loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM: Ukitoa vifaa vyenye corona kesi ya jinai

RAIS John Magufuli ametoa maagizo kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na watendaji wengine, kutopokea vifaa vya kupambana na virusi vya corona vinavyogawiwa kwenye taasisi na watu mbalimbali, bali lazima vipitie wizarani na vihakikiwe ubora wake.

Amesema kwenye vita dhidi ya corona, upo uwezekano wa kupandikizwa virusi kupitia vifaa hivyo; na kwamba yeyote anayetoa vifaa vya msaada na baada ya kupimwa, vikakutwa na virusi vya corona, atafunguliwa mashitaka ya jinai na ikiwezekana kesi ya mauaji.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana jana Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali sita aliowateua hivi karibuni wakiwamo mabalozi watatu, naibu waziri, Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Lazima tukubali kwamba corona bado ipo na lazima tuchukue tahadhari, ni kweli kwamba imepungua nchini, na ugonjwa huu ni vita na katika vita kuna mbinu nyingi… unaweza letewa hata barakoa zenye corona kupitia vifaa hivi, vitu vya bure vinaua, kama ni kuvipokea vipitie Wizara ya Afya na vihakikiwe,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hilo linawezekana, kwani nchi imechukuwa hatua mbalimbali za kukabiliana na janga hilo na sasa iko kwenye hatua nzuri, kwani maambukizi yamepungua zaidi, na hiyo ni vita na kwani nchi iko kwenye hali nzuri kwa sasa kutokana na hatua hizo, hivyo ni lazima kuwa makini na vifaa vya misaada vinavyotolewa.

Aliongeza kuwa serikali itanunua vifaa vilivyopimwa na kuhakikiwa kabla ya kuingia nchini, lakini pia vikifika nchini vitapimwa tena kwenye maabara ya ndani, kuhakikisha ubora wake ili kuhakikisha ubora wake kwa afya ya Watanzania na kusema lazima kwenye vita hiyo tahadhari ichukuliwe.

“Mtu akitaka kusambaza msaada wowote hatukatai, ila upelekwe Wizara ya Afya uhakikiwe, wizara simamieni hili, vya dezo vinaua, ila tunahitaji msaada na lazima tuhakiki kwanza kabla ya matumizi,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliipongeza Wizara ya afya na waziri wake, Ummy Mwalimu na kusema ni mmoja wa mawaziri anayefanya kazi vizuri na katika hilo la corona ameonesha ujasiri na kuchapa kazi vizuri kuliko hata wataalamu wa afya waliopo ndani ya wizara hiyo.

“Niipongeze Wizara ya Afya, waziri amefanya kazi nzuri sana…yeye ni mwanasiasa wala hana fani ya udaktari lakini anaongoza vizuri wizara hii na amesimamia janga hili kidete. Kuna wakati alibaki mwenyewe, ila hakuyumba akasimama imara, watendaji wengine tena wenye fani hiyo wapo tu walimwangalia, nasema kwa wazi wala simsemi mtu, ila meseji senti,” alisema Rais Magufuli.

Alisema anafikiria kutumia fedha zilizotolewa na Mfuko wa Global Fund, kutengenezea vifaa vya nchi kwa ajili ya kujikinga na corona. Alisititiza kwamba iwapo fedha hizo zitatumika vizuri kwenye eneo hilo, zitasaidia kutengeneza pia ajira na kuwa na vifaa vya kutosha vya kupambana na corona na vifaa vingine vya afya.

“Hivi sasa tunatengeneza vifaa vya kujikinga na corona (PPE) pale Muhimbili, wizara imefanya kazi nzuri na hata Jeshi la Magereza nao, sasa nafikiria hata zile pesa tulizopewa na Mfuko wa Global Fund tutazitumia kwenye utengenezaji wa vifaa hivyo ili tuwe na vyetu wenyewe, vitusaidie,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema ndani ya wiki moja kuanzia sasa, wameruhusu ndege za watalii kutua nchini na watalii hao hawatawekwa karantini, bali watachunguzwa afya zao, kama wana viashiria vyovyote vya virusi vya corona, kisha wataenda kutalii kwenye maeneo yaliyoyapenda.

“Kuanzia Mei 27 na 28, mwaka huu tutaruhusu ndege za watalii kuja hatutawaweka karantini, niviombe vyombo vya ulinzi na usalama kuwapa ushirikiano na sio kuwakwamisha, tena wametoka vifungoni sasa wakifika huko kwenye utalii mnaweza mkawakaribisha kupiga nyungu (kujifukiza),” alisema Rais Magufuli.

Awali, aliushukuru Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Sweden kwa mchango wao wa fedha waliotoa Dola za Marekani milioni 63, kwa ajili ya kusaidia nguvu kwenye mapambano dhidi ya corona.

Akielezea msaada huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema nchi mbalimbani duniani zimeelewa hatua zinazochukuliwa na Tanzania kukabili virusi vya corona.

Profesa Kabudi alisema, “Wengi wameelewa hatua za Serikali ya Tanzania katika vita hii ya corona, jana (juzi) nimepokea simu kutoka Canada wanatupongeza kwa hatua na wamesema watatusaidia kwenye afya.”

Alifafanua kuwa EU wametoa mchango wao wa fedha wa Dola za Marekani milioni 38, Sweden wanatoa Dola milioni 20 kwenye elimu na Dola milioni 10 kwenye Mfuko wa Kusaidia Kaya Maskini katika Tasaf.

Akizungumzia kuapishwa kwa viongozi hao hususan kwa mabalozi, Profesa Kabudi aliwapongeza na nafasi hizo na kuwaeleza kuwa wamekabidhiwa jukumu la kupeperusha vyema bendera ya Tanzania nje.

“Niwapongeze kwa kuteuliwa kwenu na uapisho wa leo, basi mfahamu kwamba mnakwenda kumwakilisha Rais Magufuli huko mlikopangwa, mkatumike vizuri kwenye nchi mnazokwenda na kuhakikisha maslahi ya taifa na ushirikiano unaendelezwa,” alisema Profesa Kabudi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Watanzania wengi waliugua hofu na sio corona na kuitaka jamii kuacha kutishana, bali wachukue tahadhari huku wakitekeleza majukumu yao.

“Watu wengi waliugua hofu na sio corona, na tulishajiandaa kupanga vitanda Uwanja wa Sabasaba zaidi ya vitanda 1,000 tuwapeleke wagonjwa, lakini sasa hatuna wagonjwa wengi, na tumefuta mpango huo,” alisema Ummy, aliyekiri alipitia kipindi kigumu katika uongozi wake, lakini akasema amejifunza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo aliwataka watendaji hao hususan Katibu Tawala wa Pwani, Dk Delphina Magere, kuhakikisha anasimamia vyema majukumu yake.

Kuhusu vita dhidi ya corona, Jafo alisema wiki ijayo atazindua awamu ya pili ya kupiga nyungu (kujifukiza), kama njia mojawapo ya kukabiliana na virusi vya corona. Walioapishwa jana ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel (Mbunge wa Siha) aliyeteuliwa wiki hii na RAS Mkoa wa Pwani, Dk Magere.

Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Meja Jenerali Jacob Kingu, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Kamishna Phaustine Kasike, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, John Simbachawene na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi