loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Silaha za JPM zinazoinua Tanzania vita ya Corona

RAIS John Magufuli amewaomba Watanzania kupitia viongozi wa dini kufanya ibada ya shukurani kutokana na matendo makuu ambayo Mungu amelifanyia taifa kwa kuliponya na corona.

Ameomba ibada ifanyike siku tatu kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili wiki hii. Ibada hiyo inalenga kumshukuru Mungu kwa kujibu maombi ya siku tatu yaliyofanyika hivi karibuni kuomba aliponye taifa dhidi ya maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid- 19).

Watanzania wa dini na madhehebu walitumia siku tatu kuanzia Aprili 17 hadi 19 kufunga na kuomba. Ilifuatia ibada maalumu ya kitaifa iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam ikishirikisha viongozi wa dini zote kwa ajili ya kuombea nchi dhidi ya maambukizi ya corona.

Msingi wa maombi ya shukurani unatokana na taarifa ya Rais Magufuli kupitia hotuba ya hivi karibuni aliyoitoa aliposhiriki ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Chato mkoani Geita, kwamba maambukizi na idadi ya wagonjwa imepungua.

Lakini pia, kiwango cha maambukizi ni tofauti na makisio yaliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa kuanzia katikati ya Aprili, Tanzania ingekuwa na wagonjwa wengi wa Covid-19.

Msimamo wa Rais Magufuli wa kushirikisha wananchi kumtanguliza Mungu katika mapambano dhidi ya corona, unavutia watu wengi wakielezea kuwa ni bahati kwa nchi kuwa na kiongozi anayeamini katika Mungu. “Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa na kiongozi mwenye hofu ya Mungu.

Tunamwona ni kiongozi ambaye atatuvusha… Anamtanguliza Mungu, ni unyenyekevu mkubwa na ni bahati kubwa,” Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini (Tudarco), Profesa Andrew Mollel anasema.

Anasema wapo baadhi ya viongozi wa nchi hujigamba na vyombo vya ulinzi na usalama wakiamini ndiyo ulinzi tosha. Lakini kwa Rais Magufuli, Profesa Mollel anasema licha ya kwamba pia yeye anavyo hivyo vyombo, amekuwa kiongozi anayemtanguliza Mungu.

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma anashukuru namna ambavyo viongozi wa dini wameshirikishwa tangu mwanzo katika mapambano dhidi ya Covid-19.

“Sisi tunashukuru sana nafasi ya viongozi wa dini imekuwa kubwa tangu mwanzo… Rais ameendelea kututia moyo sisi viongozi wa dini na wananchi kwamba tukimtegemea Mungu mambo yanawezekana,” anasema.

Akirejelea hotuba za Magufuli ambazo amekuwa akihimiza wananchi kumtanguliza Mungu katika vita hii, Mruma anasema Rais ametoa ujumbe wa matumaini unaosaidia kupambana na ugonjwa bila hofu. Anakiri kwamba kupitia kwa Rais Magufuli, ipo nguvu ya matumaini iliyopatikana kutokana na ibada na sala zinazoendelea kwenye nyumba za ibada.

Katika kufanyia kazi ombi la kufanya ibada ya shukurani, Bakwata ilitoa maelekezo kwa mikoa kuhakikisha swala za jamaa misikiti yote zinaendana na maombi ya kumwomba Mwenyezi Mungu kuipusha nchi na corona kwa kuleta dua maalumu iitwayo kunuti katika kila swala.

Shehe Sharrif Abdulqadir al-Ahdal, ambaye ni Rais wa Taasisi ya Alhikma Foundation, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwawezesha Waislamu kufunga Ranadhani na kusali misikitini.

Amekuwa akiwataka waumini kutumia kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani kuzidisha dua akiamini Mungu ataondoka kabisa corona Tanzania. Mtume na Nabii, Manfred Kashasha wa Kanisa Sauti ya Uhuru Shangwe Habari Njema (RHMI) lililopo Kigamboni, Maweni Dar es Salaam anaeleza furaha ya nchi kuwa na kiongozi anayemtanguliza Mungu katika kipindi kigumu kama hiki.

“Tangu Mwanzo niko naye kwa maana kumtegemea Mungu katika kupambana na hili. Kwa binadamu pekee hatuwezi. Nimekuwa naye bega kwa bega katika kumwombea Rais wetu,” anasema Kashasha.

Kiongozi huyu wa dini anakiri kwamba maombi yamesaidia nchi na watu kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kuua hofu iliyokuwa imefunguliwa milango hivyo kusababisha maradhi mengine. Kashasha anasimamia taarifa za kitaalamu kama ilivyowahi kuelezwa na na mtaalamu wa utoaji elimu ya juu ya covid-19 kutoka Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dk Tumaini Haonga.

Dk Haonga alisema msongo wa mawazo na wasiwasi uliopitiliza unasababisha kinga ya mwili kushuka na kuwa katika hatari ya kudhoofu endapo mhusika atapata maradhi yoyote. Mtume na nabii Kashasha anasisitiza kwamba kumtumaini Mungu kwa mafundisho, kinga ya mwili inakuwa katika hali nzuri.

“Ni jambo la kumshukuru sana Mungu kwamba rais wetu amekuwa msomaji wa maandiko juu ya namna Mungu anavyotusaidia… Rais amewapa watu matumaini.”

Samson Mwigamba ni mwanachuo wa mwaka wa Kwanza, Shahada ya Uzamili katika Sayansi, Uhasibu na Fedha katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambaye pia anaeleza anavyofarijika na namna Rais anavyomtegemea Mungu.

“Nimefurahi rais anavyomtegemea Mungu. Sisi tumejifunza wafalme waliotambua ukuu wa Mungu wamefanikiwa sana. Nimefurahishwa kwamba baada ya maombi sasa turudi kwenye shukurani,” anasema Mwigamba akisisitiza kiongozi mwenye hofu ya Mungu ni tuzo kwa wananchi.

Chama cha Demokrasia (DP) kinaeleza bayana kinavyoguswa na namna Rais Magufuli anavyoliinua taifa kwa kumtanguliza Mungu hususani katika kipindi hiki cha vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Mwenyekiti wa DP, Georgia Mtikila anaeleza miongoni mwa mambo yaliyosukuma chama kutangaza kutosimamisha mgombea katika uchaguzi mkuu mwaka huu, badala yake kinamuunga mkono Magufuli, ni kutokana na kumtanguliza Mungu.

Wakati Rais Magufuli alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi kusimama na kubainisha msimamo wake wa kumtanguliza Mungu katika suala zima la mapambano dhidi ya Covid-19 kwa kuelekeza maombi ya kitaifa, amefuatiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye hivi karibuni alikaririwa akiwaambia Wamarekani kwamba pia wamwamini Mungu, wataweza kushinda vita hiyo.

Aliposhiriki Ibada ya Ijumaa Kuu, Rais Magufuli alisema maombi yanaweza kulivusha taifa katika janga hili; Kauli ambayo pia Trump anaisimamia kama alivyonukuliwa hivi karibuni wakati akitoa tamko la siku ya maombi akihimiza Wamarekani kumtanguliza Mungu.

Trump alitangaza Mei 7, 2020, kama Siku ya Maombi ya Kitaifa kwa kuhimiza Wamarekani wote kuiadhimisha kwa kuzingatia umuhimu wa maombi na baraka ambazo taifa hilo limepokea.

Kwa mujibu wa Trump, mwaka 1988, Bunge, kwa Sheria ya Umma 100-307, kama ilivyorekebishwa, lilitaka Rais kutangaza kila Alhamisi ya kwanza Mei kama Siku ya Maombi ya Kitaifa ambayo watu wa Marekani wanaweza kumgeukia Mungu kwa maombi makanisani, vikundi na watu binafsi.

Trump alielezea umuhimu wa kumtanguliza Mungu akirejelea historia ya taifa hilo kwamba, tangu zamani, utegemezi wao kwa Mungu umewawezesha kutafuta ushauri na hekima ya kimungu.

Anataja viongozi waliopita mara nyingi walihimiza wananchi kutafuta hekima kutoka kwa Mungu na wakagundua nguvu yake inavyoongoza taifa. Alitoa mfano wa wakati wa utawala wa George Washington alipotangaza siku ya kitaifa ya kufunga na kusali kwa unyenyekevu kuomba radhi ya Mwenyezi Mungu kutokana na uharibifu mkubwa uliotokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Alitaja viongozi wengine akiwamo Rais Lincoln na Reagan walivyobaini nguvu ya maombi katika historia ya Marekani. “Leo, kama kawaida, utamaduni wetu wa maombi unaendelea wakati taifa letu likipambana na virusi vya corona…kwa hiyo tunapaswa kutafuta hekima na nguvu ya Mungu,” alisema Trump.

Hekima, imani na nguvu ya ki-Mungu anayoonesha Rais Magufuli kiasi cha kutoamuru kufungwa kwa nyumba za ibada, ndiyo inaendelea kumuinua mbele ya watu wa kada tofauti na mataifa na kuifanya vita ya Tanzania dhidi ya Covid-19 kuwa ya tofauti.

“Inafurahisha kuona sisi kama taifa huru tumeweza kutumia model (mtindo) yetu…hatuwezi kuamrishwa na mtu kufungia watu, Rais ameangalia njia zinazoendana na mazingira yetu,” anasema Mwigamba.

Hamasa juu ya ibada na maombi, kuhimiza tiba mbadala ikiwamo kujifukiza, kutofungia watu ndani na hotuba zinazoodoa hofu za Rais Magufuli, zinatajwa na watu wa kada mbalimbali kwamba zinaipambanua na kuiinua Tanzania kati kati ya vita dhidi ya corona.

Viongozi wa dini, wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaida kama walivyonukuliwa na makala haya, wanamtaja Rais Magufuli kuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu atakayeivusha nchi kwenye janga hili.

Anatajwa kuwa kiunganishi cha Watanzania kwa kufanikisha watu wenye imani tofauti kuungana na kuinua mioyo yao kwa Mungu kuomba akomeshe janga huku wakiendelea kuzingatia maelekezo ya wataalamu bila hofu wala taharuki.

Kwa umoja huo wa dini na madhehebu mbalimbali, taifa linaendelea wiki na ibada ya kumshukuru Mungu wiki hii kwa kujibu maombi yaliyowezesha maambukizi ya corona kupungua nchini.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi