa kwa afya ikiwemo kuboresha kinga ya mwili na kupunguza baadhi ya dalili au athari za corona.

Anazitaja faida zitokanazo na mmea huo kuwa ni pamoja na kupunguza baadhi ya matatizo katika mfumo wa chakula kama vile kichefuchefu, kutapika na kuharisha, kupunguza baadhi ya vimelea vya aina ya bakteria na virusi na kuondoa chembechembe za sumu kutokana na uwepo wa viondoa sumu (antioxidants).

“Tumia kiasi kidogo cha mdalasini kwenye kinywaji kilichochemshwa kama chai au kwenye chakula. Inashauriwa kutumia kijiko kimoja cha chai kwa siku na ili kupata faida za ziada, unaweza kuchanganya na tangawizi na asali,” anasisitiza Kariathi.

Tangawizi Ofisa huyo anasema tangawizi imekuwa ikitumika kama sehemu ya matibabu ya magonjwa mbalimbali maeneo kadhaa ya Asia, India na Ulaya kutokana na uwepo wa kemikali ya Gingerol.

Anasema tangawizi hutumika kuboresha kinga ya mwili pamoja na kupunguza madhara ya dalili za maambukizi ya corona.

“Hutumika kupunguza dalili za mafua, mchafuko wa tumbo, maumivu ya mwili na misuli, kichefuchefu kwa wajawazito wenye saratani na baada ya upasuaji na kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa na bakteria na baadhi ya virusi wanaoshambulia mfumo wa hewa,” anaongeza.

Anasema mtu mzima anatakiwa kutumia tangawizi kwa saizi ya kidole cha mkono, kutumia ikiwa mbichi, iliyokaushwa au sharubati yake ama kuongezea kwenye chai au chakula.

Kitunguu saumu Vyanzo mbalimbali vinakielezea kitunguu saumu kuwa chenye kemikali ya sulfa hususan ‘allicin’ inayokipa uwezo wa kutumika kama tiba na kwamba, kemikali hiyo hupatikana pale kitunguu saumu kibichi kinapokatwa, kupondwa au kutafunwa.

Kinasaidia kuboresha kinga mwili na kupunguza dalili zinazoambatana na maambukizi ya virusi hivyo. Kariathi anasema, kitunguu saumu kinatumika zaidi katika kuzuia au kutibu magonjwa ya mafua kwani asilimia 60 hadi 70 ya watu waliotumia vitunguu saumu walipunguza muda wa kuonesha dalili za mafua kutoka siku tano hadi 1.5.

“Kinaweza kurekebisha shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo kwa kupunguza kiwango cha lehemu, na maambukizi yatokanayo na bakteria. Husaidia uyeyushaji na ufyonzaji wa chakula na kuzuia kuharisha,” anasema na kuongeza: “Kitunguu saumu kinaweza kutumika kwa kuongezwa kwenye vyakula vya aina mbalimbali ili kuongeza ladha na inashauriwa mtu mzima asitumie zaidi ya punje sita kwa siku.”

Mchaichai Mmea huu hutumika kutengeneza dawa kwa magonjwa mbalimbali kutokana na wingi wa viondoa sumu, virutubishi vingine kama vile vitamini C na A. Hata hivyo, hakuna ushahidi kwamba mchaichai unaweza kuzuia maambukizi ya virusi vya corona au kutibu ugonjwa wa covid-19, bali hutumika kuimarisha kinga mwili na kupunguza dalili na madhara ya corona.

“Husaidia kupunguza dalili za mafua na homa, kupunguza baadhi ya vimelea vya aina ya bakteria na fangasi, kuondoa chembechembe za sumu mwilini, kusaidia mmeng’enyo wa chakula na kuchochea ufanyaji kazi wa mwili na kutumia mafuta,” anasema Ofisa huyo.

Asali Hii imekuwa ikitumika kutibu maradhi mbalimbali kutokana na wingi wa viinilishe vya aina tofauti vyenye faida ya lishe na tiba pia kuimarisha kinga mwili.

Wanga uliopo kwenye asali humeng’enywa kwa urahisi na hivyo, husaidia kuwapatia nishati watu wenye matatizo ya kumeng’enya chakula na kwamba uwepo wa madini ya chuma, shaba na manganese husaidia kutengeneza chembechembe za damu mwilini na hivyo, kuzuia upungufu wa damu.

Kati ya faida nyingi zitokanazo na asali ni pamoja na kuzuia upungufu wa damu, kusaidia kutibu magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na kikohozi kikavu, kuzuia vijidudu, kutibu vidonda na baadhi ya magonjwa ya mfumo wa chakula, kudhibiti uwiano mzuri wa lehemu mbaya na nzuri katika damu na ni dawa ya usingizi kwa wenye matatizo ya kupata usingizi.

Jamii inasisitizwa kuendelea kutumia matunda na viungo hivyo ili kuimarisha kinga mwili na kupunguza dalili na kudhibiti magonjwa nyemelezi yatokanayo na maambukizi ya virusi vya corona.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi